WIKI hii Shirika la Fedha Duniani (IMF) lilitoa ripoti ambayo pamoja na mambo mengine imesifu eneo la ukuaji wa uchumi lakini ikiacha shaka katika eneo la mzunguko wa fedha.
Katika ripoti yake, IMF imeonyesha kuridhishwa na kasi ya ukuaji wa uchumi inayofikia asilimia 7, ukusanyaji wa kodi ambapo wastani umeongezeka kutoka bilioni 800 kwa mwezi hadi kufikia bilioni 1,100.
Pamoja na hayo, IMF inaona uchumi wetu unakabiliwa na ukata na kwamba ili kuondokana na changamoto hiyo ni lazima Serikali itafute namna ya kuhakikisha biashara katika sekta binafsi hazifi bali zinazidi kustawi.
Kumekuwa na mjadala mkubwa tangu IMF itoe ripoti hiyo hasa kutokana na kile kinachotajwa kuwa ni uamuzi wa Serikali kukopa katika benki za ndani kiasi cha bilioni 1,200 ili kugharamia bajeti yake.
Uamuzi huo tayari umeonekana kuwashtua baadhi ya wachambuzi ambao wanasema utazifanya benki hizo kushindwa kuzikopesha sekta binafsi hali ambayo inaweza kuzidisha ukata na mdororo wa biashara.
Taarifa hizi pamoja na ripoti hii ya IMF imekuja wakati ambapo tulipata kuandika huko nyuma kwamba pamoja na nia njema ya Serikali, lakini uamuzi wake wa kuhamisha mafungu yake yaliyokuwa yakiwekwa katika benki mbalimbali za kibiashara na kuyapeleka moja kwa moja Benki Kuu ya Tanzania (BoT) kama njia ya kuwabana wale wote waliokuwa wakitumia mwanya huo kujinufaisha, umesababisha mtikisiko mkubwa wa kifedha si tu katika taasisi hizo za kifedha bali na jamii kwa ujumla.
Uamuzi huo ulipata kupingwa na baadhi wakiwamo wachumi wakisema una athari kubwa na kwamba kabla ya kubadili hilo pengine Serikali ingetafuta namna ya kuwabana wale waliokuwa wakiutumia vibaya.
Tayari zipo taarifa kutoka katika benki hizo zinazoeleza kuwa uwezo wa wateja kujiwekea amana umepungua na hivyo kuwaathiri kwani amana zikishuka na uwezo wa mabenki hayo kukopesha unashuka.
Si hayo tu, baadhi ya wakuu wa taasisi hizo za kifedha waliwahi kueleza hatari wanayoiona mbele ya watu kupoteza ajira, kasi ya kukua kwa uchumi kupungua endapo hakutakuwa na juhudi za makusudi za benki wenyewe au Serikali kushughulikia jambo hilo.
Gavana wa BoT, Profesa Benno Ndulu, aliwahi kukiri kulitambua jambo hilo huku akiahidi BoT kuzisaidia benki hizo kupata suluhisho, lakini hata hivyo hakueleza ni kwa jinsi gani.
Pamoja na hilo, Gavana huyo alizitaka benki hizo kwa upande wake kufanya ubunifu ambao utazisaidia kutoka hapo zilipo hivi sasa.
Pamoja na hayo yote, tayari jamii imeshuhudia athari zake kwani wengi waliotegemea kupata mikopo kwa ajili ya kuimarisha biashara au shughuli zao za kimaendeleo wameshindwa kufanya hivyo.
Licha ya Serikali kueleza azma yake hiyo kuwa imetokana na msimamo wake wa kudhibiti matumizi yasiyo ya lazima na kudhibiti ufisadi, lakini athari zimeonekana kuwapata zaidi watu wa chini wasiojihusisha na ufisadi.
Kwa sababu hiyo basi, Serikali haipaswi kupuuza ripoti hiyo ya IMF pamoja na ushauri iliyoutoa ili kasi ya kukua kwa uchumi itoe maana halisi katika maisha ya watu.