27.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, February 8, 2023

Contact us: [email protected]

RIPOTI MAALUMU: MTANDAO MPYA WIZI VIPURI VYA MAGARI

EVANS MAGEGE na FARAJA MASINDE-DAR ES SALAAM

KASI ya wizi wa vipuri vya magari sasa inadaiwa kufanywa na kutekelezwa chini ya mtandao mpya na mpana unaohusisha watu wa kada tano tofauti.

Kwa muda sasa kumekuwa na wimbi la wizi wa vipuri vya magari nchini, huku jambo hilo likibaki kama changamoto kubwa kwa vyombo vya dola.

MTANZANIA Jumapili katika uchunguzi wake ambao kwa nyakati tofauti, timu yake ya waandishi ilipiga kambi na hata kufanya mazungumzo ya siri na ya wazi na wafanyakazi wa maduka ya vipuri vya magari, gereji, na watu wanaojihusisha na biashara hiyo kwa kuuza vifaa ya wizi jijini Dar es Salaam, limebaini kuwa wizi huo sasa unahusisha pia makampuni makubwa.

Inadaiwa kuwa mbali na makampuni hayo, mtandao huo pia unaunganisha baadhi ya mafundi wakubwa wa magari ya kisasa katika gereji maarufu kama ‘za Wachina’, ‘Wakorea’ au zile zilizoingia mkataba na kampuni za bima.

Wengine walioko kwenye mtandao huo, ni baadhi ya watumishi wa kampuni zinazotoa huduma ya bima za magari, wenye maduka ya vipuri, waoshaji na wamiliki.

Katika uchunguzi wake, MTANZANIA Jumapili limebaini kuwa mtandao huo kwa sasa una nguvu kuliko ule wa wafanyabiashara wa magari ya wizi ambao ulitikisa kwa kiasi chake miaka ya nyuma.

Kwa mujibu wa uchunguzi huo jijini Dar es Salaam ambako kumekuwa na malalamiko mengi, maeneo ambayo yametajwa sana kuendesha biashara hiyo haramu ni Sinza, Mikocheni, Mwananyamala, Magomeni, Kinondoni, Ilala, Tabata Dampo, Kariakoo – Gerezani, Msimbazi na Temeke.

MTANDAO

Timu ya waandishi walioshiriki katika uchunguzi huu ambao baadhi walijifanya ni wateja, wengine wauzaji, wamebaini kuwa wizi wa vipuri vya magari hufanywa na makundi matatu ambayo yote huunganishwa na mtandao mmoja.

Kundi la kwanza linahusisha vibaka ambao kazi yao ni kuiba vipuri vyepesi kama redio, side mirror, power window, taa, vioo, shoo, AC na dash board.

Kundi la pili ni wamiliki wenyewe wa magari, ambao kutokana na tamaa ya fedha, baadhi yao hujiibia vipuri wenyewe na kisha kutoa taarifa katika kampuni zinazowapatia huduma ya bima ili waweze kufidiwa.

MTANZANIA Jumapili limedokezwa kuwa kampuni ya bima inapofanya uchunguzi na kumhakikishia mteja kuwa italipa fidia, mteja hurejesha vipuri vilevile vya gari lake hivyo kujipatia fedha ya bure.

Kundi la tatu ni lile linalohusika na kuiba gari zima na kulikata vipande kisha kuanza kuuza vipuri kwa kuvisambaza katika maduka mbalimbali.

Pia makundi hayo matatu yanatajwa kuwa na ushirika wa karibu na baadhi ya mafundi kutoka gereji kubwa zikiwamo zile zinazomilikiwa na raia wa kigeni hasa kutoka China na Korea au zile zenye mkataba na kampuni za bima.

Ndani ya mtandao huo, wanatajwa pia baadhi ya watumishi wa kampuni zinazotoa huduma ya bima za magari ambao wanadaiwa kushirikiana ama na mteja au gereji na hivyo kunufaika na fedha ya fidia ya bima inayolipwa kwa mwathirika.

Kwa msingi huo, watumishi hao wa kampuni za bima wanatajwa kushiriki mipango ya magenge ya wizi wa vipuri ikiwa ni pamoja na kuviiba vile vya wateja wao.

“Mchezo wa kuiba unapofanikiwa vipuri hupelekwa katika gereji hizo kubwa na mara nyingi watumishi hao wa bima kwa mfano mwathirika akitoa taarifa kwamba kaibiwa, utasikia anampangia gereji ya kupeleka gari kwa ajili ya ukarabati na huko ndiko ambako vipuri hivyo vilikofichwa.

“Sasa kazi inayofanyika pale ni kurejesha vipuri vya gari hiyo na fedha ya fidia inayotolewa na kampuni ya bima inakuwa imemnufaisha mtumishi asiye mwaminifu, ambaye amejihusisha na mpango wa wizi huo pamoja na mafundi wachache wa gereji husika,” anasimulia mfanyabiashara wa vipuri hivyo ambaye jina lake tunalihifadhi kwa sababu za kiusalama.

