31.2 C
Dar es Salaam
Saturday, December 2, 2023

Contact us: [email protected]

Ripoti yafichua kampuni za China, India zinavyowafanyia unyama wafanyakazi Watanzania

Na FARAJA MASINDE-DAR ES SALAAM

RIPOTI mpya iliyozinduliwa na Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), imefichua namna baadhi ya kampuni zinazomilikiwa na raia wa China na India zinavyowafanyia vitendo vya kinyama wafanyakazi wazawa.

Katika Ripoti hiyo inayofahamika kama, Ripoti ya Haki za Binadamu na Biashara Tanzania Bara ya mwaka 2018/19, iliyozinduliwa juzi jijini Dar es Salaam, imebainisha ubaguzi wa aina mbalimbali unaofanywa na raia hao wa kigeni.

Ripoti hiyo imeeleza kuwa katika mahojiano na wafanyakazi mahala pao pa kazi, malalamiko ya ubaguzi wa rangi yalitolewa zaidi katika kampuni zinazomilikiwa na wawekezaji wa wenye asili ya kiasia, hasa kutoka katika mataifa ya China na India.

“Wafanyakazi hao walilalamika kunyanyaswa na kubughudhiwa na wasimamizi au mabosi wao wenye asili ya kigeni, huku wakipewa vitisho mbalimbali ikiwa wataenda kinyume na matakwa yao,” imeeleza ripoti hiyo.

Aidha, ripoti hiyo imeitaja moja kwa moja kampuni moja ya China  inayojihusisha na miundombinu ya barabara na madaraja, kwamba wafanyakazi wake walidai wananyanyaswa na mwajiri wao mwenye asili ya kichina kwa kulipwa ujira mdogo ikiwamo kutokupewa vifaa vya kazi huku wakitishwa kwa ukali kwamba watakomeshwa wengine kutishwa hata kuuawa.

“Na hii hasa ni pale wanapodai nyongeza ya mishahara, malalamiko kama hayo yalitolewa pia katika kampuni (inatajwa, ambayo sisi hatuwezi kuitaja kwa sababu za kimaadili), iliyopo mkoani Kilimanjaro huku katika kampuni ya (inatajwa), kulikuwa na malalamiko ya vitendo vya kibaguzi kwa wafanyakazi wa kitanzania ikiwamo kupigwa, kupunguziwa mshahara bila maelezo ya msingi na kufanyishwa kazi bila mkataba,” imeeleza ripoti hiyo.

Kama hiyo haitoshi, ripoti imeeleza kuwa katika kampuni moja ya China iliyopo mkoani Pwani, iliripotiwa kwamba mfanyakazi mmoja aliyejulikana kwa jina la Juma Abiud alifanyiwa kitendo cha kikatili cha kufungiwa kwenye banda la mbwa na bosi wake mwenye asili ya kiasia, sababu tu alidai mazingira ya kazi yaboreshwe.

“Nilipiga kelele kuomba msaada lakini hakuna aliyejitokeza, baada ya muda yule mchina akaja akanichukua na kunipakia kwenye gari lake tukaenda kituo cha polisi cha Mkuranga, hawakunifikisha kituoni, alipaki pembeni akaenda kuchukua PF3, polisi walitoa PF3 bila hata kuniona, nilipelekwa Muhimbili(Hospitali ya Taifa) lakini baadaye nikahamishwa kwa kuwa wachina walilalamika gharama za matibabu ni kubwa,” alisema Abiud.

Mfanyakazi mwingine kutoka moja ya kampuni inayomilikiwa na wachina alinukuliwa akisema kuwa; 

“Hawa wachina ukimaliza kazi wanasema umewatia hasara, ukibisha wanaanza kutupiga ‘kung fu’ na wanatupiga kwelikweli si mchezo. Mimi hadi sasa nina uvimbe na maumivu makali na nimechukua PF3 kwa ajili ya matibabu,” alisema mfanyakazi huyo.

Ni bayana kuwa matukio hayo yanakinzana na Sheria za kazi zinazotumika nchini, ikiwamo Sheria ya Kazi na Mahusiano Kazini ya mwaka 2004 sambamba na zile za kimataifa, hususani zinazotokana na Shirika la kazi Duniani (ILO), ambazo zinakataza ubaguzi wa aina yoyote mahala pa kazi, miongoni mwa ubaguzi huo ni pamoja na ule wa rangi, na kabila.

“Katika utafiti uliofanyika, malalamiko kadhaa yalitolewa kuhusu aina hiyo ya ubaguzi, ambapo ubaguzi mahala pa kazi kwa kigezo cha rangi au kabila ulilalamikiwa na wafanyakazi wengi zaidi waliofikiwa asilimia 43, ukifuatiwa na ubaguzi wa jinsia kwa asilimia 27 na ubaguzi kwa kigezo cha ulemavu kwa asilimia 13.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
579,000SubscribersSubscribe

Latest Articles