26 C
Dar es Salaam
Friday, November 15, 2024

Contact us: [email protected]

RC Malima: Wapuuzeni watu wanaozusha kuhusu Sensa

Na Clara Matimo, Mwanza

Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Adam Malima, amewataka wananchi kupuuza uvumi unaoenezwa na baadhi ya wananchi kuhusu Sensa ya watu na makazi itakayofanyika Agosti 23, mwaka huu kwani watu hao hawana nia njema na wanataka kukwamisha zoezi hilo muhimu kwa maendeleo ya taifa.

Wakuu wa Wilaya zilizopo mkoani Mwanza pamoja na kamati za ulinzi na usalama za wilaya hizo wakiwa katika kikao cha daharura kilichoandaliwa na Mkuu wa Mkoa huo, Adam Malima kilicholenga kutathmini hali ya maandalizi ya sensa mkoani humo.

Malima ametoa wito huo juzi wakati akizungumza katika kikao cha dharura kilichojumuisha wakuu wa wilaya zote saba zilizopo mkoani humo na kamati za ulinzi na usalama za wilaya hizo kwa ajili ya kutathmini hali ya maandalizi ya sensa Mkoani Mwanza.

Alisema mtu yeyoye anayetoa taarifa za kupotosha umuhimu wa zoezi la sensa ni adui wa maendeleo ndani ya mkoa wa Mwanza pamoja na malengo mazuri ya Rais Samia Suluhu Hassan kwa ustawi wa maendeleo ya wananchi wake.

“Maandalizi ya zoezi la sensa  ndani ya mkoa wetu yanakwenda vizuri. Lakini yapo mambo madogo madogo ambayo ni changamoto tulizozibaini ndiyo maana tumekutana ili kuzitatua nia yetu ni kuhakikisha zoezi la sensa linafanikiwe kwa asilimia 100 maana kuna watu wanaingiza ajenda zao za binafsi kwenye jambo la sensa.

“Wapo wanaosema mimi kwenye kata yangu nilikuwa natarajia ingejengwa shule,  kituo cha afya, niliahidiwa barabara ya TARURA ingepita hapa lakini haikupita. Anayesikia kauli hizo naye anaenda kwa wananchi anasema kwa kuwa barabara haikupita, kwa kuwa hatukujengewa kituo cha afya tusishiriki kwenye sensa.  Kwa kweli hatumung’unyi maneno, ukimuona mtu anahusika na kupotosha umuhimu wa sensa ndani ya mkoa wetu huyo ni adui wa maendeleo yetu,”alisema Malima na kuongeza:

“Sensa ndiyo msingi wa maendeleo kwa hiyo huyu anayewaongopea wananchi wenzake kwamba msishiriki kwenye sensa basi huyo ni adui kuliko maadui wote tunaowafahamu. Tunataka  tujue tuna watu wangapi kwa kila kata, wilaya  ili iwe rahisi kupanga mipango ya maendeleo kama huna takwimu sahihi za watu unaotaka kuwahudumia utakuwa unawahudumia kwa kubahatisha,”alisema Malima.

Malima amesisitiza kuwa sensa ni muhimu maana huisaidia serikali kupata taarifa za msingi zitakazosaidia mchakato wa utekelezaji wa dira ya maendeleo, mageuzi ya masuala ya afya na jamii pamoja na ufuatiliaji wa ajenda za maendeleo za kimataifa.

Kwa upande wao wakuu wa wilaya hizo akiwemo, Hassa Masalla wa Ilemela, Jiharo Samizi wa Kwimba, Amina Makilagi wa Nyamagana na Senyi Ngaga wa Sengerema waliahidi kuendelea kutoa elimu ya umuhimu wa sensa ya watu na makazi kwa wananchi wa kata zote zilizopo  katika wilaya zao ili kila mtu atambue umuhimu wa sensa ashiriki kikamilifu kufanikisha zoezi hilo.

Mkuu wa Wilaya  ya Sengerema Senyi Ngaga alisema: “Usipokuwa na idadi kamili ya watu ambao unawaandalia chakula unaweza ukapika chakula kingi kikabaki na hivyo ikawa ni uharibufu wa chakula. Pia, unaweza ukapika kidogo kisiwashibishe watu uliolenga kuwalisha hivyo jamii inatakiwa kutambua kwamba sensa ni muhimu kwa maendeleo yetu wananchi wote wa nchi yetu,” alisema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles