23.3 C
Dar es Salaam
Saturday, April 20, 2024

Contact us: [email protected]

RC Mgumba aipa tano DIT kwa kuzalisha wataalam

Mwandishi Wetu, Songwe

Mkuu wa Mkoa wa Songwe, Omary Mgumba ameipongeza Taasisi ya Teknolojia Dar es Salaam (DIT) kuzalisha vijana ambao watatumika katika maendeleo ya mkoa huo na taifa kwa ujumla.

Mgumba amewashauri pia wahitimu kujiunga katika vikundi vya kitaaluma kuanzisha kampuni za kikandarasi ili aweze kujiajiri wenyewe na pia iwe rahisi miradi ikitokea serikalini waweze kupata kazi.

Mgumba amesema hayo leo Alhamisi Februari 17, 2022 alipokuwa mgeni rasmi katika mahafali ya kwanza ya DIT Kampasi ya Myunga wilaya ya Momba Mkoani Songwe ambayo wanafunzi 70 wamehitimu.

“Wahitimu hawajakosea kuja hapa DIT kwasababu Taasisi hii imebeba dhana ya kutufikisha katika nchi zinazoendelea, kule wenzetu walipo……. Taasisi hii imesaidia sana kuleta maendeleo katika mkoa wetu kwa kutuzalishia wataalam,” amesema Mgumba.

Mgumba amesema nchi zilizoendelea zimebobea katika teknolojia kama nchi inahitajika kuwekeza katika teknolojia, na DIT sehemu muafaka kwa vijana kupata elimu hiyo kwani ina wataalam wa kutosha.

Mgumba amesema DIT ina wajibu mkubwa wa kuivusha nchi kufikia katika uchumi endelevu wa kidigitali.

Mkuu huyo wa Mkoa amepongeza bunifu mbalimbali alizoziona katika maonesho yaliyoandaliwa katika mahafali hayo ambayo yalikua na lengo la  kuonesha shughuli mbalimbali zinazofanywa na Taasisi pamoja idara zake.

Wakati huo huo, Mgumba amewashauri wananchi kukubali kutoa bure maeneo yao au kukubali kulipwa fidia ili watoe ardhi katika maeneo yao ili serikali iweze kuwekeza vyuo ambavyo ni kichocheo kikubwa cha maendeleo. 

Mkuu wa Mkoa wa Songwe, Omary Mgumba.

“Mkoa wa Songwe ni mkoa mpya ukilinganisha na mikoa mingine hivyo tuna kazi kubwa ya kufanya ili kupata maendeleo kama ilivyo katika mikoa mingine, tunahitaji wataalam mbalimbali na wadau wa maendeleo ili kuendana na kasi tuliyoikusudia” amesema Mgimba.

Mgumba ameongeza kuwa, “Wataalam hawa pia tutawatumia katika kushauri na kutekeleza mikakati mbalimbali ya maendeleo mkoani mwetu,” amesema.

Kwa upande wake Mkuu wa Taasisi hiyo, Prof Preksedis Ndomba amesema idadi ya wasichana bado ni ndogo, kati ya wahitimu  wasichana ni asilimia 31 pekee na kwamba Taasisi itaendelea kuweka mikakati mbalimbali ya kuongeza udahili wa wanafunzi wa kike. 

Wahitimu hao walidahiliwa na kuanza masomo katika mwaka wa masomo 2019/2020. 

“Mfumo huu umezalisha wahitimu waliobobea katika ufundi, ubunifu na ujasiriamali ambao wanaweza kujiajiri na kuajiriwa, wahitimu wa programu hizi ni mafundi stadi wanaohitajika sana kuhudumia sehemu mbalimbali zikiwemo mashuleni, mahospitalini,” amesema Prof. Ndomba.

Mkuu wa Wilaya ya Ileje, Anna Gidarya amesema ameishukuru DIT kuwaletea huduma ya elimu karibu, amesema “tumeona ni namna gani vijana wetu wamepata mafunzo badala ya kufanya kazi kwa mazoea bila kuwa na mafinzo yoyote.”

Mwenyekiti wa Baraza la DIT, Dkt. Mhandisi Richard Masika amewapongeza wahitimu hao ambao ni wa miaka miwili ya elimu ya Ufundi stadi katika fani ya Ufundi bomba pamoja na wahitimu wengine wa kozi fupi (uanagenzi) ya miezi nane katika fani za Ufundi bomba na Ufundi wa mifumo ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA).

Akitoa historia ya DIT – Kampasi ya Myunga amesema ilianza mwaka 2014 wakati Baraza la Taasisi hiyo lilipokabidhiwa na Serikali majengo na miundombinu ya iliyokuwa Kambi ya Ujenzi wa Barabara ya Tunduma – Sumbawanga, mwaka 2017 Baraza lilianzisha rasmi DIT-Kampasi ya Myunga.

“Moja ya malengo ya uanzishwaji wa Kampasi hii ni kutoa mafunzo ya Teknolojia ya Uchimbaji wa madini hasa kwa kuzingatia kuwa Mkoa wako Mhe Mkuu wa Mkoa wa Songwe una maeneo mengi yenye miamba,”

“Lakini pia wanafunzi wanaotoka Mkoa huu na Mikoa ya jirani, mfano Mbeya, Rukwa, Katavi, Njombe na Ruvuma wanaweza kutumia fursa hii kupata mafunzo kwa fani zinazopatikana katika Kampasi hii badala ya kusafiri kwenda Dar es Salaam ilipo Kampasi kuu ya DIT, na hivyo basi kupunguza gharama” amesema.

Wahitimu hao ni wa Ufundi Stadi katika fani ya Ufundi Bomba  (NVA Level II in Plumbing and Pipe Fitting watano, Mafunzo ya Wanagenzi katika fani ya Ufundi Bomba 32 na Mafunzo ya Wanagenzi katika fani ya Ufundi wa mifumo ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) 33.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles