24.8 C
Dar es Salaam
Friday, October 4, 2024

Contact us: [email protected]

Rekebisha hili ili mahusiano yako yadumu

UHUSIANO wowote makini unadumu kutokana na nguvu za waliopo katika mahusiano hayo. Mapenzi hayadumu kwa sababu yanatakiwa kudumu. Busara, malengo na utulivu wa wapendanao wanaojenga mahusiano husika ndiyo chachu ya mahusiano hayo kudumu.

Ili mahusiano yako yaweze kudumu ni lazima ujione una jukumu kubwa la kufanya katika kudumisha penzi lako. Lipi unalifanya ili mahusiano yako yawe imara?

Wewe ni mwaminifu kwa mwenzako? Msikivu, unamjali na kumpa heshima, ni mbunifu na mwenye kuitaka furaha ya mwenzako muda mwingi?

 Mahusiano mengi yanashindwa kudumu kwa sababu wengi wanayoyajenga ni wabinafsi. Hakuna mahusiano makini yanayoweza kujengwa wahusika wakiwa wabinafsi.

 Unakuta mtu yeye ndiyo anataka kila siku aanze kujuliwa hali, asikilizwe yeye na abembelezwe yeye tu. Njia kuu ya kujenga uimara wa mapenzi ni kumfikiria mwenzako katika uzito mkubwa unaostahili.

Sasa jiulize, kwa kuwa kwako mbinafsi, ni kwa namna gani mwenzako atajihisi amani na furaha ya kuwa na wewe? Na kama mwenzako akiacha kupata raha na faraja kamili kutoka kwako, hayo mahusiano yatakuaje?

 Unakuta mtu anamwona mwenzake hana furaha ama muda mwingi yuko na ghadhabu. Badala ya kuwa mpole, mnyenyekevu na kumuuliza mwenzake kwa upendo  nini kinamsibu, yeye anaanza kudai mwenzake kabadilika.

 Kila kitu katika maisha kina sababu yake. Mwenzako huenda kakerwa kazini, huenda biashara zake haziendi sawa, huenda kuna taarifa za kuumiza kapata, sasa usiwe na haraka kukimbilia kutoa hukumu juu ya hali yake.

Kaa naye kwa upendo kisha sema naye taratibu. Bila kujua uhalisia wa hali ya mwenzako na wewe kukimbilia kutoa hukumu, si tu unamkosea ila pia unalegeza kamba iliyoshikilia uhusiano wenu.

Mapenzi ni kubembelezana, kuoneana huruma siyo kutunishiana misuli ama kukomoana. Mahusiano ya mapenzi yaliodumu kwa muda mrefu ni yale ambayo wahusika waliamua kwa dhati kujitoa kwa wenzao.

Yaani waliamua kuwasikiliza, kuwajali na kufanya mengi ya kuwafurahisha wenzao.

Wanawake wengi wanakosea katika namna ya kuishi na waume zao katika nyumba. Wanawake wanatakiwa kutambua kuwa mipango ya kifedha ya mwanaume ikiwa inaenda mrama, akili yake haiwezi kuwa sawa hata kidogo.

Kwa sababu mwanamume kaishi akifundishwa kuwa fedha na mali ndiyo silaha muhimu za kumlinda na kumjenga. Sasa kiumbe huyu mwenye imani hii akiikosa pesa siyo tu anajihisi mnyonge ila pia anaona kama anaingia katika dunia ya kudharaulika na kitwana.

 Mwanamke makini anatakiwa kujua namna ya kuishi na mwanaume ambaye anapitia katika changamoto hii. Mwanaume ambaye yuko katika kipindi kigumu cha kifedha huwa hana amani, wakati mwingine huwa mkali na hukaa kinyonge. Katika hali hii mwanamke anatakiwa awe mjanja kumuelewa.

Ajue katia hali hii, huyu anahitaji kusikilizwa zaidi, anahitaji kupewa nafasi zaidi na pia ahitaji kubembeleza sana labda kubembelezwa.

 Bahati mbaya wanawake wengi wakiona mwanaume anakuwa hovyo kitabia, anakuwa mkali, wao hukimbilia kudai wamechokwa. Wao hukimbilia kudai mwanaume husika kapata mchepuko nje. Tafsiri za hovyo kabisa.

 Pia mwanaume anatakiwa kuishi na mwanamke kwa akili na maarifa sana. Wakati mwingine kuna hisia zinamvaa mwanamke na kujikuta akisema mambo ambayo hata hamaanishi.

 Unaweza kukuta mwanamke yuko na mume wake halafu anasema ‘sijui nitapendwa na nani mimi’. Kauli hii haifai kumvuruga mwanaume. Kauli hii hutamkwa na wanawake ili kutaka kupata uhakika kama kweli wanapendwa na kujaliwa.

 Badala ya kukasirika, mwanaume hapa anatakiwa kuonesha ni kwa namna gani anampenda na kumuhitaji mwanamke husika. Anatakiwa aongee naye kwa utulivu huku akionesha wazi ni kwa namna gani anampenda na kumjali.

 Kitaalamu wanawake ni watu ambao hata uwajali vipi, uwasikilize vipi ila huona bado tu kuna kitu unatakiwa kufanya zaidi kuonyesha upendo wako kwao. Hili suala lisikusumbue sana. Ni ulemavu wao.

 Unachotakiwa kufanya ni kuacha kukimbilia katika kutoa hukumu. Onyesha upendo wako kwake, uonesha unavyomjali na kumthamini. Kujiona ni fundi sana wa kutoa hukumu katika kauli za mwenzako siyo tu utakaribisha matatizo katika mahusiano yako ila pia utamfanya muhusika akuone mtu usiyejali na kuthamini.

 Ili kuishi kwa amani katika uhusiano wako, jifunze kuwa na udhibiti wa hisia zako. Acha kuruhusu kupelekwa puta na hisia zako. Kuwa na udhibiti nazo ili uweze kutoa maamuzi ya maana na ya kujenga.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
590,000SubscribersSubscribe

Latest Articles