REKODI YA GABORONE YAIPA UJASIRI YANGA

0
1001

MOHAMED KASSARA-DAR ES SALAAM

KIKOSI cha wawakilishi wa Tanzania katika michuano ya kimataifa, Yanga kinatarajia kutua leo, jijini Cairo, Misri tayari kuikabili Pyramids katika mchezo wa marudiano wa Kombe la Shirikisho Afrika utakaopigwa Jumapili kwenye Uwanja wa June 30.

Licha ya kupoteza mchezo wa kwanza uliochezwa Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza, kwa mabao 2-1, vijana hao wa Mwinyi Zahera wanaamini watapindua meza ugenini kama walivyofanya walipoitungua Township Rollers kwao.

Timu hiyo ilianza kulazimishwa sare ya bao 1-1 na Rollers katika mchezo wa kwanza wa hatua ya awali ya Ligi Mabingwa Afrika nyumbani, lakini ilishinda ugenini bao 1-0 katika mchezo wa marudiano uliopigwa Mjini Gaborone.

Hata hivyo, Yanga inahitaji kupata ushindi wa kuanzia mabao 2-0 dhidi ya Pyramids  ili kufuzu hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho.

Kikosi cha wachezaji 20, benchi la ufundi na viongozi watatu uliondoka jana usiku kuelekea Misri kwa ajili ya mchezo huo wa marudiano ukiwa matumaini makubwa ya kufanya vizuri.

Wachezaji walioondoka jana ni makipa, Farouk Shikalo, Metacha Mnata na Ramadhan Kabwili, huku mabeki wakiwa ni Juma Abdul, Ally Ally, Ally Mtoni ‘Sonso’, Lamine Moro na Muharami Said Issa ‘Marcelo’.

Viungo ni nahodha Papy Tshishimbi, Feisal Salum ‘Fei Toto’, Mapinduzi Balama, Abdulaziz Makame, Deus Kaseke, Jaffar Mohammed, Mrisho Ngassa, Patrick Sibomana na Issa Bigirimana, wakati washambuliaji ni Sadney Urikhob na Juma Balinya.

Akizungumza na MTANZANIA jana, Mkuu wa Kitengo cha Habari na Mawasiliano  wa Yanga, Hassan Bumbuli kikosi hicho kinaondoka kikiwa na matumaini makubwa ya kufanya vizuri ugenini.

“Kikosi kipo tayari kwa mapambano, tunakwenda Misri tukijua tuna kazi nzito ya kufanya, lakini tuna imani kila kitu kinawezekana iwpo tu wachezaji watashika maagizo ya kocha na kujituma.

“Tuna hakika bado tuna nafasi ya kufuzu hatua ya makundi, tunajua wengi wametukatia tamaa kutokana na matokeo ya nyumbani, tutafanya yale tuliyofanya Gaborone na kuwaacha midomo wazi,” alisema Bumbuli.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here