27.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, October 16, 2024

Contact us: [email protected]

REKODI ZA NDEGE ZAMUUMBUA TRUMP

NEW YORK, MAREKANI


RAIS Donald Trump, mara mbili alimdanganya aliyekuwa Mkurugenzi wa Shirika la Upelelezi Marekani (FBI), James Comey, kuwa hakutumia hata usiku mmoja wakati alipohudhuria shindano la Miss Universe mjini Moscow, Urusi mwaka 2013.

Rekodi za ndege na mitandao ya jamii zimeonyesha alikuwa Moscow kwa siku tatu.

Trump anadaiwa kudanganya ili kukwepa kuonyesha ukaribu wake na Urusi, ambayo inatuhumiwa kuingilia Uchaguzi Mkuu wa 2016 Marekani ili kumsaidia dhidi ya mpinzani wake Hillary Clinton, madai ambayo amekuwa akiyakana.

Lakini rekodi za ndege, ambazo mtandao wa Bloomberg imezipata pamoja na mitandao ya jamii, ikiwamo alizoweka mwenyewe kwenye akaunti yake, Trump alikuwa Urusi kuanzia Ijumaa Novemba 8, 2013 hadi siku ya tatu – Jumapili asubuhi.

Kwa mujibu wa maelezo ya Comey, ambaye Trump alimfukuza kutoka FBI, Mei 9 mwaka jana kwa kile kilichoonekana kutofurahishwa na uchunguzi kuhusu uhusiano wake wa Urusi, rais huyo alisema ziara ya Moscow ilikuwa ya haraka mno kiasi kwamba hakupata fursa ya kuonja japo usiku mmoja.

Trump alikanusha kwa mara ya kwanza juu ya uwepo wake nchini Urusi, wakati wa chakula cha usiku Ikulu mjini hapa mwishoni mwa Januari 2017.

“Alisema aliwasili asubuhi, kisha kuoga na kuvaa kwa ajili ya shindano hotelini, na kisha kwenda kwenye tukio.

“Baadaye baada ya shindano, alirudi hotelini kukusanya vitu vyake kwa sababu waliondoka usiku ule ule kuelekea New York kwa ndege.

“Katika tukio la pili Februari 2017 Ikulu, Trump alirudia tena kuwa hakulala wakati wa ziara ya Urusi kuhudhuria shindano la Miss Universe,” aliandika Comey.

Lakini rekodi zilizokusanywa na mtandao huo zimeonyesha Trump alianza safari yake kuelekea Moscow kutokea North Carolina, ambako alihudhuria siku ya kuzaliwa kwa mhubiri Billy Graham, ambaye sasa ni marehemu Alhamisi ya Novemba 7, 2013.

Rekodi za ndege zinaonyesha ndege ya Trump mwenyewe – Cessna, ilirudi New York usiku huo ikitokea Asheville, North Carolina bila uwapo wa rais huyo.

Kwa mujibu wa ripoti ya gazeti la New York Times Januari 2017, badala yake, Trump alielekea Moscow kwa ndege binafsi ya Bombardier Global 5000 iliyomilikiwa na Phil Ruffin, mshirika wake katika Hoteli ya Kimataifa ya Trump na Jengo la kibiashara huko Las Vegas.

Trump kutumia ndege ya Ruffin pia kumeripotiwa katika kitabu kipya cha Russian Roulette, kinachozungumzia harakati za Rais wa Urusi, Vladimir Putin dhidi ya Marekani na kuchaguliwa urais kwa rais wake.

Kwa mujibu ya mmoja wa waandaaji wa Miss Universe, Aras Agalarov, ndege hiyo ilitua Moscow Ijumaa ya Novemba 8 uwanja wa ndege wa Vnukovo, mwendo wa saa isiyozidi moja kwa gari hadi Hoteli ya Ritz-Carlton, ambayo Trump alifikia.

Trump aliibuka katika mtandao wa Facebook baadaye siku hiyo akiwa kwenye mgahawa wa Nobu Moscow kabla ya kuhudhuria sherehe ya kuzaliwa ya Agalarov usiku wa siku hiyo.

Mchana wa siku iliyofuata, picha zilizowekwa Facebook zilimwonyesha akiwa Ritz Hotel na jioni akaeleza katika akaunti yake ya twitter yuko ziarani Moscow.

Usiku wa Jumamosi akahudhuria shindano la Miss Universe lililofuatiwa na tafrija iliyofanyika saa 7 usiku Jumapili.

Baada ya hapo akaondoka Moscow kwa ndege aliyokwenda nayo ya mshirika wake Ruffin saa 9:58 alfajiri na kuwasili uwanja wa ndege wa kimataifa wa Newark Liberty nje kidogo ya Jiji la New York City.

Jioni ya Jumapili, Trump alituma taarifa katika twitter akisema: “Ndiyo nimerudi kutoka Urusi. Nimejifunza mengi mno. Moscow kunavutia na ni mahali kwa aina yake!”

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
590,000SubscribersSubscribe

Latest Articles