LYON, UFARANSA
MSHAMBULIAJI wa timu ya taifa ya Ureno, Cristiano Ronaldo, amewataka mashabiki wa timu hiyo kujiandaa kushangilia ubingwa wa michuano ya Euro 2016 baada ya timu hiyo kuingia fainali ya michuano hiyo.
Timu hiyo imeingia fainali baada ya kushinda mabao 2-0 dhidi ya Wales kwenye mchezo wa nusu fainali juzi, huku mchezaji huyo akifunga bao moja na kusababisha bao la pili.
Staa huyo wa klabu ya Real Madrid, amedai kwamba Ureno ilianza katika mazingira magumu kwenye michuano hiyo tofauti na timu nyingine, lakini imefanikiwa kufika fainali na ina uwezo wa kutwaa taji hilo.
Ronaldo amedai kwamba timu hiyo imefikia historia ya miaka 12 iliyopita ambapo iliingia fainali mwaka 2004 kwenye michuano hiyo lakini ilitolewa na Ugiriki.
“Hii ni ndoto yetu ya kila mwaka kwa taifa letu, nadhani baada ya kumaliza fainali kila mmoja wetu atakuwa anacheka pamoja na machozi ya furaha kutokana na kile ambacho tutakifanya mbele ya mashabiki wetu.
“Siku zote ndoto zangu zinasema kutwaa ubingwa nikiwa na taifa langu, naona ndoto hizo zinakaribia na ninaamini kila kitu kitakuwa sawa mwaka huu kwa kuwa uwezo wa kufanya hivyo tunao.
“Siku zote ni vizuri timu ikaanza vibaya lakini ije kumaliza vizuri, ndivyo ilivyo na itavyokuwa kwenye mchezo wa fainali, kila mchezaji yupo kwa ajili ya kulitumikia taifa na ninaamini tupo tayari kufia uwanjani kwenye mchezo huo ujao.
“Mashabiki wakae tayari kushangilia ubingwa msimu huu, hii ni nafasi ya pekee kutangaza ubingwa, hivyo mashabiki wakae tayari kwa hilo,” alisema Ronaldo.
Hata hivyo, mchezaji huyo amedai kwamba Ureno si timu ya mtu mmoja kama watu wanavyodhani, ni timu ya wachezaji 11 hivyo kila mmoja anatakiwa kuonesha uwezo wake kwa ajili ya kupigania taifa lake.
“Si lazima nifunge bao japokuwa kufunga ni jambo muhimu na zuri, ila kila mchezaji ana jukumu lake la kuhakikisha timu inafanya vizuri na inasonga mbele, si timu ya Ronaldo,” aliongeza.
Bao la mchezaji huyo juzi lilimfanya aifikie rekodi ya mchezaji wa zamani wa timu ya taifa ya Ufaransa, Michel Platini, ambaye kwa sasa ni rais wa Uefa, nyota huyo alifunga mabao tisa hadi anamaliza soka lake mwaka 1984, wakati Ronaldo amefikisha idadi hiyo ya ufungaji bora wa miaka yote tangu pale alipoanza kucheza michuano hiyo mwaka 2004.