23.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, September 28, 2021

RITA yaendelea kuwasaidia wajane

Na ASHA BANI -DAR ES SALAAM

WAKALA wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (RITA) umeendelea kuwasaidia wajane katika usimamizi wa mirathi, uandaaji na utunzaji wa wosia ili kuepuka migogoro inayojitokeza mara kwa mara katika familia.

RITA iliandaa mafunzo kwa wajane Dar es Salaam  jana na kuhudhuriwa na Kaimu Kabidhi Wasihi Mkuu wa Wakala huo, Emmy Hudson.

Akizungumza wakati wa mafunzo hayo, Emmy alisema wajane ni kundi muhimu katika jamii ambalo limekuwa na changamoto zinazohitajika kupatiwa suluhisho.

“Siku ya leo (jana), tumeona ni vema kushirikiana nao na kusikia japo kwa uchache wanayoyapitia katika maisha, tumeona tuwapatie mafunzo yatakayowasaidia wao na kuwa mabalozi kwa wengine ambao hawajapata huduma hii, hasa masuala ya sheria,” alisema Emmy.

Alisema mwingiliano uliopo kati ya RITA na wajane ni pamoja na kusaidia kuongeza hamasa kwa wengine kuhusu umuhimu wa kuandaa na kuhifadhi wosia.

Emmy alisema kupitia huduma ya usimamizi wa mirathi, wajane wamekuwa sehemu ya wanufaika.

Alisema takwimu za mirathi ambazo zinasimamiwa na wakala hadi sasa ni 94, huku wakala huo ukikutana na changamoto mbalimbali ili kuwezesha mirathi hizo kuisha kwa wakati.

Emmy alisema suala la migogoro ya kifamilia miongoni mwa warithi, linasababisha kuchelewa kufungwa mirathi sambamba na kutopata ushirikiano kutoka kwa warithi.

Kuhusu wosia, alisema takwimu zinaonyesha mwaka jana na hadi mwaka huu, wosia 77 ndiyo ziliandikwa na kuhifadhiwa.

“Natoa msisitizo juu ya umuhimu wa kuandika na kuhifadhi wosia kwa maana inarahisisha mashauri ya mirathi,” alisema Emmy.

Mwenyekiti wa Chama cha Wajane Tanzania (Tawia), Rose Sarwati alisema muungano wao umefanikisha wajane kuwa kitu kimoja na hasa kushauriana mambo mbalimbali ya maendeleo.

Alisema pia umewasaidia kutambulika serikalini na kupata misaada na mikopo ya fedha kuendesha maisha yao.

Mwanasheria kutoka Shirika la Wanawake katika Sheria na Maendeleo Afrika (WiLDAF) – Tanzania, Zakia Msangi alisema sheria ya mirathi ya kimila inahitaji kufanyiwa marekebisho kwa sababu ina upungufu mwingi.

Moja ya upungufu huo, alisema ni kutokuweka muda  maalumu wa usikilizaji wa mashauri ya mirathi.

“Sheria  inaweka hitaji la lazima  la kuwepo kwa muhtasari wa kikao cha ndugu, ni tatizo kwa kuwa mara nyingi kunakuwa na ugomvi baina ya ndugu wa marehemu na mke wa marehemu, hivyo kusababisha kushindwa kufikia mwafaka, mjane kutengwa na hata kufukuzwa katika vikao,” alisema Zakia.

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

66,457FansLike
158,460FollowersFollow
519,000SubscribersSubscribe

Latest Articles