29.2 C
Dar es Salaam
Friday, November 15, 2024

Contact us: [email protected]

RC Mwanza, OUT kujenga madarasa gereza la Butimba

Na Clara Matimo, Mwanza

OFISI ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza kwa kushirikiana na Chuo Kikuu Huria Tanzania (OUT) wameanza mchakato wa kujenga madarasa mawili na ofisi moja katika gereza kuu la Butimba lililopo jijini Mwanza ili kuwapa fursa wafungwa wenye sifa za kusoma elimu ya juu kutimiza ndoto zao bure.

Hayo yameelezwa na Mkuu wa Mkoa huo, Adam Malima Machi 27, 2023 jijini humo wakati akifungua mafunzo kwa washauri nasaha ambao watawaongoza wanafunzi na wasimamizi wa madawati ya kijinsia katika chuo hicho mikoa yote 31 nchini, ambayo yamefanyika Chuo Kikuu Huria Tanzania (OUT) tawi la Mwanza.

Washiriki wa mafunzo ambao watawaongoza wanafunzi na wasimamizi wa madawati ya kijinsia katika Chuo Kikuu Huria Tanzania (OUT), wakimsikiliza Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Adam Malima (aliyesimama mbele)wakati akizungumza kwenye ufunguzi wa mafunzo hayo.

Malima ambaye pia ni Mwenyekiti wa kamati ya ushauri ya chuo hicho amesema ujenzi wa madarasa hayo utatoka kwenye mradi wa madarasa 1,100 yaliyotolewa na Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, ambapo amewataka wanasheria wa mkoa, OUT na Magereza kuandaa hati ya makubaliano (MOU) kufanikisha mkakati huo.

Amesema lengo ni kuwawezesha wafungwa katika gereza kuu la Butimba kusoma masomo ya chuo kikuu ambapo kupitia mpango huo wataweka mazingira salama kwa wafungwa na serikali.

“Serikali ya mkoa wa Mwanza tunakwenda kujenga madarasa mawili na ofisi ili wafungwa wasome wenzetu wa jeshi la magereza watatusaidia eneo, mafundi kwenye ujenzi na vitendea kazi ikiwamo madawati, tutajenga madarasa ya mfano.

“Tulichogundua watu wengi mle ndani (Butimba) wanataka kusoma kuna wafungwa 1,800 kati ya hao hawakosi 50 wanaohitaji elimu ya juu tunao mfano mzuri wa mfungwa mmoja kutoka gereza hilo ana kifungo cha muda mrefu alianza kusoma diploma kwa sasa ana degree na bado anahitaji kuendelea kwa hiyo chuo hiki kitawapa fursa watu kama hao,” amesema Malima.

Akizungumzia ukatili wa kijinsia, Malima amewataka watu wote wanaojihusisha na unyanyasaji kwa wanawake na watoto kuacha mara moja kwani watakaobainika serikali haitawafumbia  macho.

“Wito wangu kwenu wote washiriki wa mafunzo haya hakikisheni mnazielewa vizuri mada zote mtakazofundishwa  ili mwende kuwa njia ya kupokea malalamiko kwa wanaonyanyaswa na wanaonyanyasa wakikosa pa kutokea matukio ya unyanyasaji  yatapungua,”amesema Malima.

Washiriki wa mafunzo ambao watawaongoza wanafunzi na wasimamizi wa madawati ya kijinsia katika Chuo Kikuu Huria Tanzania (OUT), wakimsikiliza Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Adam Malima (aliyesimama mbele)wakati akizungumza kwenye ufunguzi wa mafunzo hayo.

Mkuu wa Magereza Mkoa wa Mwanza, Justin Kaziulaya amesema kumuendeleza mfungwa ni jambo la muhimu na wanaliunga mkono kwani ni utaratibu ambao wanaamini wadau wote watauridhia kwa kuwa  wafungwa hao pia wana watu wanaowategemea wakiwamo watoto na wazazi hivyo kuendelezwa kwao  ni kumsaidia anaporejea uraiani kujikimu kimaisha,  kujisimamia na kushawishi watu wengine kusoma.

Naye Mshauri Msaidizi wa wanafunzi Chuo Kikuu Huria Tanzania (OUT), Sophia Nchimbi amesema ni utaratibu wa chuo hicho kutoa elimu magereza ambapo wamekuwa wakiwatembelea na kuwapa mitihani huku wafungwa wengi wakipendelea kusoma sheria ili kuwasaidia wenzao walioko gerezani na hawana msaada wa kisheria.

“Tumeweka malengo mahsusi kusaini MOU (mkataba wa makubaliano) baina ya chuo Kikuu Huria Tanzania, magereza na ofisi ya mkuu wa mkoa kufungua madarasa hasa katika mkoa huu wa Mwanza ambayo yatasaidia kuwafundisha wale ambao wamefungwa lakini wanataka kujiendeleza kimasomo,”

“Ni nafasi nzuri ambayo mkuu wa mkoa ameichukua kwa kipaumbele zaidi na kusaini MOU kwa kuhakikisha kesho kabla hatujamaliza mafunzo haya mkataba huu unasainiwa kwahiyo ni utaratibu mzuri ambao tunauweka na utakaokuwa na tija kubwa kwa wafungwa ambao watapata nafasi ya kutimiza malengo yao ikiwemo ajira baada ya kumaliza vifungo vyao,” amesema Nchimbi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles