RIPOTI YADAI MADURO AFIKIRIA KUTOROKA VENEZUELA

0
596

TEXAS, MAREKANI


RIPOTI mpya imefichua Rais wa Venezuela, Nicolas Maduro, anahaha kutafuta hifadhi ya kisiasa nchini Cuba au Urusi baada ya kuongezeka kwa shinikizo la kimataifa dhidi ya utawala wake.

Habari zilizotokana na ripoti ya Kituo cha Kimataifa cha Ushauri (Strator) kilichopo hapa, inasema wachambuzi wake wamekuwa wakipokea ripoti kwa zaidi ya mwaka sasa kuwa Maduro ‘anafiiria kuomba hifadhi ya kisiasa katika nchi za Urusi au Cuba.’

“Cuba inatoa mchango mkubwa katika kufanya mazungumzo yasiyo ya moja kwa moja kwa Urusi na Marekani kuhusu Venezuela,” taasisi hiyo imesema katika ripoti hiyo iliyotolewa hivi karibuni.

Ripoti hiyo, ambayo hajataja chanzo chochote inasema, “Serikali za Urusi na Cuba ziko radhi kumpokea Rais Nikolas na mkewe Cicilia Flores lakini si wanasiasa wengine.”

Maofisa wa Cuba pia walihusika kwa majadiliano ya miezi kadhaa na Hispania ambayo yaliwezesha kufikiwa uamuzi wa Maduro kumwachia huru kutoka gerezani, mwanzoni mwa mwezi huu kiongozi wa upinzani Leopold Lopez.

Kwa mujibu wa Strator, kuachiwa huru kwa Lopez kumekwenda sawia na kukubaliana na Marekani.

Maduro anakabiliwa na shinikizo kutoka kwa utawala wa Rais Donald Trump wa hapa, ambaye mapema wiki hii alimtaja rais huyo wa Venezuela kuwa kiongozi mbaya anayeota ndoto kuwa dikteta.

Trump alitishia kuiwekea vikwazo vya kiuchumi nchi hiyo ikiwa Maduro ataendelea na mipango yake ya kuunda Bunge la Katiba Julai 30.

“Marekani kwa mara nyingine inatoa wito wa kufanyika uchaguzi mkuu huru na wa haki na inasimama na wananchi wa Venzuela katika shauku yao ya kuirejesha nchi kwenye ustawi na demokrasia ya kweli,”alisema Rais Trump.

Wakati Maduro akikabiliwa na shinikizo la kimataifa, upinzani umekuwa ukiandaa mfululizo wa maandamano ya kumpinga kuhakikisha hafanikiwi mpango wa kubadili katiba.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here