LONDON, ENGLAND
BINGWA namba tatu kwa ubora wa mchezo wa tenisi duniani raia wa nchini Uswis, Roger Federer, amefanikiwa kuingia hatua ya nne katika fainali za ATP baada ya kumchapa mpinzani wake Novak Djokovic baada ya kutumia dakika 72.
Djokovic raia wa nchini Serbia, amekubali kichapo hicho kwa seti 6-4, 6-3, hivyo kushindwa kuingia hatua inayofuata, hivyo Federer anapewa nafasi kubwa ya ya kutwaa taji hilo la Wimbledon wakati huu wa kiangazi.
Baada ya ushindi huo Federer mwenye umri wa miaka 38, Agosti 8 alikuwa anasherehekea kutimiza miaka hiyo, hivyo amedai furaha yake inaendelea kutokana na hatua aliyoingia.
“Nilicheza kwenye kiwango cha hali ya juu, nilijua lazima nifanya hivyo ili niweze kuingia hatua inayofuata, ushindani ulikuwa wa hali ya juu, mipango yangu ilikuwa hivyo.
“Tofauti ni kwamba nimeweza kupambana na nyota wa mchezo huu, kila mmoja alikuwa kwenye ubora wake na alionesha ushindani, ninafuraha kubwa, lakini ninampongeza mpinzani wangu kwa kuonesha ushindani mkubwa,” alisema mshindi huyo.
Kwa upande mwingine, Djokovic alisisitiza kukutana na ushindani mkubwa kutoka kwa mpinzani wake, lakini anaamini atayafanyia kazi makosa yake ili kuja kufanya vizuri kwenye michuano mingine.
“Nimekuwa nikijifunza mambo mengi kutoka kwake, ushindani wake ni wa hali ya juu hasa pale ninapokutana naye, kile anachokionesha uwanjani kinaonesha maana halisi ya upinzani kwenye mchezo.
“Kwa hatua aliyoingia bado ninaamini ana nafasi kubwa ya kufanya vizuri japokuwa kila hatua ina ushindani wake, ila ana nafasi kubwa ya kuwa mshindi, ninamtakia kila la heri katika hatua yake inayofuata,” alisema Djokovic.
Katika mchezo wa nusu fainali Federer anatarajia kukutana na Dominic Thiem, wakati huo Rafael Nadal akipambana jana na Stefanos Tsistsipas.