25.2 C
Dar es Salaam
Thursday, June 1, 2023

Contact us: [email protected]

RIPOTI YA CAG YAVURUGA BUNGE

*PAC, LAAC wasema mawaziri wanadhalilisha Bunge

*Dk. Tulia adai wanachofanya wanatoa mawazo yao binasi


Na Fredy Azzah-Dodoma

SIKU moja baada ya Mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe (ACT-Wazalendo) kutoa uchambuzi wake kuhusu ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) na kupinga hatua ya mawaziri kujibu, hatimaye hoja hiyo inaonekana kulivuruga Bunge.

Kutokana na hali hiyo kamati za Bunge zinazosimamia fedha za umma na baadhi ya wabunge, wamekuwa wakali juu ya kitendo hicho cha mawaziri hao.

Walioibua suala hilo kwa siku ya jana ni Mbunge wa Nyamagana, Stanslaus Mabula na mwenzake wa Ulanga,  Goodluck Mlinga wote kutoka CCM, ambapo walilazimika kuomba mwongozo kwa Naibu Spika wakihoji uhalali wa mawaziri kujibu hoja hizo za CAG.

Jana baada ya kuisha kipindi cha maswali na majibu, Mabula alihoji sababu za baadhi ya mawaziri ambao wizara zao zimeguswa katika ukaguzi huo wa mwaka 2016/17 kuzungumza na waandishi wakijibu hoja za CAG.

“Tunapozungumza uchumi wa nchi haina tofauti kabisa na taarifa ya CAG, hivi majuzi baada ya taarifa ya CAG mijadala mikubwa iliibuka huku bungeni na nje ya Bunge na haswa pale mawaziri walipojaribu kueleza uchumi wan chi uko imara ama hauko imara, matamshi mengine yameendelea kutoka kueleza kwamba jambo hili labda siyo sawa.

“Nje wananchi wanachanganyikiwa, nataka mwongozo wako ni nini kifanyike kwamba jambo hili ni sawa ama si sawa,” alisema.

Kwa upande wake Mlinga, alisema. “Mawaziri wamekuwa wakijibu kila mmoja kivyake, sasa nilikuwa nataka mwongozo wako nini kauli ya kiti, baada ya wao kutoa kauli hizi ndo jambo hili limekwisha, kama ndiyo hivyo na mimi nataka nijipange na wana Ulanga nasisi tunakujaje kutokana na ripoti hiyo ya CAG,” alisema.

Akijibu mwongozo huo Naibu Spika wa Bunge, Dk. Tulia Ackson, alisema wanachofanya mawaziri hao wanatoa maoni yao binafsi na kwamba kwa mujibu wa Sheria ya Ukaguzi, wanapaswa kutoa majibu katika vikao vya Kamati za Bunge.

“Sheria kama ambavyo haimkatazi CAG kuzungumza na vyombo vya habari kwa namna hiyo hiyo haimkatazi mtu yeyote kuzungumzia taarifa ya CAG, sheria haijasema CAG azungumze na vyombo vya habari na pia haijamkataza mtu yoyote kuzungumzia taarifa hii.

“Ndiyo maana vyama vya siasa vingine vimeshaeleza kile wanachoona inafaa. Sheria hizi mkizipitia waheshimiwa wabunge majibu huwa hayatolewi kwa mdomo. Waziri anatoa mawazo yake,” alisema Dk. Tulia.

Aliema anayepeleka taarifa ya CAG bungeni ni waziri, kwamba CAG hana mahali pa kupeleka hiyo taarifa isipokuwa kupitia kwa waziri.

“Kwa hivyo waziri anavyotoa maelezo si kwamba amejibu hoja za CAG, hoja za CAG zinajibiwa kwenye kamati kwa mujibu wa sheria na anayejibu kwenye kamati ni Ofisa Masuuli (Katibu Mkuu wa Wizara).

“Msitake kuliweka hili jambo kuonesha hakuna utawala wa sheria nchini. Sheria zipo na mzisome vizuri kuliko kutoa maelezo ya kuchanganya umma.

“Sheria ipo wazi kwamba ikishaletwa taarifa ya CAG hapa bungeni mtu yeyote ana ruhusa kuizungumzia. Hiki kinachojibiwa na mawaziri ni maoni yao,” alisema Dk Tulia.

PAC na LAAC

 

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), Naghenjwa Kaboyoka, akizungumza na waandishi wa habari alisema hatua hiyo ya mawaziri ni kinyume cha taratibu za kibunge na pia ni udhalilishaji wa Bunge.

“Bunge linawajibika kusimamia matumizi ya fedha za umma  na CAG ni jicho la Bunge, anaangalia kama hizi fedha zimetumika kama Bunge lilivyopitisha.

“Bunge tusingeweza kukaa wote, CAG anavyopitia taarifa anarudisha kwa muhusika anawapa siku 21 kujibu, akimaliza akifunga mjadala analeta bungeni na yaliyo kwenye ripoti inamaana ni hoja zilizoshindwa kujibiwa na wahusika, wakija hapa sisi tunawahoji,” alisema.

Akizungumzia kauli ya Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Philip Mpango, alisema mafuta ambayo CAG alisema yalitakiwa yaende migodini lakini yakatumiwa na watu wengine, fedha zake zimeaza kurudishwa, akihoji ni nani aliyethibitisha hilo.

“Nani ataha kikisha hilo kwasababu, huku ni kumdhalilisha CAG aonekane taarifa zake zimepitwa na wakati. Kwenye kamati tungehoji zaidi hizi fedha zimerudishwa vipi.

“Kama tunataka hadhi ya Bunge ibaki ilivyo taratibu zilizopo zifuatwe, kama tunataka kulidhalilisha basi tuvunje taratibu,” alisema Kaboyoka.

Naye Mwenyekiti wa Kamati ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC), Vedasto Ngombale, alisema hoja yao kubwa ni suala la utaratibu kufuatwa.

“Huu si utaratibu wala utamaduni mawaziri kufanya hivi, utaratibu wa kibunge ni kuwa ripoti hii ikishatolewa inapelekwa kwa maafisa masuuli wakimaliza wairudishe, kamati ziwaite ziwahoji na CAG akiridhika ndiyo afute hoja husika,” alisema Ngombale.

 

 

Kwa habari zaidi jipatie nakala ya gazeti la MTANZANIA.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
213,226FollowersFollow
567,000SubscribersSubscribe

Latest Articles