26.5 C
Dar es Salaam
Sunday, July 21, 2024

Contact us: [email protected]

REA, wadau wakubaliana kuunganisha usimamizi miradi ya umeme vijijini

Na Veronica Simba – Lindi

Wakala wa Nishati Vijijini (REA) na Wadau wake mbalimbali mkoani Lindi, wamekubaliana kuunganisha nguvu katika kusimamia utekelezaji wa miradi ya umeme vijijini ili kuhakikisha inakamilika kwa wakati na viwango vinavyotakiwa.

Azimio hilo limefikiwa leo Januari 27, 2023 katika kikao kazi kilichojumuisha Ujumbe kutoka REA ukiongozwa na mmoja wa Wajumbe wa Bodi ya Nishati Vijijini, Oswald Urassa, Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Lindi ambaye ni Katibu Tawala wa Mkoa huo Ngusa Samike, Ujumbe kutoka TANESCO, Wabunge wa Lindi pamoja na Wakandarasi wanaotekeleza miradi ya umeme vijijini mkoani humo.

Mjumbe wa Bodi ya Nishati Vijijini (REB), Oswald Urassa akizungumza wakati wa kikao cha Wadau wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA) Mkoa wa Lindi, kilichoketi kujadili namna bora ya utekelezaji wa miradi ya umeme vijijini mkoani humo, Januri 27, 2023 katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa. Kushoto kwake ni Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Lindi ambaye ni Katibu Tawala wa Mkoa huo, Ngusa Samike pamoja na wa kwanza kulia ni Mbunge wa Kilwa Kusini, Ally Kasinge.

Akizungumza na Waandishi wa Habari, Urassa amesema kikao kimekubaliana kuwa kila Mkandarasi atatakiwa kuandaa na kuwasilisha Mpango Mkakati unaodadavua namna atakavyotekeleza kazi zake kwa mlengo wa kukamilisha Mradi kwa wakati.

Akifafanua, amesema Mpango Mkakati huo utaainisha taarifa ya kila wiki na kila mwezi kuanzia sasa hadi Aprili 30 mwaka huu ambayo ndiyo siku ya hitimisho kwa kila mmoja kuwa amekamilisha na kukabidhi Mradi.

Amesema Bodi ya REA itahakikisha inafuatilia kwa ukaribu na hatua kwa hatua, utekelezaji wa Mradi kwa kila Mkandarasi ili malengo ya Serikali kuwekeza fedha nyingi kwa ajili ya kuwapelekea huduma ya umeme wananchi waishio vijijini itimie.

“Fedha hizi ni za wananchi hivyo ni lazima zitumike kama inavyopaswa. Hivyo, ni jukumu lenu ninyi Wakandarasi kuhakikisha mnatimiza makubaliano yetu tuliyoazimia leo ya kukamilisha miradi kwa wakati,” amesisitiza Mjumbe huyo wa Bodi.

Akizungumza katika kikao hicho, Mwakilishi wa Mkurugenzi Mkuu wa REA, Mhandisi Thomas Mbaga amewaasa Wakandarasi kuheshimu Mikataba yao ya kazi na kutenda kadri inavyoelekeza ili kuepuka changamoto mbalimbali.

Aidha, amesema kuwa katika kuhakikisha Miradi inatekelezwa na kukamilishwa kwa wakati, REA imemwongezea nguvu kazi Mshauri Mwelekezi kwa kuongeza idadi ya wasimamizi wa miradi kutoka 10 hadi 20.

Vilevile amesema REA imejipanga kuhakikisha kwamba kila Mkoa unakuwa na usimamizi thabiti wa miradi na kwamba itaendelea kushirikiana na TANESCO katika kutekeleza kazi hiyo.

Mhandisi Mbaga amesema Mpango Kazi utakaowasilishwa na Wakadarasi sasa utatumika kama ‘Msahafu’ kwa wote ikiwemo REA, TANESCO na wadau wengine hivyo ndiyo utakaotumika kwa wakandarasi wenyewe kujihukumu kutokana na kazi itakayofanyika.
“Tutawapima kulingana na huo Mpango Kazi ili kuhakikisha juhudi za Serikali katika kuwapelekea umeme wananchi wa vijijini zinazaa matunda,” amesisitiza.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa kikao hicho, Kaimu Mkuu wa Mkoa, Ngusa Samike amesema Serikali ina nia njema kuwatumia wakandarasi wazawa kwani miradi hiyo wangepewa wageni, asilimia kubwa ya fedha ingeenda nje ya nchi.

Ni kwa sababu hiyo, Kaimu Mkuu wa Mkoa amewataka wakandarasi walioaminiwa na Serikali kutoipoteza imani hiyo kwa kutekeleza kwa viwango na wakati miradi husika.

“Mliomba kazi, mkapewa kazi, fanyeni kazi kwa uaminifu. Ni wakati sasa wa kuidhihirishia Serikali kuwa imani iliyowapatia haipotei bure ili muendelee kuaminiwa,” amesisitiza.

Mbunge wa Kilwa Kusini, Ally Kasinge akizungumza wakati wa kikao cha Wadau wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA) Mkoa wa Lindi, kilichoketi Januri 27, 2023 kujadili namna bora ya utekelezaji wa miradi ya umeme vijijini. Kushoto kwake ni Mkuugenzi wa TANESCO Kanda ya Kusini Mhandisi Felician Makota.

Aidha, amesema Ofisi ya Mkuu wa Mkoa itafuatilia kikamilifu makubaliano ya kikao hicho ambacho kimepitisha azimio la kwamba baada ya mwezi mmoja kutoka siku ya kikao, utafanyika ufuatiliaji kuona kila mkandarasi anavyotekeleza maagizo ya kuongeza kasi ya kazi ambapo hatua itakayokuwa imefikiwa itatoa dira endapo Mradi utakamilika kwa wakati au la na kuchukua hatua stahiki.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti, Meneja Mradi wa Kampuni ya White City International Contractors LTD, Mhandisi Jacqueline Mushi na Meneja Mradi wa Kampuni ya Nakuroi Investment Company Limited, Mhandisi William Madibu wameahidi kufanyia kazi makubaliano ya kikao hicho na kwamba watakamilisha miradi kwa wakati.

Kikao hicho kilihudhuriwa pia na Mbunge wa Kilwa Kusini, Ally Kasinge pamoja na Makatibu wa Wabunge wa Mkoa wa Lindi ambao wote wamepongeza hatua ya REA kukutana na Wadau ili kuweka mikakati ya pamoja katika kusimamia utekelezaji wa miradi ya umeme vijijini katika Mkoa wa Lindi.

Taarifa ya Msimamizi wa Miradi ya REA Mkoa wa Lindi, Mhandisi Daniel Mwandupe inaeleza kuwa mkoa huo una jumla ya vijiji 524 ambapo kati yake, vyenye umeme ni 326 na vilivyobaki 198 vitapatiwa umeme kupitia Mradi wa REA Awamu ya Tatu Mzunguko wa Pili kwa gharama ya Sh bilioni 71.9.

Kampuni mbili za Ukandarasi zinatekeleza Mradi wa Umeme Vijijini Awamu ya Tatu mkoani Lindi ambapo kampuni ya Nakuroi Investment inatekeleza katika Wilaya za Kilwa, Lindi Vijijini na Ruangwa huku kampuni ya White City ikitekeleza katika Wilaya za Liwale na Nachingwea.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles