26.9 C
Dar es Salaam
Thursday, April 25, 2024

Contact us: [email protected]

Ridhiwani: Mwacheni baba apumzike

Na GRACE SHITUNDU – DAR ES SALAAM

MBUNGE wa Chalinze Ridhiwani Kikwete ambaye pia ni mtoto wa Rais Mstaafu, Jakaya Kikwete amewataka watu hasa wa kwenye mitandao ya kijamii wanaompelekea  malalamiko baba yake, kumuacha apumzike katika kipindi chake hiki alichostaafu.

Kauli hiyo ya Ridhiwani ilikuja baada ya kutuma picha ya katika ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa Instagram inayoonyesha nyumbani kwa Mzee Kikwete huko Msoga.

Katika picha hiyo Ridhiwani ambaye ni mtoto wa kwanza wa Rais mstaafu Kikwete aliambatanisha na maneno machache; “Nyumbani Msoga #MsogaUlaya #BarakaYa Mvua”.

Baada ya andiko lake hilo baadhi ya wanaomfuatilia katika ukurasa wake huo wa Instagram walimwambia amsalimie Rais Mstaafu na kudai kwamba wamemkumbuka.

Mmoja kati ya wafuasi hao aliyetambulika kwa jina la Robinson Bumela naye aliandika; “Msalimie Mzee mwambie sekta binafsi imekufa”.

Kutokana na kauli hiyo Ridhiwani uzalendo ulionekana kumshinda na kumjibu moja kwa moja; “Muacheni apumzike”.

Katika siku za karibuni imeonekana baadhi ya watu wakitumia kivuli cha hotuba na kauli za Kikwete kutoa maoni waliyonayo.

Hali hiyo ilijitokeza wiki mbili zilizopita baada ya Rais huyo Mstaafu Kikwete kutoa hotuba yake  katika kongamano la Kumbukizi ya Miaka 20 tangu kifo cha Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere na kuibua neno ‘Kujimwambafai’ akiwa na maana ya kujikweza.

Neno hilo lilizua mjadala huku kila mmoja akilitumia neno hilo kwa namna yake kwa jinsi walivyolitafsiri.

 Kutokana na mijadala iliyokuwa ikiendelea Katibu wa Rais Mstaafu alitoa taarifa ilionyesha kusikitishwa na upotoshaji wa baadhi ya watu kuhusiana na hotuba hiyo.

Katika taarifa hiyo Kikwete aliwataka watu kuwa na ujasiri wa kutoa  maoni yao na kuacha tabia ya kujificha katika kivuli cha hotuba zake.

Alieleza kusikitishwa na upotoshwa unaofanywa na baadhi ya watu kuhusu hotuba yake kwani katika hotuba yake hiyo alieleeza alivyokuwa anamfahamu Mwalimu Nyerere kulingana na mada iliyokuwa katika kongamano hilo na si vingivevyo.

Taarifa hiyo ilieleza kuwa cha kushangaza wamejitokeza watu wanaopotosha ukweli kuhusu maneno aliyosema Rais Mstaafu , kwamba wapo wanaojaribu kumuwekea maneno kinywani mwake ambayo hakuyasema hususani waliodai kuwa alikuwa anawasema baadhi ya viongozi waliopo sasa.

Taarifa hiyo ilieleza kuwa  kamwe Rais huyo mstaafu hakuzungumzia mtu mwingine yoyote zaidi ya Mwalimu Nyerere.

Katika hotuba yake ya Oktoba 8 Rais Mstaafu Kikwete alisema Mwalimu alikuwa anaheshimu utu wa mtu na alikuwa hajikwezi kwa kuwa ni kiongozi mkubwa bali alikuwa ni ‘humble man, simple’.

Alisema kwa namna alivyokuwa anaishi na watu, mtu akikaa naye hapati hofu ya kwamba amekaa na Rais.

Alisema kwamba alifanya hivyo kwa sababu ya kusisitiza utu, hivyo mtu hata akiwa ana dhamana ya uongozi haifanyi kuwa ni mtu zaidi  ya raia mwingine au una haki zaidi ya mwingine.

Alisema mambo hayo yaliyoyafanya Mwalimu Nyerere ni vyema viongozi wakayatambua kuwa kujishusha hakuwezi kumfanya asiwe kiongozi na kujimwambafai (kujikweza) hakukufanyi kuwa kiongozi zaidi.

Kikwete katika hotuba yake hiyo aliongea mambo mengi ya Mwalimu Nyerere ambayo alisema baadhi ya mambo yameshakuwa tunu za taifa

Mambo mengine aliyosisitiza Kikwete ni amani na umoja ambao alisema Mwalimu Nyerere aliujenga.

Alisema pamoja na kuwa na itikadi tofauti ya vyama vya siasa, dini tofauti na makabaila zaidi ya 120 lakini Mwalimu aliwaweka watanzania pamoja tunu ambayo inapaswa kutunzwa .

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles