25.6 C
Dar es Salaam
Wednesday, January 19, 2022

RIPOTI MAALUMU: MAPATO YAPOROMOKA, MATUMIZI JUU

Na JUSTIN DAMIAN,

RIPOTI ya hali ya uchumi kwa mwezi Machi iliyotolewa na Benki Kuu ya Tanzania (BoT) hivi karibuni, inaonyesha hali kutokuwa nzuri kutokana na malengo ya makusanyo kutofikiwa, huku matumizi yakizidi malengo.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo,  Serikali ilijiwekea malengo ya kukusanya Sh bilioni 492.8 kutoka kwenye bidhaa zinazoingizwa kutoka nje ya nchi, lakini badala yake ilifanikikwa kukusanya Sh bilioni 408.6, ikiwa na maana kuwa ilishindwa kukusanya kiasi cha Sh bilioni 84.2.

Kupitia kodi ya mapato, lengo ilikuwa ni kukusanya Sh bilioni 626.3, lakini makusanyo halisi yalikuwa ni Sh bilioni 559.5, ikiwa na maana kuwa Sh bilioni 66.8 hazikuweza kukusanywa kama ilivyotarajiwa.

Malengo ya makusanyo kutoka katika vyanzo visivyo vya kikodi yalikuwa ni Sh bilioni 226.7, huku makusanyo halisi yakiwa Sh bilioni 97.6, ikiwa na maana kuwa kiasi cha Sh bilioni 129.1 hakikuweza kukusanywa.

Serikali pia ililenga kukusanya Sh bilioni 91.8 kupitia vyanzo vingine vya kodi, lakini iliweza kukusanya Sh bilioni 86.7, huku Sh bilioni 5.1 zikishindwa kukusanywa.

Kwenye vyanzo vyote vitano ambavyo Serikali ililenga kukusanya mapato kulingana na ripoti hiyo, ni chanzo kimoja tu ambacho kimeweza kufanya vizuri kwa kufikia malengo.

 Chanzo hicho ni makusanyo kupitia bidhaa za ndani na huduma. Malengo yalikuwa ni kukusanya Sh bilioni 250.0, lakini makusanyo halisi yalikuwa ni Sh bilioni 256.3, ikimaanisha Sh bilioni 6.3 zilikusanywa juu ya lengo.

Sehemu nyingine ambayo Serikali ilikuwa ikitarajia kupata fedha ni ruzuku. Lengo lilikuwa ni kupata Sh bilioni 146.2, lakini iliweza kupata Sh bilioni 14.2, huku kiasi cha Sh bilioni 132 kikishindwa kupatikana.

Matumizi ya Serikali yapanda na kushuka

Katika kipindi hicho cha mwezi Machi, Serikali ilijiwekea makadirio ya kutumia Sh bilioni 551.6 kulipa mishahara kwa watumishi wa umma, lakini ilitumia Sh bilioni 529.2, ikifanikiwa kuokoa Sh bilioni 22.4.

Serikali ilikadiria kutumia Sh bilioni 298.5 kulipa riba za mikopo yake mbalimbali, lakini ilitumia Sh bilioni 232.6, ikifanikiwa kuokoa Sh bilioni 65.9.

Katika kipindi hicho hicho, Serikali ilikadiria kutumia Sh  bilioni 393.0 kwa shughuli za kimaendeleo kwa fedha zinazotokana na vyanzo vya ndani, lakini ilifanikiwa kutumia Sh bilioni 235.7 ikiacha pengo la Sh bilioni  157.3.

Kwenye matumizi mengine yasiyo ya kimaendeleo, makadirio yalikuwa ni kutumia Sh bilioni 392.8, lakini zilitumika Sh bilioni 397.9, ikiwa na maana Sh bilioni 5.1 zilitumika juu ya lengo.

Matumizi kwa shughuli za maendeleo kupitia fedha za kutoka nje, makadirio yalikuwa ni kutumia Sh bilioni 112.5, lakini zilitumika Sh bilioni 225.4 ikiwa ni ongezeko la Sh bilioni 112.9.

Bei za mazao ya vyakula zapanda

Ripoti hiyo pia inaonyesha   kupanda kwa bei ya mazao ya chakula katika kipindi cha mwezi Machi, mwaka huu, ukilinganisha na kipindi cha mwezi Machi mwaka uliopita.

Zao la mahindi ndilo linaloonekana kuongoza kwa kupanda bei likifuatiwa na mtama.

Taarifa hiyo kwa upande mwingne inafafanua kuwa akiba ya chakula hadi kufikia mwishoni mwa mwezi Machi ilikuwa tani 84,666 na kuongeza kuwa hakuna chakula kilichouzwa au kununuliwa kwa kipindi cha mwaka huu.

Wasomi, wanasiasa wazungumza

Profesa Honest Ngowi ambaye ni mhadhiri wa uchumi Chuo Kikuu cha Mzumbe tawi la Dar es Salaam, aliliambia gazeti hili kuwa kushindwa kufikiwa kwa malengo kunaweza kuwa kumesababishwa na sababu mbalimbali.

Alieleza baadhi ya sababu kuwa ni pamoja kuweka malengo makubwa ambayo kiuhalisia utekelezaji wa kuyafikia unakuwa mgumu kutokana na hali halisi ya uchumi wa nchi kwa sasa.

Akitolea mfano wa kodi ya mapato ambayo lengo la makusanyo limeshindwa kufikiwa, Profesa Ngowi alisema kodi hiyo hutozwa kwenye faida ambayo hutengenezwa na makampuni na biashara mbalimbali.

“Sasa hivi biashara nyingi hazifanyi vizuri sana na kwa hiyo hata faida inayotengenezwa ni ndogo. Hii ina maana kuwa kodi inayolipwa pia ni ndogo,” anaeleza Profesa Ngowi.

Aliongeza kuwa katazo la kusafirisha mchanga wa dhahabu ambalo Serikali imelitangaza, limeathiri mapato ya makampuni yanayosafirisha bidhaa hiyo jambo ambalo pia limeathiri kodi ambayo Serikali ilikuwa ikipata kabla ya katazo.

“Makampuni ya bia yamekuwa yakilalamika kushuka kwa mapato kutokana na katazo la kuuza bidhaa kama pombe ya kwenye viroba. Hii yote inaweza kuwa na athari ya moja kwa moja kwa kodi kwa kuwa Serikali haiwezi kupata kiasi ilichokuwa ikipata mwanzoni,” alifafanua.

Kwa upande wake, Profesa Haji Semboja ambaye ni mhadhiri wa uchumi kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, alisema TRA haipaswi kulaumiwa kwa kushindwa kufikia malengo kwa kuwa hali ya uchumi katika eneo la Kusini mwa Jangwa la Sahara si nzuri kwa ujumla.

Alisema hali mbaya katika eneo hilo imeiathiri Tanzania pia na kwa hiyo suala la kutofikiwa malengo kwenye makusanyo si la kushangaza.

Profesa Semboja alitaja sababu nyingine ambayo inaweza kuwa imechangia ni ukosefu wa mvua.

“Uchumi wa Tanzania kwa kiasi kikubwa unategemea kilimo na hasa kinachotegemea mvua, kwa kipindi kirefu mvua hazikuwepo na kwa hiyo hili liliathiri uchumi pia,” alisema.

Mtaalamu huyo wa uchumi alisema msisitizo mkubwa ambao umewekwa kwenye sekta ya umma, huku sekta binafsi ikipewa msukumo mdogo, inaweza kuwa sababu ya kushindwa kufikiwa kwa malengo.

Naye Mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe (ACT-Wazalendo), alisema kuna haja Serikali itazame upya sera zake za kiuchumi.

“Utaona kuwa vyanzo vyote vya mapato makusanyao yamekuwa chini ya kiwango. Hii inadhihirisha kuwa hali ya uchumi na uzalishaji imeshuka na hivyo kuathiri mapato ya Serikali,” alisema.

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
175,234FollowersFollow
531,000SubscribersSubscribe

Latest Articles