28.7 C
Dar es Salaam
Wednesday, January 19, 2022

RC Pwani ampa siri tatu Sawala

Na GUSTAPHU HAULE-PWANI

MKUU wa Mkoa wa Pwani, Evarist Ndikilo, amemuapisha Mkuu wa Wilaya mpya wa Rufiji Luteni Kanali Patrick Sawala na kumtaka aende kufanyakazi ya kuwahudumia wananchi kwa kutatua kero zao.

Sawala aliapishwa jana katika ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani hafla ambayo ilishuhudiwa na  kamati ya ulinzi na usalama, Katibu Tawala wa Mkoa huo Dk. Delphine Magere, familia ya Sawala pamoja na waandishi wa habari.

Katika hafla hiyo Ndikilo, alimueleza Mkuu huyo wa Wilaya kuwa Rufiji kuna changamoto nyingi na aende kufanyakazi kulingana na kiapo chake huku akisema kila kitu kilichopo ndani ya Wilaya hiyo kinamhusu.

Ndikilo alisema jambo kubwa analotakiwa kulifanya ni kuhakikisha anakwenda kudumisha ulinzi na usalama  ili wananchi wake waishi kwa amani  itakayowasaidia kufanya shughuli zao hususani kilimo kwa uhuru.

Aidha, Ndikilo alitaja kero ya migogoro ya wakulima na wafugaji kuwa changamoto kubwa Wilayani humo na kwamba lazima aweke mikakati ya utatuzi wake na ikiwezekana ashirikiane na wananchi kikamilifu katika kushughulikia kero hiyo.

Akifafanua kuhusu kilimo Ndikilo alisema kuwa Wilaya ya Rufiji ni maarufu kwa kilimo cha korosho na ufuta kwani mazao hayo yamekuwa yakiongeza pato la mkoa na Taifa kwa asilimia kubwa huku aliongeza mwaka 2019/20 korosho ziliingiza bilioni 60 wakati ufuta ukiingiza bilioni 12.

“Nenda Rufiji … jitahidi ukijue kila kitu kwakuwa vyote vinakuhusu kwani hakuna jambo ambalo halitakuhusu”alisema Ndikilo.

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Rufiji, Luteni Kanali Patrick Sawala, akizungumza na waandishi wa habari alisema kuwa ameyachukua maelekezo aliyopewa na anakwenda kuyafanyia kazi kikamilifu.

Sawala alisema ametambua ipo kero ya wakulima na wafugaji, migogoro ya ardhi na changamoto nyingine za kijamii hivyo yupo tayari kuzipa kipaumbele changamoto hizo kwa kutafuta ufumbuzi wake.

Alisema atahakikisha anashirikiana na wananchi wa Wilaya hiyo katika utekelezaji wa majukumu yake ili waweze kutatuliwa kero zao kwa urahisi zaidi .

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
175,266FollowersFollow
531,000SubscribersSubscribe

Latest Articles