25.4 C
Dar es Salaam
Monday, November 18, 2024

Contact us: [email protected]

RIPOTI MAALUMU USALAMA BARABARANI : Uhaba magari ya wagonjwa hukwamisha uokozi kwa majeruhi

Na VERONICA ROMWALD – DAR ES SALAAM

HUU ni mwendelezo wa ripoti maalumu kuhusu usalama barabarani, katika makala haya mwandishi wetu ameangazia juu ya mfumo wa utoaji huduma kwa wagonjwa hasa majeruhi.

Wiki iliyopita pamoja na mambo mengine alieleza hali ya ajali nchini kwa ujumla na namna Jeshi la Polisi Kikosi cha Usalama Barabarani linavyopambana kuzitokomeza, endelea…

Julai 25, mwaka huu, majira ya jioni akiwa Mbezi Luis jijini hapa alijaribu kupiga namba hiyo mara kadhaa ambapo licha ya kuita kwa muda mrefu haikupokewa na kukata.

Alijaribu kwa mara nyingine napo iliita muda mrefu bila kupokewa kisha kukata, ilipofika usiku alijaribu tena kupiga nambari hiyo iliita bila kupokewa na kukata.

Mwandishi alijaribu tena kupiga nambari hiyo Julai 26, mwaka huu (siku iliyofuata) saa 11: 40 asubuhi iliita bila kupokewa na kukata.

Baada ya kuona hivyo, MTANZANIA lilimtafuta Msemaji wa Jeshi hilo, Inspekta Joseph Mwasabeja, na kumweleza juu ya jambo hilo ambapo kwanza alishangazwa na hali hiyo na kusisitiza simu hiyo ipo hewani na inafanya kazi.

“Siamini kama ulipiga na haikupokewa, tutajaribu hapa, nambari zetu wakati wowote zipo hewani,  lakini inawezekana kweli ulipiga na haikupokewa kwa sababu kinachotokea wananchi huwa wanafanya nambari zile ziwe ‘bize’ wakati wote.

“Unakuta mtu anapiga simu hana tukio, au anadanganya tukio, sasa wakati yeye ameshikilia laini, wewe unaitafuta na kuikosa ndipo inapotokea shida.

“Lakini tumeigawa ni rahisi na unahitaji tu kuwa na chaji ya kutosha na hata kama huna salio, inakwenda na inapokewa na maofisa wetu tayari kukusikiliza na kwenda kutoa huduma,” anasema.

Wakati mahojiano yalipokuwa yakiendelea katika ofisi ya jeshi hilo iliyopo ndani ya Wizara ya Mambo ya Ndani, Inspekta Mwasabeja aliamuru mmoja wa maofisa wa jeshi hilo kujaribu kupiga nambari hiyo ili kujiridhisha iwapo  inafanya kazi au la!

Awamu hii iliita na kupokewa. Hata hivyo, ofisa huyo alisema ilikuwa ni ya Wilaya ya Ilala.

 

Historia ya Jeshi

Anasema jeshi hilo liliundwa mwaka 1945 kipindi cha vita vya kwanza vya dunia na wakati huo lilikuwa linaitwa ‘The Police Fire Brigade’.

“Mwaka 1950 vilianzishwa vikosi mbalimbali vingine vikiwa kwenye Halmashauri za Miji na wakati huo vingine vilikuwa kwenye utumishi wa umma hasa katika Wizara ya Ujenzi.

“Awali kila kikosi kilikuwa kinajitegemea yaani iwe ni ndani ya Wizara ya Ujenzi, viwanja vya ndege, Bandari, vikosi vya mijini vilijitegemea, vilikuwa chini ya halmashauri za miji,” anasema.

Anaongeza: “Kwa mfano, Kituo cha Zimamoto (Ilala) kilichopo Fire kile kilijengwa mwaka 1954 na chief wa kwanza kukiongoza alikuwa Mzungu.

“Lengo lao wakati huo kwa kuwa vikosi vyote havikuwa majeshi na vilikuwa vinafanya kazi kwa kujitegemea chini ya halmashauri ya miji, tuliendelea kwenye mfumo huo hadi ilipofika 2007 ambapo Bunge lilianzisha Sheria namba 14 ya Jeshi la Zimamoto na Uokoaji.

“Hii ilikusanya vikosi vyote na kuviweka chini ya ‘Command’ moja na hapo ndipo tukaanza kupata Kamishna Jenerali wa kwanza wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Tanzania, anayesimamia hivi vikosi vyote na vipo chini ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi,” anaeleza.

Anasema tangu wakati huo, Kamishna Jenerali aliyekuwa wakati huo alivikusanya na kuvileta kwa pamoja kufanya kazi na hakukuwa tena na kundi la watu wa mijini na viwanja vya ndege.

“Isipokuwa wale wa bandarini bado hawajawekwa humu, hivi sasa mchakato unaendelea ili kikosi kile nacho kiwe ndani ya Jeshi kwa mujibu wa sheria,” anabainisha.

Anaongeza: “Katika malengo makuu ya jeshi hili ni kuokoa maisha na mali ingawa yapo mengi ambayo pia yanahusika lakini haya mawili ndiyo ambayo humgusa binadamu kwa namna moja au nyingine,” anasema.

Inspekta Mwasabeja anasema kwa upande wa mambo ya dharura, zile zote ambazo si za jinai zinalihusu jeshi hilo ikijumuisha uokozi kwenye maji, migodini, kuporomoka kwa majengo, mafuriko, maporomoko ya udongo, ajali za ndege na ajali zote za barabarani.

“Ajali za barabarani zinapotokea, tunawashauri Watanzania wote kutambua kwamba mdau mkuu ni Jeshi la Zimamoto na Uokoaji, wanapaswa kwanza kutupigia ili twende kuokoa maisha ya majeruhi.

“Ndipo wawasiliane na Jeshi la Polisi ili likapime ajali, lakini changamoto ni kwamba Watanzania wengi inapotokea ajali wanalisahau hili kwamba Jeshi la Zimamoto na Uokoaji ndiye mdau mkuu kwani tunavyo vifaa vyote vya uokozi,” anasema.

Anasisitiza: “Tunafanya kazi kwa ushirikiano wa karibu na wenzetu wa Jeshi la Polisi pindi inapotokea ajali na mara nyingi tunapokea taarifa kutoka kwao hivyo, sisi tunasonga mbele kwenda kuokoa watu.

“Wanasaidia kwa upande wa ulinzi hivyo watu wetu wanafanya kazi ya uokozi katika hali ya usalama,” anasema.

 

Uwezo wa Jeshi

Anasema askari wa Jeshi hilo kitaalamu wanamuita ‘First Aider’ yaani ndiye mtoa huduma wa kwanza.

Inspekta Mwasabeja anasema hiyo ni kwa sababu amesomea huduma ya kwanza, anajua namna gani ya kumsaidia majeruhi aliyeumia.

 

Magari ya wagonjwa hayatoshelezi

MTANZANIA lilihitaji kujua iwapo Jeshi hilo linazo gari za kubebea wagonjwa (ambulance) na iwapo zinatoshelezi mahitaji halisi katika kutoa huduma ya uokozi kwa majeruhi.

“Pamoja na gari za kuzima moto ‘Fire’ tunazo pia gari za kubeba wagonjwa (ambulance), hizi ni zile zilizojitosheleza ni tofauti kabisa na magari mengine ambayo yanaitwa ‘ambulance’ lakini hayana vifaa, haya yana vifaa vyote muhimu vinavyohitajika katika kumpatia mgonjwa huduma,” anasema Inspekta Mwasabeja.

Anasema jeshi hilo lina vituo katika kila mkoa.

“Lakini kwa kuwa hayatoshelezi katika baadhi ya vituo vyetu kuna magari ya kuzima moto pekee, kwa hapa Dar es Salaam kituo chetu cha Ilala ndicho kina ambulance moja na kwa upande wa mikoani ipo Mwanza, Iringa na Kagera,” anasema.

Anaongeza: “Tanzania nzima tuna vituo lakini pia tumeanza kujitanua zaidi na sasa tumefungua vituo katika wilaya 29 nchini na katika viwanja vya ndege 19 tunatoa huduma, bado tunazidi kusogeza huduma zetu kwa jamii.

“Serikali ya awamu ya tano inaliangalia Jeshi la Zimamoto na Uokoaji kwa namna ya pekee hivyo tunategemea tutakuwa na vifaa vya kutosha ili twende na viwango vya kimataifa.

 

Wanafanyaje kazi?

“Kwa kuwa vifaa tulivyonavyo havitoshelezi, huwa tunafanya kazi na hospitali za umma na binafsi, na tumeunganishwa na mfumo maalumu wa mawasiliano,” anasema.

“Inapotokea ajali, tukitumia mfumo huo hospitali zote zinapokea mawasiliano yetu na wote kwa pamoja tunaelekea katika eneo la tukio na huwa wanaleta ambulance zao na madaktari kwa ajili ya kutoa huduma,” anasema.

 

Tanzania Red Cross Society (TRCS)

MTANZANIA lilihitaji kujua pia namna Tanzania Red Cross Society (TRCS) kinavyoshiriki katika kutoa huduma za kwanza kwa wagonjwa hasa majeruhi wa ajali za barabarani.

Mratibu wa Huduma ya kwanza wa taasisi hiyo, Kheri Issa, anasema TRCS ilianzishwa rasmi kwa Sheria namba 71 iliyopitishwa na Bunge mwaka 1962.

“Kabla ya Uhuru Taasisi ilikuwa tawi la British Red Cross,  Mara baada ya Uhuru ndipo ilipopitishwa rasmi; ‘Tanganyika Red Cross Society’ na baada ya Muungano wa mwaka 1964Taasisi hiyo ilitambulika kwa jina la ‘Tanzania Red Cross Society’ ikitekeleza majukumu yake bara na visiwani.

“TRCS ni taasisi ya huduma za kibinadamu na ni kisaidizi cha Serikali/ mamlaka za umma wakati wa maafa na dharura,” anasema.

Anasema wakati wa dharura kuna nyenzo nyingi zinazotumika kusaidia watu kulingana na dharura husika na nyenzo mojawapo ni hiyo ya huduma za kwanza.

“Zipo nyenzo nyingi kutegemeana na dharura, ikiwa kuna dharura watu hawapati maji basi tutapeleka maji (water and sanitation), ikiwa kuna uhaba wa damu basi tunafanya uhamasishaji wa wachangia damu ili kupata damu inayohitajika, ikiwa watu wameharibikiwa makazi huwa tunatengeneza makazi ya muda kwa ajili yao,” anasema.

Anafafanua: “Huduma ya kwanza ni njia yoyote utakayoitumia lazima iwe imefanyiwa utafiti na ikaonekana inafaa. Kila mara, huwa kunakuwa na utafiti wa kisayansi kuangalia tija ya njia mbalimbali za huduma ya kwanza au kuvumbuliwa kwa teknolojia mpya. Taasisi ina utaratibu wa kutoa mafunzo ya msingi na yale rejelezi kulingana na jinsi ambavyo ushahidi wa kisayansi unavyoeleza.

“Kwa msingi huo, TRCS imewekeza katika mambo hayo makuu matatu, jambo la kwanza tunaendesha mafunzo ya wakufunzi, baadae wanakwenda kuendesha mafunzo kwa wale wanachama wetu tunaowatumia wakati wa dharura ili wawe na ujuzi.”

“Muda umefika sasa wa kuwekeza kwenye teknolojia na mbinu za kisasa na sasa tunatoa mafunzo kulingana na tafiti zinazofanyika, maana yake ni kwamba tunaanza kuwekeza upya  kulingana na wakati uliopo,” anasema.

Anaongeza: “Tunafanya hivyo kwa sababu kuna mabadiliko, fursa za uwapo wa vifaa vya kisasa inafungua milango ya kutoa huduma bora zaidi na kwa ufanisi.”

“Wakati tulionao kuna mashine za kusaidia kushtua moyo, zamani zilikuwa katika nchi zilizoendelea pekee lakini sasa zipo hadi katika nchi zinazoendelea, kuna mabadiliko makubwa, tutawafundisha ili wasiwe wageni wa vifaa na mbinu nyingine mpya,” anasema.

 

Wanamsaidiaje majeruhi?

“Huduma ya kwanza si tiba, ni msaada wa awali napatiwa majeruhi au mtu aliyeugua ghafla kwa nia ya kulinda uhai, kusitisha majeraha yasiendelee na kumuandaa mgonjwa kufika kituo cha tiba”.

“Hivyo, tunampatia huduma ya kwanza ili kumsaidia, kulinda uhai wake, kuzuia majeraha yasiendelee, kuzuia maumivu nakuanzisha mchakato wa kumsaidia kupona.

“Mgonjwa anapatiwa huduma ya kwanza kisha anampelekwa hospitalini kwa matibabu zaidi, huduma ya kwanza hutegemeana na aina ya jeraha, ikiwa mtu amevunjika kuna aina ya huduma ya kumpatia, ikiwa amepoteza fahamu kuna aina ya huduma ya kumpatia na hata matatizo mengine kuna huduma maalum za kuwapatia wagonjwa,” anabainisha.

Itaendelea…

Mwandishi wa makala haya ni miongoni mwa waandishi waliochaguliwa kushiriki mafunzo ya uandishi wa habari za usalama barabarani yanayotolewa na Shirika la Afya Duniani (WHO) kwa kushirikiana na Wizara  ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto na Jeshi la Polisi Kikosi cha Usalama Barabarani kupitia mradi wa Bloomberg (BIGRS).

- Advertisement -

Related Articles

1 COMMENT

  1. Kutokana na tatizo hilo la uhaba was magari Mungu atunusulu katika hilo.Maana tunaweza kuwa na magari yakutosha lakini kama Mungu ameruhusu no sawa na been re.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles