23.2 C
Dar es Salaam
Thursday, August 11, 2022

Ripoti yamsafisha Trump, kibano bado kingalipo

JOSEPH HIZA Na MASHIRIKA

MWANASHERIA Mkuu wa Marekani, William Barr amelikabidhi Bunge muhtasari wa ripoti ya Mwanasheria Maalumu Robert Mueller, ikimsafisha Rais Donald Trump dhidi ya tuhuma kuwa alishirikiana na Urusi kumsaidia kushinda uchaguzi wa rais mwaka 2016.

Barr amesema Mueller hakuwa na uhakika iwapo timu ya kampeni ya Trump ilipanga au kuhusika na mpango wa Serikali ya Urusi wa kuingilia uchaguzi huo, hitimisho ambalo linampa Trump ushindi mkubwa kisiasa.

Tayari Makamu wake, Mike Pence amesema hitimisho hilo ni uthibitisho wa jumla kuwa Rais Trump na jopo lake la kampeni yake wamevuliwa tuhuma mbaya mno na ni muhimu matokeo hayo kupokewa kwa furaha na Wamarekani wanaopenda ukweli na uadilifu.

Aidha Pence ameiita siku iliyotolewa ripoti hiyo kuwa ni muhimu kwa Taifa la Marekani, kwa Rais Trump na utawala wake. 

Mueller alitumia karibu miaka miwili kuchunguza madai kwamba Urusi iliingilia kati uchaguzi wa urais wa Marekani na kumsaidia Trump kumshinda mpinzani wake, Hillary Clinton.

Lakini pia mwanasheria huyo mkuu amesema uchunguzi huo haujamwondolea Trump tuhuma za uwezekano wa kuzuia haki kutendeka.

Lakini kwa upande wa wapinzani wake, Chama cha Democrats ni pigo kubwa kisiasa.

Baada ya miaka miwili ya kuhaha usiku na mchana kutafuta makosa ya Trump, inakutana na kitu isichopenda kukisikia kwani kinaweza kukigharimu chama chao ikizushwa kwamba wana chuki binafsi na Rais. Hivyo, ni mbaya kwao kusikia eti: hakuna ushahidi wa mwingilio wa uchaguzi, hakuna ushahidi wa kuzuia haki kutendeka na mbaya zaidi Hillary Clinton hayupo Ikulu!.

Kama ilivyotarajiwa Democrats tayari wameanza kushinikiza kutolewa ripoti nzima ili wajue cha kufanya zaidi, yaani mapambano bado yanaendelea!.

Ajenda yao ilikuwa moja tu kumwangusha Trump na kutangaza ushindi. Kwa karibu miaka miwili Democrats walitishia kumpigia kura ya kutokuwa na imani bungeni iwapo atathubutu kumfukuza Mueller wakikumbuka vitendo kama hivyo dhidi ya waliokuwa wakimchunguza Trump.

Kwa ripoti yake hiyo, Mueller machoni mwa wengi ametoka kuwa shujaa hadi dhalili. Kwa sasa atatazamwa kwamba amekula njama ya kuzuia haki kwa Clinton kuikamata Ikulu.

Spika wa Bunge Nancy Pelosi na kiongozi wa wa shughuli za Bunge, Chuck Schumer wote wanachama waandamizi wa Democratic wamesema  ripoti  hiyo inaibua maswali mengi kuliko majibu. Hivyo wanataka ripoti yote ichapishwe hadharani.

Ukiachana na hayo, hitimisho la uchunguzi wa Mueller kupitia muhtasari wa Mwanasheria Mkuu William Barr, unalazimisha Wamarekani na dunia kwa ujumla kutowaza kuutegemea mfumo wa jinai katika kutatua matatizo ya kijamii.

Waliberali, wahafidhina, vyama vya Democrats na Republicans vilikuwa vimebeba matumaini kwa Mueller kwa ajili ya ufumbuzi wa matatizo yaliyosababishwa na utawala wa Trump.

Muhtasari wa Barr unaugawa uchunguzi wa Mueller katika maeneo mawili: Uingiliaji wa Urusi na uzuiaji wa haki kutendeka. Wakati wengi wa mashahidi na ushahidi ambao Mueller aliuegemea unabakia kutojulikana bado, muhtasari wa Barr unamkariri Mueller akisema uchunguzi haukubainisha iwapo wajumbe wa timu ya kampeni ya Trump ulikula njama au walishirikiana na Serikali ya Urusi kuingia shughuli za uchaguzi wa urais wa Marekani.”

Barr haelezi anachomaanisha Mueller kubainisha au kiwango cha sheria kilichotumika ukizingatia ripoti nzima bado haijatolewa. Lakini anathibitisha kwamba Urusi ilipanga kuingilia uchaguzi na ilitoa ofa nyingi za kuisaidia timu ya kampeni ya Trump kupitia ‘washenga’.

Na inafahamika wazi kuwa timu ya kampeni ya Trum kamwe haikuwahi kuripoti ofa hizo za Urusi, ambazo zilishuhudia mkwewe na mtoto wake wakiwa katikati ya njama hizo, haifahamiki wazi iwapo hilo lilizingatiwa.

Akiwa kama rais, ambaye anajiweka karibu na wanaohesabiwa kuwa madikteta duniani hasa wale wanaojitoa ufahamu kwa kumsifu ili kumpaka mafuta ya mgongo rais huyo mpenda sifa, upo ushahidi kuwa aliwaongopea Wamarekani kuhusu nia yake ya kufanya biashara nchini Urusi.

Tuhuma hizi zinaanzia na mshirika wa Trump aliyezaliwa Urusi hadi ofa iliyotolewa na Rais wa Urusi Vladimir Putin ya jengo, bure lenye thamani ya dola 50 kama sehemu ya kuvutia soko.

Wanasheria wa Rais wamekanusha Trump kushiriki katika dili hilo. Ikumbukwe mwenyewe awali alikana walau kwenda Urusi lakini picha za video na mnato zilimuumbua zikichora ramani jinsi alivyojiandaa na safari, weekend yake kuhudhuria shindano la urembo Urusi na kurudi kwake New York huku akisifu Urusi kupitia mtandao wake wa Twitter.

Kuhusu kuzuia haki kutendeka, muhtasari wa Barr unazua maswali zaidi kuliko majibu kwa vile unahusisha nukuu tata kutoka kwa Mueller kwamba ‘wakati ripoti hii ikiwa haihitimishi kwamba Rais alitenda jinai, lakini pia haimuondolei hatia.”

Kwa wajuzi wa sheria, kuna matendo mengi ya Rais ambayo yalisababisha ukwamishaji wa haki kutendeka, mengi yakiwa ya hadharani ikiwamo kauli za vitisho kwa Mueller, kwa mara nyingine ukiwa ni mwenendo wa kusikitisha sana kama tutakavyogusia kidogo baadaye.

Wakati wa kipindi cha miaka miwili ya uchunguzi wa Mueller, alifichua na kusababisha kufichuka kwa masuala mengi yanayokera kuhusu Rais, watu waliomzunguka na uongozi wa taifa hilo.

Kinachoshangaza ni Mueller kutofanya maamuzi. Ikumbukwe kuna sababu mbili kwanini Mueller alikuwa chaguo bora kwa kazi hiyo.

Kwanza hakuwa na upande. Aliteuliwa kwa sababu Wizara ya Sheria ilikuwa na mgongano wa kimaslahi katika kumchunguza Rais. Imeelezwa wazi linapokuja suala la mwanasheria maalumu, kutokuwa na upande ni moja ya vigezo vya kuzingatiwa.

Pili, hakuna mtu duniani anayejua kwa undani zaidi kuhusu uchunguzi huu zaidi ya Mueller. Ilikuwa kazi ya Mueller kufanya chunguzi zote kwa kugusa kila eneo linaloshukiwa na kufungua mashitaka ikibidi katika suala hilo na kuamua iwapo kuna ushahidi wa mashitaka au la.

Wengi wanabakia kutoridhishwa na muhtasari wa Barr katika suala la ukwamishaji wa haki kutendeka, hasa linalohusiana na ufukuzaji wa bosi wa zamani wa Shirika la Upelelezi (FBI), James Comey.

 Baada ya Comey kukataa ombi la Rais la kulainisha ukali wa uchunguzi wake dhidi ya Mshauri wa Usalama wa Taifa Michael Flynn, Trump akahitimisha kibarua cha mtu huyo aliyeongoza chunguzi dhidi ya timu yake ya kampeni. Trump alikana madai ya Comey ya kumuomba alegeze uchunguzi.

Ijapokuwa Rais na Wizara ya Sheria vinadai Comey alifukuzwa kutokana na namna alivyoshughulikia kashfa ya barua pepe za Hillary Clinton, haikuchukua muda katika mahojiano yake na mwandishi wa NBC, Lester Holt alisema alikuwa akifikiria ‘kitu hiki Urusi’ wakati akimfukuza Comey.

Trump pia aliendesha kampeni ya mashambulizi yasiyokwisha dhidi ya Mueller na wapelelezi wake wakati mwingine akiwaita wahalifu mafisadi wanaosaka mchawi kwa lengo la kumuangusha urais.

Kwa mujibu wa barua ya Barr, kwa sababu zisizojulikana, Mueller hakutoa hitimisho katika suala la ukwamishaji  haki, lakini ameliacha suala hilo kwa ngazi nyingine.

Barr kisha akaashiria kwamba yeye na Naibu Mwanasheria Mkuu Rod Rosenstein wanadhani Mueller aliona wakati wa uchunguzi wake huo, ushahidi aliopata haukutosha kubainisha kuwa Rais alikwamisha haki.

Kukubali kwamba Trump hakushirikiana na Urus ni rahisi kwa sababu uchunguzi ulizingirwa na mazingira ya usiri. Hata hivyo, hili la kukwamisha haki ni tofauti kwa vile lilishuhudiwa na wengi na hivyo kushikiwa bango.

Kwa kushindwa kutoa hitimisho la uwezekano wa kuzuia haki kutendeka, ripoti ya Mueller inakabidhi suala hilo kwa Bunge hasa la wawakilishi linalodhibitiwa na chama cha Democratic, kuangalia iwapo ukwamishaji wa haki kutendeka ulifanyika au la.

Iwapo jibu la swali hilo ni ndiyo, viongozi wa Bunge watakuwa chini ya shinikizo kubwa la kuanza mchakato wa kumng’oa Trump.

Ijapokuwa Barr anasema sehemu ya ripoti ya Mueller lazima ibakie siri kulinda usiri wa kisheria, kuna uwezekano mkubwa hilo kutokubalika na haitakuwa ajabu ikavuja kwa vyombo vya habari muda si mrefu kuanzia sasa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
198,395FollowersFollow
550,000SubscribersSubscribe

Latest Articles