Rita kuhudumia kivingine kukabili corona

0
612

Na ASHA BANI-DAR ES SALAM

WAKALA wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (Rita) umewataka wananchi wanaofika katika ofisi ya wakala hiyo kupata huduma kuzingatia maelekezo yanayotolewa na viongozi na wataalamu wa afya kuhusu kujikinga na maambukizi ya ugonjwa wa corona.

Kwa mujibu wa Meneja Masoko na Mawasiliano Rita, Josephat Kimaro alisema wakala umechukua hatua mbalimbali kuimarisha mapambano dhidi ya ugonjwa huo lengo kubwa likiwa kuwalinda watumishi na wateja wanaofika kupata huduma katika ofisi zake kote nchini. 

“Huduma zote za wakala zinaendelea kutolewa katika ofisi zetu kote nchini na kutokana kuhitajika na wananchi wengi kutokana na umuhimu wake katika maisha ya kila mmoja, hivyo imetubidi kuchukua hatua madhubuti kuhakikisha tunayalinda makundi yote yanayohusika katika kutoa na kupata huduma,” alisema Kimaro.

Alizitaja njia zinazotumika kupambana na maambukizi ya corona katika ofisi zote za wakala huo ni pamoja na kuweka maji, sabuni na vitakasa mikono katika milango yote ya kuingia katika majengo yao, kuhakikisha watumishi wote wa wakala wanavaa barakoa wakiwa kazini, kuweka vitakasa mikono katika maeneo mbalimbali ya ofisi na kuweka vifaa vya kuwapima joto kila mtu anayeingia katika jengo la Rita Makao Makuu. 

Alisema maeneo yote ya ofisi kumewekwa matangazo yanayotoa maelekezo mbalimbali yanayohusiana na ugonjwa wa corona.

“Pia wakala uliandaa mafunzo kuhusu ugonjwa wa corona iliyoendeshwa na mtaalamu kutoka Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, lakini tunaendelea kuwasisitiza wananchi kuzingatia agizo la kuvaa barakoa wanapofika kupata huduma katika ofisi zetu na tunafurahi kuona asilimia kubwa  wanafuata maelekezo,” alisema Kimaro.

Alisema pia wakala unaendelea kusisitiza wananchi kutumia njia mbadala za mawasiliano kupata huduma ambazo sio lazima kufika ofisi za wakala kama vile kupata maelezo kuhusu huduma zinazotolewa, kupakuwa fomu za maombi ya huduma zote, kuuliza maswali au kutoa maoni.

Aliongeza kuwa wapo wananchi ambao wanafika ofisi za Rita kupata maelezo ya jinsi ya kupata cheti cha kuzaliwa na gharama zake au amepoteza cheti anawezaje kupata nakala wakati taarifa zote hizi zinaweza kupatikana bila yeye kufika ofisini.

Alieleza njia mbadala za kupata taarifa hiyo ni pamoja na ukurasa wa facebook ([email protected]) kupiga simu bure 0800 117 482, kutuma barua pepe [email protected]  na katika tovuti ya wakala www.rita.go.tz. 

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here