Mfanyabiashara huyo ambaye mmoja wa waandishi walioshiriki katika timu hii ya uchunguzi aliunda naye urafiki kwa miezi kadhaa  anasema: “Siyo jambo rahisi kugundua mchezo huu kwani unachezwa kwa umakini wa hali ya juu mno, kiasi kwamba unaibiwa bila kujua kinachoendelea, wanachokifanya wanahakikisha kuwa wanakufuatilia ili kufahamu unakoishi wakisaidiwa na baadhi ya taarifa zako ambazo tayari watu wa bima wanazo.

“Hivyo wakishatambua vyema maeneo unayoishi au unayopendelea kuegesha gari lako mara kwa mara, huo ndio mwanya wanaoutumia kukuumiza bila ya wewe kujua.”

Mbali na watumishi wa bima, baadhi ya madereva walioajiriwa na wamiliki wa magari, au kampuni nao wametajwa kuwamo katika mtandao huo.

 VIFAA VINAVYOIBWA SANA

Vifaa ambavyo vimekuwa vikitajwa kukimbiliwa na wezi hao, ni vile vyenye thamani kubwa kama control box, side mirror, power window, vioo, taa, dash board, redio na baadhi ya vifaa vya injini huku wakilenga zaidi magari yenye thamani kubwa.

Kwa mujibu wa watu wanaoshiriki katika mtandao huo, magari ambayo wamekuwa wakiyalenga na ambayo mara nyingi vifaa vyake huhitajika, ni aina ya Toyota Vitz, Passo, Carina, Premio old model, Toyota Allion, Mark II Gx110, Brevis, Verossa, Premio new model, Spacio new model na Toyota IST.

Na kwa upande wa magari yenye thamani kubwa ambayo vifaa vyake vinawindwa sana ni pamoja na BMW, Nissan Rogue, Lexus, Klugger, Harrier na mengine.

 SABABU ZA WIZI

Umasikini unatajwa kuchochea vijana wengi kujihusisha na wizi huo wa vifaa vya magari.

Inaelezwa kuwa ili kufanikisha wizi, vijana hao wamekuwa wakitumiwa na genge la wezi wa vipuri vya magari, kuonyesha mazingira na kutoa taarifa za kiusalama katika makazi ya baadhi ya wamiliki wa magari wanaowafahamu.

Sababu nyingine inayoelezwa kuwa chanzo cha kuendelea kwa wizi huo, ni pamoja na kuwapo kwa mafundi wa magari wasio waaminifu, ambao wamekuwa wakitumia mwanya wa kuaminiwa na wamiliki wa magari kuchonga funguo za ziada ambazo huzitumia kufungua gari kwa siri na kuiba baadhi ya vipuri au kuiba gari zima ili likakatwe vipande vipande na kuuza vipuri vyake.

 WAOSHA MAGARI

Kundi jingine linalotajwa kushirikiana na wezi kwa kiwango kikubwa ikiwamo kuchongesha funguo za magari na kisha kuanza kulifuatilia ili kuiba vipuri vyake ni waosha magari.

Kwa sababu hiyo, wamiliki wa magari wanapaswa kuwa makini na watu wanaowaoshea magari na inashauriwa kutomuachia funguo.

 GEREZANI – KARIAKOO

Uchunguzi wa gazeti hili ulianzia katika eneo la Gerezani, Kariakoo ambako ni maarufu kwa uuzaji wa vipuri vya magari.

Mmoja wa waandishi wa habari hii aliyejivika uhusika wa mtu aliyeibiwa power window na taa za gari lake aina ya Toyota IST maeneo ya Kigogo Fresh, alifika katika eneo hilo na kuzungumza na baadhi ya wafanyabiashara.

 “Kaka karibu sana, hapa ndio Gerezani, kila kitu utapata. Vipi unatafuta vifaa vya namna gani? Funguka, kuwa huru tu,” alisema kijana mmoja aliyejitambulisha kwa jina moja la Hemed.

Wakati mwandishi akiendelea kutafakari, Hemed aliendelea kupigia chapuo vifaa vinavyopatikana kwenye duka lake kwa madai kuwa ni imara na kwamba havijaibwa mahala popote.

“Unajua hapa ukisema umsikilize kila mtu ‘watakuingiza chaka’ hawa, we cha msingi njoo tuzungumze ili tuone ni namna gani unaweza kupata vifaa kwa bei rahisi, au unahitaji vilevile vyako?” alihoji Hemed.

Mwandishi alimjibu kuwa iwapo kama angesaidiwa kuvipata vilevile vya kwake lingekuwa ni jambo jema zaidi, lakini akajibiwa kwamba hilo lisingewezekana kulingana na mazingira ya sasa.

“Kaka nakwambia zunguka hapa pote hutopata hivyo vifaa vyako, wewe cha masingi hapa hakikisha tu kwamba unatoa pesa hapa nikupe vitu vingine ambavyo ni ‘super’ kabisa, lakini kusema kuwa utapata hivyo vya kwako hapo siyo leo,” alisema.

MTANZANIA Jumapili lilidokezwa kuwa katika miaka ya hivi karibuni eneo hilo limepunguza kwa kiasi kikubwa kuuza vifaa ya wizi tofati na lilivyokuwa likisifika awali.

 “Vifaa hivyo kwenye maduka yaliyopo Gerezani, Ilala na Tandale vimepungua kwa kiwango kikubwa, wamiliki wa magari wanaogopa sana kununua siku hizi, lakini sikatai kwamba hakuna wanaouza japo nakuhakikishia kabisa kuwa kama wapo basi wanafanya kwa ujanja wa hali ya juu mno, maana huwezi kufanya mchezo huo na Serikali hii ya sasa, wakikudaka si ni balaa,” alisema Hemed.

 MADUKA YA TANDALE

Sufian Suleiman anayemiliki duka la vipuri vya magari katika eneo la Tandale, anabainisha kuwa wao wamekuwa wakijihusisha na uuzaji wa vifaa vinavyotoka katika magari mengi yanayopata ajali na kuharibika kabisa tofauti na inavyoelezwa kuwa wamekuwa wakishiriki kununua vifaa vya wizi.

“Unajua hizi habari zimekuwapo siku nyingi sana na hakuna mtu yeyote ambaye amewahi kuja mfano kwangu kupata ukweli kama wewe ulivyofanya juu ya kinachofanyika, wengi huamini kuwa spea hizi tunazouza zote tunaletewa kutoka kwenye magari yaliyoibwa.

“Kinachofanyika ni kuwa huwa tuna makubaliano na wamiliki pindi magari yao yanapokuwa yamegongwa na kuharibika vibaya, huwa wanatuuzia hivyo vifaa au tunakubaliana kuwa pindi kifaa chake kitakapopata soko kuna pesa ambayo atapata, lakini siyo kwamba huwa tunapokea mzigo wa wizi la hasha… mimi ninachojua ni kwamba wizi huo umeisha kabisa siku hizi, hasa katika Serikali hii mpya, hakuna kabisa kitu kama hicho ikilinganishwa na uongozi uliopita,” alisema Suleiman.

 KAMPUNI ZA BIMA

Kutokana na tuhuma nyingi kuelekezwa kwenye kampuni za bima, MTANZANIA Jumapili lilipita kwenye baadhi ya kampuni za bima likiwamo Shirika la Bima la Zanzibar na lile la Jubilee.

Imam Ally Makame ambaye ni kiongozi wa kanda wa Shirika la Bima la Zanzibar, alipoulizwa juu ya baadhi ya kampuni za bima kujihusisha na mtandao wa wizi wa vipuri vya magari, alionekana kushtushwa na taarifa hiyo, lakini akasema kuwa jambo hilo linawezekana kwa kampuni ambazo wafanyakazi wao si waaminifu.

“Upande wetu sisi kama Zanzibar hatuna gereji zetu kama ilivyo kwa kampuni nyingine ambazo zimekuwa zikishirikiana na gereji kutoa huduma kwa wateja wao.

“Hivyo kwetu sisi hili halipo kwani mteja akipata tatizo tunakagua na tukijiridhisha tunamlipa pesa yake moja kwa moja, na hata wafanyakazi wetu wamekuwa ni watu ambao wanahudumu kwa uaminifu mkubwa kulingana na wito wa kazi wao unavyowataka kufanya, hivyo hakuna mtu yeyote anayeweza kujihusisha na vitendo visivyofaa,” alisema Makame.

Alisema kuwa changamoto ambazo zimekuwapo katika huduma yao hiyo, ni pamoja na baadhi ya wateja wasiokuwa waaminifu kuondoa vifaa vya magari yao na kuvificha na kisha kudai kutaka kulipwa na bima.

“Japo kwetu sisi changamoto kubwa imekuwa ni katika ajali za kila siku, lakini pia kumekuwapo na changamoto hii ya ukosekanaji wa uaminifu kutoka kwa baadhi ya wateja kwani wapo wanaoiba kwa namna mbalimbali, ikiwamo kupandisha bei ya kifaa kilichoibwa kwa lengo la kujipatia kipato na pia wapo ambao wamekuwa wakificha magari yao ili tu kutaka kulipwa na kampuni,” alisema.

Chanzo kingine kutoka katika Kampuni ya Bima ya Jubilee ambacho hakikutaka kutajwa gazetini kwa sababu za kutokuwa msemaji, kilieleza kuwa mtandao huo inawezekana ukawapo kulingana na watu kuwa na akili nyingi, lakini kwa upande wao hawajawahi kupata kesi kama hiyo.

 JESHI LA POLISI

Jeshi la Polisi nchini lilipoulizwa lilisema kuwa linafanyia kazi taarifa za kuwapo kwa mtandao huo wa wizi wa vipuri vya magari, ikiwa ni pamoja na kukusanya taarifa za matukio yote ya aina hiyo kwa nchi nzima na kuahidi kutoa taarifa kamili siku chache zijazo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
208,871FollowersFollow
561,000SubscribersSubscribe

Latest Articles