24.2 C
Dar es Salaam
Thursday, April 25, 2024

Contact us: [email protected]

Repoa, CRDB kufanya utafiti kuboresha huduma kwa wateja

Na MWANDISHI WETU-DAR ES SALAAM

BENKI ya CRDB imeingia makubaliano na Taasisi ya Utafiti ya Repoa, kufanya tafiti zitakazosaidia kuboresha huduma kwa wateja na kusaidia jitihada za Serikali katika kukuza uchumi.

Akizungumza jana wakati wa kusaini mkataba wa makubaliano hayo, Ofisa Mkuu wa Biashara wa CRDB, Dk. Joseph Witts, alisema tafiti hizo zinalenga kuboresha huduma kwa wateja kwa kuja na suluhisho la changamoto mbalimbali na kusaidia jitihada za Serikali za kukuza uchumi.

Alisema tafiti za Repoa zimetumiwa katika kutunga sera na mikakati mbalimbali ya maendeleo nchini, ikiwamo Dira ya Maendeleo ya Taifa ya 2025, Mkakati wa Taifa wa Kumaliza Umasikini (NPES), Mkakati wa Ufadhili kwa Tanzania (TAS), Mkakati wa Kupunguza Umasikini (PRSP) na Mkakati wa Kukuza Uchumi na Kupunguza Umasikini (Mkukuta).

 “Benki ya CRDB inatambua umuhimu wa tafiti za kisayansi katika kuchochea maendeleo ya nchi kwa kusaidia katika utungaji wa sera na mikakati mbambali ya maendeleo. Repoa itaisaidia benki kufanya tafiti mbalimbali ambazo zitasaidia kuboresha huduma na mikakati mbalimbali ya maendeleo ya nchi.

“Benki ya CRDB ni kubwa nchini, hatufikirii tu ushindani uliopo ndani, tunafikiria masoko ya nje pia, tupo Burundi lakini kuna masoko mengine tunayafikiria, kwahiyo ili kuweza kuingia lazima uwe na tafiti zenye viwango vya kimataifa, uweze kujua yakoje, mahitaji yaliyopo na mambo mengine,” alisema Dk. Witts. 

Kwa mujibu wa Dk. Witts kupitia makubaliano hayo, Repoa pia itawajengea uwezo wafanyakazi wa benki hiyo katika kufanya tafiti mbalimbali.

“Kupitia tafiti tumekuwa tukijua mahitaji halisi ya wateja, kubuni bidhaa na huduma bora zinazokidhi mahitaji ya wateja na kuweka mikakati mbalimbali ya kibiashara ili kuongeza ushiriki wa benki katika kupunguza umasikini na kukuza uchumi wa taifa letu,” alisema Dk. Witts.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Repoa, Dk. Donald Mmari, alisema wapo tayari kushirikiana na CRDB ili kuleta mabadiliko chanya na kuongeza ufanisi katika maeneo mbalimbali ya kiutendaji ya benki hiyo.

 “Ushirikiano huu utasaidia kuijenga Benki ya CRDB na wafanyakazi wake kwenye uwezo wa kufanya tafiti mbalimbali, huku lengo likibaki kuwahudumia vyema Watanzania na kushiriki kikamilifu katika kuleta maendeleo nchini,” alisema Dk. Mmari. 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles