RITA: IDADI YA WATANZANIA WALIOJISAJILI VYETI VYA KUZALIWA HAIRIDHISHI

0
548

Na Maregesi Paul – Morogoro

WANANCHI hushindwa kumudu gharama za kufikia huduma za kujisajili na kupata vyeti vya kuzaliwa kutokana na kuwa mbali nao.

Hadi sasa ni asilimia 13.4 ya Watanzania ndio wamesajiliwa na kuwa na vyeti kati ya zaidi ya milioni 50.

Akizungumza jana wakati wa semina ya wahariri wa vyombo vya habari kuhusu maboresho ya mfumo wa usajili wa matukio muhimu ya binadamu na ukusanyaji wa takwimu (CRVS), Mwenyekiti wa Bodi ya Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (RITA), Profesa Hamis Dihenga, alisema kuwa takwimu hizo ni kulingana na sensa ya watu na makazi ya mwaka 2012 na kwamba hali hiyo imekuwa ikichangia Serikali kushindwa kupanga mipango yake kutokana na kutokuwa na takwimu sahihi za wananchi.

Profesa Dihenga alisema  pamoja na takwimu hizo, lakini pia wapo wananchi ambao huzaliwa na kufa bila  taarifa zao kuonekana katika kumbukumbu zozote serikalini,  hivyo hali ya usajili wa matukio ya vifo, ndoa na talaka nayo hairidhishi pamoja na ukweli kwamba takwimu zake ni za muhimu.

Alisema Serikali inafahamu  kwamba hili ni tatizo na tayari imeanza kuchukua hatua kwa kufanya maboresho ya mfumo wa usajili uliopo na kuanzisha mfumo utakaofanya kazi vizuri ili kusajili matukio muhimu ya binadamu na takwimu (CRVS-Civil Registration And Vital Stastitics) unaolenga kutatua changamoto zilizopo.

“Usajili wa matukio muhimu ndio mfumo mama katika nchi yoyote kwani husajili taarifa za mtu anapoingia duniani kwa kuzaliwa, unaweka kumbukumbu kadiri anavyokua na kupita katika hatua mbalimbali hadi anapotoka duniani kwa kufariki.

“Taarifa kutoka kwenye mfumo huu hupaswa kutumika na mifumo mingine ya Serikali kama kianzio kwa mifumo mingine ya Serikali kama uraia, utaifa na daftari la kupiga kura,” alisema Profesa Dihenga.

Alisema kwa sasa Serikali imekusudia kukuza uchumi kupitia viwanda, hivyo takwimu sahihi za makundi yote ya wananchi zitachochea  kukua kwa sekta hiyo kutokana na ukweli kwamba zitawezesha  wawekezaji kujua uhakika  wa masoko na bidhaa.

Akifungua semina hiyo, Waziri wa Sheria na Katiba, Profesa Palamagamba Kabudi, alisema Serikali imetekeleza usajili wa watoto walio na umri chini ya miaka mitano na kwamba imefanikiwa kwa asilimia 100 katika mikoa ya Iringa, Njombe, Geita na Shinyanga.

Profesa Kabudi alisema RITA wamekwishatekeleza maboresho ya mfumo kama jinsi ya mkakati wa CRVS  unaotekelezwa kupitia mpango wa usajili wa watoto walio na umri wa miaka mitano, na kwamba mpango huo wa kudumu umeanza kutekelezwa katika mikoa saba na kuonyesha mafanikio makubwa kwa kuweza kusajili watoto kwa wastani wa asilimia 77 kwa idadi ya watoto wote wa kundi hilo kwa mikoa husika.

Alisema kwa mikoa minne ya Iringa, Njombe, Geita na Shinyanga imeweza kufanikiwa kwa asilimia 100 kwa kusajili watoto wa kundi hilo  na kwamba kazi inaendelea.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here