23.2 C
Dar es Salaam
Friday, April 19, 2024

Contact us: [email protected]

ROLLS ROYCE YAZINDUA GARI GHALI ZAIDI DUNIANI

Na JUSTIN DAMIAN,

KUENDESHA gari zuri la kifahari ni moja kati ya ndoto za binadamu wengi. Tatizo huja kwenye uwezo wa kununua gari hilo.  Lakini kwa wenye nazo si tatizo, wanapata kilicho bora kwa kutumia fedha zao.

Katika hali isiyo ya kawaida, kampuni maarufu ya kutengeneza magari ya kifahari zaidi duniani ya Rolls Royce, imezindua gari lake dogo aina ya Rolls Rorce Sweptail  linalouzwa Dola za Marekani milioni 13 sawa na Sh bilioni 29 za Kitanzania.  Wataalamu wa magari ya kifahari wanasema gari hilo ndio la gharama kubwa zaidi kuwahi kutengenezwa duniani.

Rolls Royce ni moja kati ya kampuni za kwanza kutengeneza magari ya kifahari na ambayo kipindi cha nyuma na hata mpaka sasa hutumiwa na viongozi wakubwa duniani. Mara baada ya Uhuru, Mwalimu Julius Nyerere alipewa gari aina ya Rolls Royce na Serikali ya Uingereza kwa ajili ya matumizi ya kiserikali. Kwa ambao wamepata nafasi ya kutembelea makumbusho ya taifa yaliyopo jijini Dar es Salaam, bila shaka watakuwa wamepata nafasi ya kuona baadhi ya magari aina ya Rolls Royce yaliyotumiwa na Serikali ya Mwalimu Nyerere

Gari hili jipya ambalo limewaacha midomo wazi watu wengi duniani ikiwamo matajiri wenye ‘pepo la magari ya kifahari’ limetengenezwa baada ya mteja binafsi ambaye hakutaka kutajwa jina lake kusema yupo tayari kulinunua kwa ofa hiyo.

Rolls Royce walikataa kumtaja mteja huyo lakini walisema ni mtu mwenye ukwasi usio na shaka na alikuwa ametoa kazi kwa kampuni nyingine zimtengenezee ndege binafsi na boti ya kifahari kwa muundo ambao utakuwa na mfanano na gari hilo jipya.

“Sweptail ni aina ya gari la kifahari zaidi na gharama kubwa kuwahi kutengenezwa na kampuni yetu. Gari hili limetengenezwa kwa maombi ya mteja binafsi,” anasema Giles Taylor mkurugenzi wa ubunifu wa kampuni ya Rolls Royce Motor Cars.

Timu ya Rolls Royce ilifanya kazi kwa karibu na mteja huyo na kutengeneza gari hilo ambalo linamuonekano kama Rolls Royce ya mwaka 1920 na 1930 ikiwa na sehemu za kuhifadhi vitu vya gharama vya mteja huyo.

Gari hilo lina uwezo wa kubeba watu wawili na sehemu yake ya juu imetengenezwa kwa kioo cha aina yake ambacho kinalifanya kuwa na muonekano wa kipekee.

Kwa kiasi kikubwa Sweptail limetengenezwa kwa matairi ya aluminium na kampuni hiyo imesema hakuna gari jingine walilowahi kutengeneza kwa mfumo huo.

Kwa mujibu wa Rolls Royce Motor Cars, mteja alitaka gari hilo kuwa dogo lakini la kisasa na lenye uwezo wa kubeba abiria wawili tu. Mbao aina ya Macassar Ebony na Paldao ziliunganishwa na ngozi nyeusi na vionjo vingine vya siri kunakshi muundo wa ndani wa gari hilo.

Kuna batani moja kubwa ya kubonyeza ambayo akibonyeza sehemu maalum hufunguka ambapo huweza kuhifadhi briefcase yake. Batani nyingine iliyopo kati kati kufugua sehemu ambayo anaweza kuhifadhi mvinyo wake na ukaendelea kupata ubaridi.

Akiitambulisha gari hiyo nchini Italia, Ofisa Mtendaji Mkuu wa Rolls Royce Torsten Müller-Ötvös aliielezea Sweptail kama gari la aina yake ambalo linaonyesha ni kwa kiasi gari kampuni yake inavyomjali mteja.

“Sweptail inaeleza kila kitu kuhusu kumjali mteja. Siku zote huwa tunamsililiza mteja na kufanya kadiri ya matakwa yake ili kumfanya awe sehemu ya bidhaa aliyokuwa akiitamani,” anasema

Moja kati ya jambo la kushangaza ni kuwa, magari yote ya Rolls Royce, hutumia ngozi ya ng’ombe dume peke yake kutengenezea siti zake. Sababu ni kuwa  watengenezaji wake huepuka ngozi za ng’ombe jike kwa kuwa zinaweza kuwa na mikwaruzo ambayo mara nyingi hupatikana wakati ng’ombe jike akiwa ana mimba.

Gari moja hutumia ngozi za ng’ombe dume wanane ili kuweza kukamilika. Ng’ombe dume ambao hutumika kutengenezea muundo wa ndani wa Rolls Royce hufugwa sehemu maalumu barani Ulaya ambako hali ya hewa ni baridi kiasi kwamba mbu hawezi kuishi na hivyo kuwafanya kutoa ngozi isyo na mkwaruzo wa aina yoyote.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles