31.7 C
Dar es Salaam
Thursday, March 28, 2024

Contact us: [email protected]

ROBO FAINALI SHIRIKISHO ITATEGEMEA NA UTAKAVYOAMKA

NA WINFRIDA MTOI


DROO ya robo fainali ya Kombe la Shirikisho la Azam (FA), imechezeshwa jana, tayari miamba nane iliyotinga hatua hiyo kila mmoja amemjua mpinzani wake.

Michezo ya hatua hiyo itachezwa  kati ya Machi 30 na Aprili 1 mwaka huu, hii ni  kulingana na ratiba iliyotolewa na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) ambao ni wasimamizi wa michuano hiyo.

Katika droo hiyo, Yanga inaendelea kutoka nje ya Dar es Salaam, ambapo itavaana na Singida United katika Uwanja wa Namfua, Singida, Azam FC watakuwa wenyeji wa Mtibwa Sugar Uwanja wa Azam Complex.

Michezo mingine, Tanzania Prisons itawakaribisha JKT Tanzania katika dimba la Sokoine, Mbeya huku Stand United ikivaana na Njombe Mji Uwanja wa Kambarage, Shinyanga.

Kati ya timu nane zilizotinga hatua hiyo, saba zinashiriki Ligi Kuu Tanzania Bara isipokuwa moja JKT Tanzania iliyokuwa ikishiriki Ligi Daraja la Kwanza, lakini imepanda itaonekana Ligi Kuu msimu ujao wa 2018/2019.

Kutokana na matokeo ya droo hiyo ni wazi hakuna timu inayotarajia mteremko kuvuka nusu fainali kulingana na ubora wa vikosi hivyo na walichoonyesha katika hatua zilizopita.

Ikumbukwe kuwa droo ya michuano hiyo ilianza kuchezeshwa Desemba mwaka jana ikiwa ni hatua ya pili  iliyokuwa na timu 64 ambazo ni mchanganyiko kuanzia zile zinazoshiriki Ligi Kuu, daraja la kwanza na daraja la pili.

Awali mashindano hayo yalianza kwa kushirikisha timu za Ligi Daraja la Pili (SDL) na zile za Ligi ya Mabingwa wa Mikoa hivyo 16 zilizopita hapo ndizo zilifanyikiwa kutinga hatua ya 64 bora ambapo zilikutana na zile za VPL, FDL.

Hapo ndipo mechi zikaanza kuwa ngumu kutokana na kila mmoja kujipanga kusonga mbele hasa zile za VPL na FDL zilizoanzia moja kwa moja katika hatua hiyo.

Hivyo basi hadi mechi hizo za hatua ya pili zinamalizilika, timu zilizofanikiwa kufika 32 bora za VPL zilikuwa 12, FDL zilipita 11, tatu SDL na nne Mabingwa wa Mikoa.

Hatua ya tatu ya 32 ndiyo ilikuwa moto kwani kila timu ilidhihiridha ubora wake hasa baada ya kushuhudia timu za Ligi Kuu zikisumbuliwa na zile za madaraja ya chini miongoni mwao ikiwa mabingwa watetezi wa michuano hiyo, Simba waking’olewa na timu ya Ligi Daraja la Pili ya Green Warriors.

Kwa mwenendo ulivyokua huko nyuma na kutokana na matokeo ya mechi za 16 bora zilizomalizika hivi karibuni na kutoa timu nane zinazotarajia kucheza robo fainali mwezi huu, hakuna ubishi kuwa mambo bado ni magumu kwa timu zote.

Licha ya kuwa katika hatua inayofuata  mechi inayofikiriwa zaidi  ni  inayoikutanisha Yanga na Singida, lakini hali ni mbaya kwa  timu  zote ikiwamo Azam FC inayokutana na Mtibwa Sugar.

Hilo linathibitishwa na matokeo raundi iliyopita kwani Yanga ilivuka kwa ushindi mwembamba wa mabao 2-1 dhidi ya Majimaji, Azam waliifunga KMC 3-1 na Prisons waliing’oa Kiluvya United kwa bao 1-0.

Kwa upande wa Njombe Mji ambao ni vibonde katika ligi kuu wakiwa mkiani, walifanikiwa kuwatoa Mbao FC ilifika fainali ya michuano hiyo msimu uliopita ilipokutana na Simba Mjini Dodoma na kuchapwa mabao 2-1.

JKT Tanzania ilifika robo fainali kwa kuitoa Ndanda FC kwa bao 1-0, Stand United iliwatoa Dodoma FC kwa penalti 4-3, Mtibwa Sugar iliitoa Buseresere kwa mabao 3-0 huku Singida United iliwafungashia virago Polisi Tanzania kwa mabao 2-0.

MTANZANIA limezungumza na makocha wa baadhi ya timu zilitinga robo fainali ya michuano, ambapo wanakiri hali itakuwa ngumu na hakuna mwenye uhakika wa kusonga mbele.

“Droo nimeiona ni nzuri hakuna shida na inaonekana kabisa hakuna timu yenye unafuu kwa sababu hadi kufanikiwa kufika hapa ujue kikosi chako ni bora hivyo najipanga kwa kufahamu nakwenda kupambana na timu bora,” anasema kocha wa JKT Tanzania, Bakari Shime.

Shime anafafanua kuwa unafuu uliopo kwa vikosi vinavyoshiriki Ligi Kuu ni  kuendelea kucheza mechi zitakazowasaidia kujipanga zaidi tofauti ya JKT Tanzania haina michuano yoyote inayoendelea nayo baada ya Ligi Daraja la Kwanza kumalizika.

Aidha, kocha mkuu wa Prisons, Abdallah Mohamed, anasema hakuna timu inayomtisha mwenzake kwa kuwa asilimia kubwa zinakutana katika mechi za ligi.

“Ninachotaka ni kufika nusu fainali, najiandaa kama ilivyokuwa mechi zilizopita, timu ninayokutana nayo najua ni nzuri na ina wachezaji bora lakini hata kikosi changu pia ni bora,” anasema Mohamed.

Kwa upande wake straika wa Singida United, Tafadzwa Kutinyu, anasema haikuwa kazi rahisi kuvuka hatua hiyo, kinachotakiwa ni kujipanga zaidi waweze kufanya vizuri nusu fainali bila kujali timu wanayokutana nayo.

“Tutajiandaa kitimu, najua mechi itakuwa ngumu, ili tufanye vizuri lazima kuzingatia mazoezi kwa kuhamasishana wachezaji wote kuwa tunataka kushinda,” anasema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles