25.7 C
Dar es Salaam
Friday, April 19, 2024

Contact us: [email protected]

RIPOTI YA CAG YAMULIKA MAENEO NYETI MANANE

Na MWANDISHI WETU


MDHIBITI na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Prof. Mussa Assad, amemkabidhi Rais Dk. John Magufuli ripoti ya ukaguzi wa hesabu kwa mwaka wa fedha unaoishia Juni 2016, ambayo imegusa maeneo manane nyeti.

Akipokea ripoti hiyo, Rais Magufuli  amemwagiza pia CAG kufanya ukaguzi wa kina katika sekta ya madini na kubaini mianya yote ambayo inasababisha nchi kukosa mapato katika misamaha ya kodi, mikataba mbalimbali na ulipaji wa kodi.

 

MAENEO NYETI YALIYOGUSWA

Taarifa iliyotolewa na Ikulu jana, imesema ripoti hiyo imegusa hali ya hesabu za Serikali, misamaha ya kodi, ukusanyaji wa kodi na maduhuli ya Serikali, uandaaji na utekelezaji wa bajeti.

Imegusa pia hali ya deni la taifa, usimamizi wa rasilimali watu, usimamizi wa mali na madeni ya Serikali na usimamizi na uendeshaji wa taasisi za umma zikiwamo za kifedha na Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco).

Taarifa hiyo ya Ikulu iliyosainiwa na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Ikulu, Gerson Msigwa, imesema hafla ya kukabidhi ripoti hiyo ilihudhuriwa pia na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa.

 

TANESCO, MISAMAHA YA KODI

Akikabidhi ripoti hiyo, Prof. Assad alisema pamoja na hatua iliyopigwa na Serikali katika kuzingatia taratibu za fedha, bado kuna upungufu unaoendelea kujitokeza.

Kutokana na hali hiyo, ameshauri hatua zichukuliwe kukabiliana na hali hiyo ikiwamo kudhibiti mianya ya upotevu wa fedha za umma katika madini na kuiepusha Tanesco kununua umeme wa gharama kubwa.

Amegusia pia matumizi mabaya ya misamaha ya kodi na kuongeza mashine za kutoa risiti za kielektroniki (EFD).

Akizungumza baada ya kupokea ripoti hiyo, Rais Magufuli aliipongeza Ofisi ya CAG kwa kazi inayofanya, huku akiahidi kuwa Serikali itaendelea kushirikiana nayo kwa karibu ili kukabiliana na mianya yote inayosababisha upotevu wa fedha za umma.

 

UKAGUZI KATIKA MADINI

Rais Magufuli alimwagiza CAG kufanya ukaguzi wa kina katika sekta ya madini na kubaini mianya yote ambayo inasababisha nchi kukosa mapato makubwa, hususan katika misamaha ya kodi, mikataba mbalimbali na ulipaji wa kodi.

“Haiwezekani Watanzania wanakosa dawa hospitali wakati dhahabu zao zinaondoka, Watanzania wanakosa maji wakati dhahabu zao zinaondoka.

“Watanzania wanakosa umeme wakati dhahabu zao zinaondoka, Watanzania wanakosa barabara wakati dhahabu zao zinaondoka, nataka ukakague kwa kina hii sekta ya madini ili Watanzania wajue chao nini na kama kinapatikana sawasawa,” alisisitiza Rais Magufuli.

Pia alimwagiza Waziri Mkuu Kassim Majaliwa kuitisha kikao cha pamoja kitakachomkutanisha CAG na mawaziri wote, makatibu wakuu wa wizara zote, Gavana wa Benki Kuu na wakuu wa taasisi za umma ili kila mmoja aambiwe hali ya hesabu katika taasisi yake na kuchukua hatua.

“Waziri Mkuu ukaongoze hicho kikao na wewe CAG uwaambie kila mmoja katika eneo lake juu ya dosari zake, sitaki kuona dosari zinajirudia zilezile kila wakati,” alisema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles