31.2 C
Dar es Salaam
Friday, October 11, 2024

Contact us: [email protected]

Rekodi zilizobeba matumaini ya Simba Algeria

Na MOHAMED KASSARA – DAR ES SALAAM

WAWAKILISHI wa Tanzania katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika, Simba, wamesafiri jana kwenda Algeria kwa ajili ya kuikabili JS Saoura katika mchezo wa hatua ya makundi  wa michuano hiyo.

Kikosi cha Simba kiliondoka  jana mchana kwenda Algeria kupitia Dubai kwa ajili ya mchezo wa marudiano wa hatua makundi Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi JS Saoura utakaochezwa Jumamosi kwenye Uwanja wa Stade 20 Août 1955 uliopo mjini Bechar.

Wekundu hao wa Msimbazi wanakwenda Algeria wakiwa na mtaji wa mabao 3-0 walioupata katika mchezo wa kwanza uliochezwa  Desemba mosi mwaka jana kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Simba imeondoka na msafara wa wachezaji 20, benchi la ufundi pamoja na baadhi ya viongozi kuelekea mchezo huo.

Timu hiyo inakwenda Algeria ikijiamini baada ya kupata ushindi wa bao 1-0 dhidi ya miamba ya soka Afrika, Al alhly katika mchezo wao wa mwisho uliochezwa Februari 12, mwaka huu, Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Ushindi huo ulifufua upya matumaini ya Simba kutinga robo fainali ya michuano hiyo, baada ya kufikisha pointi sita na kushika nafasi ya pili kwenye msimamo wa kundi D, nyuma ya Al alhly yenye pointi saba, JS Saoura ikishika nafasi ya tatu ikiwa na pointi tano, huku AS Vita ikiburuza mkia na pointi zake nne.

Baada ya kuichapa Al alhly, Simba imeendeleza makali yake kwa kushinda michezo mitano mfululizo ya Ligi Kuu iliyofuata na kufunga mabao 15 kwenye michezo hiyo.

Hata hivyo, wapinzani wao wana historia nzuri kwenye uwanja wao wa nyumbani, mara ya mwisho ilipoteza mchezo Januari 4, mwaka huu walipochapwa bao 1-0 na Kabylie katika mchezo wa Ligi Kuu nchini humo.

Lakini katika michuano ya Ligi ya Mabingwa, JS Saoura imecheza michezo miwili katika uwanja wao huo na kuambulia pointi nne, baada ya kushinda mchezo mmoja dhidi ya AS Vita na kutoka sare ya bao 1-1 na Al ahly.

JS Saoura imecheza michezo miwili ugenini kwenye michuano hiyo na kuvuna pointi moja, tofauti na Simba ambayo haijaambulia kitu katika mechi zake mbili za ugenini kwenye michuano hiyo.

Simba kwa upande wao, imevuna pointi zote sita katika michezo yake miwili ya nyumbani, baada ya kuanza kuichapa JS Saoura mabao 3-0, kabla ya kuidungua Al alhly bao 1-0.

Tangu Simba na Soura zilipovaana Januari 12, kila moja imeshashuka dimbani mara tisa, zikiwamo mechi za Ligi ya Mabingwa, Waalgeria wakifungwa mbili kama ilivyo kwa wenzao Wekundu wa Msimbazi.

Saoura imecheza michezo sita ya ligi na kushinda miwili, sare miwili na kupoteza idadi kama hiyo, michezo mitatu ya Ligi ya Mabingwa Afrika, ikishinda mmoja na kutoka sare miwili.

Timu hiyo tayari imeshashuka dimbani mara 22, ikishinda mechi zao nane, ikitoa sare saba na kufungwa saba, wanashika nafasi ya nne katika msimamo wa Ligi Kuu ya Algeria.

Katika michezo yote hiyo, Saoura imefunga mabao nane na kuruhusu wavu wake kutikiswa mara nane pia.

Simba kwa upande wao, imecheza michezo sita ya ligi na kushinda yote, michezo mitatu ya Ligi ya Mabingwa ikishinda mmoja na kuchapwa miwili.

Katika michezo hiyo, Simba imefunga mabao 16 na kuruhusu mabao 10.

Wekundu hao wa Msimbazi tayari wameshacheza michezo 20  ya ligi msimu huu, wakishinda 16, wakitoa sare tatu na kupoteza mmoja.

Wachezaji hatari kwenye eneo la ushambuliaji la Saoura ni Moustapha Djallit, Ziri Hammar, Mohamed Hammia na Mohamed Boulaouidet, lakini ukweli ni kwamba kwa pamoja wameipachikia timu yao jumla ya mabao 12 msimu huu wa Ligi Kuu ya Algeria, kila mmoja akizipasia nyavu mara tatu.

Hakuna ubishi kuwa takwimu hizo zinawatupa mbali, endapo watafananishwa na makali ya safu ya ushambuliaji ya Wekundu wa Msimbazi msimu huu, ambapo Kagere na nahodha wake, Jonh Bocco, wameshachangia  mabao 21 hadi sasa na hiyo ni kwa mechi za Ligi Kuu pekee. Kagere amefunga mabao 12, huku Bocco akiwatungua walinda mlango mara tisa.

Hata hivyo, takwimu zinaonesha kuwa Simba imeruhusu nyavu zake kutikiswa mara nyingi zaidi (16), ukilinganisha  na Saoura (8), hivyo wakati Wekundu wa Msimbazi wakitambia makali ya washambuliaji wao, Emmanuel Okwi na Kagere, wasisahau kuwa ‘ukuta’ wao unapaswa kuwa makini kwa dakika zote 90 za mchezo huo.

Udhaifu mkubwa katika eneo la ulinzi la Simba kwa takwimu za kimataifa walizocheza msimu huu, ni umakini mdogo katika kuzuia hatari zitokanazo na mipira ya krosi, kama ambavyo Al Ahly walinufaika na uzembe huo kupata mabao yao matatu katika mchezo wa kwanza ambao Wekundu wa Msimbazi walichapwa 5-0.

Kama hiyo haitoshi, mabao mawili ya AS Vita wakati Simba wakiangukia pua kwa kipigo kama hicho, pia yalitokana na kosa la aina hiyo kwani mabeki wa Wekundu wa Msimbazi walizembea, wakashindwa kumzuia nyota wa AS Vita aliyeruka na kupiga kichwa mpira uliomshinda kipa Aishi Manula.

Hata hivyo, Simba itashuka Algeria ikiwa na kumbukumbu nzuri ya kupata kuitupa nje timu ya USM El Harrach nchini Algeria mwaka 1993 katika mchezo wa robo fainali ya Kombe la Caf.

Simba ilianza kwa kupata ushindi wa mabao 3-0 nyumbani, kabla ya kupoteza ugenini kwa mabao 2-0 katika mchezo wa marudiano, hivyo kusonga jumla ya mabao 3-2.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
590,000SubscribersSubscribe

Latest Articles