30.2 C
Dar es Salaam
Saturday, April 20, 2024

Contact us: [email protected]

RC aomba Wizara ya Fedha kusaidia wakulima walipwe fedha za pamba

Derick Milton -Simiyu

MKUU wa Mkoa wa Simiyu, Antony Mtaka, ameiomba Wizara ya Fedha na Mipango, kuingilia kati suala la malipo ya wakulima wa pamba ambapo mpaka sasa katika mkoa wake asilimia 27 ya wakulima wa zao hilo bado hawajalipwa.

Aliomba wizara hiyo kuangali jinsi gani wataweza kuingilia kati suala hilo kwani ndiyo yenye dhamana na benki ili kuhakikisha wanunuzi wanapata pesa za kuwalipa wakulima hao.

Mkuu huyo wa mkoa alitoa ombi hilo jana mbele ya Naibu Waziri wa Wizara ya Fedha, Dk Ashatu Kijaji, wakati wa ziara aliyofanya mkoani humo kukagua ujenzi wa Chuo cha Usimamizi wa Fedha (IFM) tawi la Simiyu.

Alisema wakulima wameendelea kudai malipo yao na sasa msimu mwingine wa kilimo umeanza wakati baadhi ya wakulima wakiwa hawajalipwa.

Mtaka aliiomba wizara hiyo kuwaita wanunuzi na wadau wengine wa pamba ili wajadiliane na kujua walipokwama wanunuzi hao.

Alisema Serikali kupitia Benki Kuu iliweza kuingilia kati suala hilo na kuwapa pesa baadhi ya wanunuzi ili wanunue pamba, lakini bado wakulima wameendelea kudai malipo yao.

“Ni vyema wizara kuingilia suala hili kwa kukutana na wanunuzi na wadau wengine, tujue kama zile pesa ambazo walipewa na benki zilipelekwa kununua pamba? Tujie wapi wamekwama ili tuweze kusaidia suala hili,” alisema Mtaka.

Kwa upande wake Dk Kijaji, aliahidi kulifanyia kazi suala hilo na kuahidi kuwa wakulima wote ambao wanadai watalipwa fedha zao.

 “Asilimia 27 ni wakulima wengi, nimelipokea na naenda kulifanyia kazi haraka sana, niwahakikishie wakulima watalipwa pesa zao zote, kama wizara tutaangalia jinsi gani ya kuhakikisha wakulima wanalipwa,” alisema Dk. Kijaji.

Akitoa taarifa ya ujenzi wa tawi hilo Makamu Mkuu wa chuo hicho, Prof. Thadeo Sata, alisema hadi kufikia Machi, 2020 tawi hilo litaanza kufanya kazi kwa kupokea wanafunzi wenye wa astashahada, na shtahada.

“Ujenzi wa majengo kwenye tawi hilo ulianza Julai mwaka huu na kwa awamu ya kwanza inatagharimu Sh milioni 900, jengo la utawala limefikia asilimia 62 na madarasa asilimia 92,” alisema Prof. Sata.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles