*Ni katika maeneo ya Soko kuu, Stendi ya mabasi
Na Clara Matimo, Mwanza
Ili kuhakikisha kunakuwa na usawa na kuondoa urasimu katika utoaji wa vyumba vya biashara kwenye miradi mipya ya Soko Kuu la Jiji la Mwanza na Stendi Kuu ya Mabasi yaendayo mikoani ya Nyegezi, watumishi wa umma wametahadharishwa kutojirundikia vyumba kisha kuvipangisha kwa bei ya juu.
Onyo hilo limetolewa na Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Mhandisi Robert Gabriel, Mei 10, mwaka huu wakati wa ziara yake ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa miradi hiyo inayojengwa wilaya ya Nyamagana mkoani humo.
Alisema serikali inatekeleza miradi kwa lengo la kuwanufaisha wananchi wake na kuweka bei ya chini ili waweze kumudu gharama za uendeshaji wa biashara zao lakini baadhi ya watumishi wa umma wenye tamaa na wanaopenda kujinufaisha wenyewe wanakuwa madalali.
“Mkuu wa wilaya ya Nyamagana unafahamu, tulikuwa wote pale makoroboi tulikuta kibanda cha halmashauri cha 200,000 walioko mle ndani wanamlipa tajiri Sh 1,000,000 ina maana anachukua cha juu Sh 800,000, akiwa na vibanda 10 anaingiza Sh milioni nane kwa mwezi mshahara ambao hata mkuu wa mkoa haupati mtu mmoja ametulia anawanyonya wananchi.
“Kiwango kisiwe kikubwa sana cha kumuumiza mfanyabiashara wala kisiwe kidogo cha kuvutia watu wachache kutumia mwanya huo kujinufaisha, twende na bei halisi ya soko, fedha lazima zirudi kwenye baadhi ya maeneo lakini wafanyabiashara wanufaike,”alisema Mhandisi Gabriel.
Mhandisi wa jiji la Mwanza, Tunaye Mahenge, alisema miradi yote miwili ujenzi wa soko kuu la mjini kati ambao umetekelezwa kwa asilimia 73 na stend kuu ya mabasi nyegezi uliofikia asilimia 85 ilitarajiwa kukamilika Aprili mwaka huu lakini imekwama kutokana na changamoto mbalimbali.
Alizitaja baadhi ya changamoto hizo kuwa ni pamoja na eneo kuwa na chem chem ya maji kutoka chini hali iliyosababisha kubadili mchoro wa msingi ili uendane na hali ya eneo katika mradi wa ujenzi wa stendi kuu ya mabasi nyegezi, upandaji horera wa bei za vifaa vya ujenzi unaoweza kuongeza gharama za utekelezaji wa miradi hiyo, vifaa kutopatikana kwa wakati kutokana na ugonjwa wa uviko 19.
“Changamoto hizo zimesababisha mkandarasi Mohammedi Builders Ltd, anaetekeleza mradi wa ujenzi wa soko kuu la mjini kati kwa gharama ya Sh bilioni 20,739,695,080 aombe kuongezewa muda wa miezi mitano huku mkandarasi wa stendi ya nyegezi anayetekeleza mradi huo kwa gharama ya Sh bilioni 15, 885, 589,063 yeye ameomba aongezewe muda wa miezi mitatu.
Mradi wa ujenzi wa soko ulianza kutekelezwa Oktoba, 2020 huku wa stend ya mabasi nyegezi ukianza Februari 5, 2019 lengo likiwa ni kuboresha huduma, kuongeza mapato ya halmashauri ya Jiji la Mwanza ili iweze kujitegemea na kupunguza utegemezi kutoka serikali kuu.