Na Clara Matimo, Mwanza
Jumla ya Makatibu Tawala Wasaidizi Mipango na Uratibu 26 kutoka mikoa 25 nchini wamekutana jijini Mwanza kwa ajili ya kupewa mafunzo ambayo yatawasaidia kuwakumbusha namna ya kuandika na kusimami miradi ya maendeleo inayotekelezwa na serikali katika maeneo mbalimbali nchini.
Akizungumza wakati akifungua mafunzo hayo Novemba 8, 2022, Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Adam Malima, aliwataka washiriki kutimiza wajibu wao kwa kufuata maadili ya kazi zao bila woga kwani wao ni roho ya maendeleo ya mkoa na taifa kwa ujumla.
“Hampaswi kuwa wanyonge mnapotimiza majukumu yenu maana taifa na serikali imewaamini mkitimiza majukumu yenu vizuri taifa litasonga mbele kwa kutumia nafasi zenu maana suala la uandishi wa miradi ni muhimu sana pia washaurini vizuri viongozi wenu wakiwemo wakuu wa mikoa na makatibu tawala bila kuwa na woga.
“Waambieni ukweli hata kama unauma kuliko kuwaambia uwongo ambao unawafurahisha lakini matokeo yake ni mabaya kwa taifa hakikisheni hamrudii makosa mliokuwa mkiyafanya kabla ya kupata mafunzo haya,”alisisitiza Malima.
Malima aliwataka kuisimamia vizuri miradi yote ambayo serikali inaitekeleza katika maeneo mbalimbali nchini ili ikamilikie kwa wakati na ikiwa na ubora uliokusudiwa.
“Nami ni mchumi kama nyie hakuna nisichofahamu epukeni kutanguliza tamaa na kuhujumu miradi mnayoisimamia vilevile kila siku kabla ya kutoka eneo la kazi mjitathmini kama mmetendea haki nafasi zenu,“alisema Malima.
Aidha Malima aliwashauri kutotumia mbinu za kizamani kwa ajili ya kufanya ufuatiliaji na tathmini badala yake wabuni mbinu mbadala itakayorahisisha utekelezaji wa majukumu yao ili yawe yenye tija zaidi.
Awali akimkaribisha Mgeni Rasmi Malima kufungua mafunzo hayo, Mkurugenzi Msaidizi Idara ya Tawala za Mikoa kutoka TAMISEMI, Johnson Nyingi, alisema mafunzo hayo yametokana na uwepo wa changamoto ya namna ya kuandaa miradi kwa washirki hao.
“Baada ya kubaini changamoto hii TAMISEMI kwa kushirikiana na Chuo Kikuu Cha Mzumbe tuliamua kuandaa mafunzo haya ya siku sita yaliyoanza Novemba 7, 2022 hadi Novemba 12, 2022 maana miradi mingi ambayo wanaiandaa imekuwa haikidhi changamoto zilizopo ama inakuwa na gharama kubwa ama inachelewa kukamilika,”alieleza Nyingi.
Akizungumza kwa niaba ya washiriki wenzake wa mafunzo hayo, Katibu Tawala Msaidizi Mipango na Uratibu kutoka Mkoa wa Morogoro, Anza Naossa alimhakikishia Malima kwamba watatekeleza majukumu yao kwa kuzingatia sheria, kanuni na miongozo ya utumishi wa umma ili kuhakikisha miradi inayotekelezwa na serikali inakuwa na tija kwa jamii na taifa.