24.8 C
Dar es Salaam
Friday, November 8, 2024

Contact us: [email protected]

RC Mwanri atoa kauli taarifa za utekaji watoto Tabora

MURUGWA THOMAS Na ALLAN VICENT


MKUU wa Mkoa wa Tabora, Aggrey Mwanri ameitisha kikao cha dharura cha Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa  kujadili madai ya kutekwa wanafunzi huku akiliagiza jeshi la polisi kufanya uchunguzi wa kina.

Vilevile  aliliagiza Jeshi hilo kufanya doria ya saa 24 kuanzia jana katika maeneo yote ya manispaa hiyo  kudhibiti matukio ya uhalifu wa aina yoyote.

“Hatuwezi kupuuza uvumi au maneno yanayosemwa na wananchi hata kidogo, nataka hatua za haraka zichukuliwe kuwaondolea hofu wananchi na kukomesha tabia zozote zisizo na staarabu,” alisema.

Hiyo ni kutokana na kutanda taharuki katika Halmashauri ya Manispaa ya Tabora baada ya kuwapo   taarifa za kutekwa wanafunzi wawili wa Shule ya Msingi Chemchem   katika manispaa hiyo.

Hali hiyo ilisababisha sintofahamu kubwa miongoni mwa wakazi wa manispaa hiyo wakiwamo wazazi na walezi na wanafunzi wa shule hiyo   ikizingatiwa kuwa  umekuwapo   uvumi wa vitendo vya utekaji watoto vinavyofanywa na watu wasiojulikana katika mitaa mbalimbali ya mji.

Hata hivyo Jeshi la Polisi mkoani Tabora lililazimika kuwatawanya wananchi waliokuwa wakiandamana kwa nia ya kufanya vurugu wakidai jeshi hilo limeshindwa kuwakamata watu wanaoteka watoto wao.

Tukio hilo lilianza   mchana ambako polisi kikosi cha kutuliza ghasia walitumia mabomu ya machozi kuwatawanya waandamanaji hao katika mitaa ya kata za Chemchem na Mwinyi.

Mashuhuda wa tuko hilo walieleza kuwa   saa 4.00 asubuhi gari   ya Noah yenye rangi nyeusi isiyokuwa na namba za usajili ilifika eneo la shule hiyo na kuitwa wanafunzi wawili ambao hawajajulikana majina na kutokomea nao kusikojulikana, hali iliyoleta taharuki kubwa.

Baada ya kuzagaa kwa taarifa hizo mamia ya wananchi wakiwamo wazazi na walezi wa watoto wanaosoma katika shule hiyo walifurika shuleni hapo wakitaka kujua ukweli wa uvumi huo na watoto gani waliotekwa.

Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya wilaya ya Tabora mjini, Komanya Kitwala alisema hadi sasa hakuna taarifa zozote za utekwaji watoto katika manispaa hiyo, hivyo akawataka wananchi kuwa watulivu wakati suala hilo likishughulikiwa.

Kamanda wa   Polisi Mkoa wa Tabora, Emanuel Nley alikanusha kuwapo   vitendo vya utekaji watoto katika manispaa hiyo, huku akiwasihi wazazi na walezi wa wanafunzi wanaosoma katika shule hiyo kuwa watulivu wakati taarifa za kutekwa watoto wa shule hiyo lichunguzwa.

 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles