25.2 C
Dar es Salaam
Friday, April 19, 2024

Contact us: [email protected]

RC Malima awaagiza wataalamu kutoa elimu kwa wakulima

Na Clara Matimo, Mwanza

Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Adam Malima, amewaagiza wataalamu wa kilimo pamoja na wakuu wa wilaya zote saba zilizopo mkoani humo  kuwahamasisha wananchi  hasa wakulima kujifunza  kanuni bora za kilimo kwa mazao ya chakula na biashara ili kuongeza tija ya uzalishaji.

Malima alitoa agizo hilo Agosti 4, 2022 wakati akifungua maonesho ya Kilimo na Sherehe za wakulima maarufu kama Nane nane Kanda ya Ziwa Magharibi inayojumuisha Mikoa ya Mwanza, Geita na Kagera ambayo kila mwaka  hufanyika  katika viwanja vya Nyamhongolo vilivyopo Manispaa ya Ilemela Mkoani Mwanza.

Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Adam Malima akitembea kuelekea kukagua vibanda vya wadau walioshiriki kuonesha shughuli wanazofanya zinazohusiana na sekta za kilimo, mifugo ma uvuvi( vibanda hivyo havipo pichani).

Alisema wakulima wakilima kwa kufuata kanuni za kilimo bora umaskini utaondoka hapa nchini lakini wakilima kwa kubahatisha taifa litabaki na umaskini kwani chakula ni kitu ambacho hakiwezi kukosa soko duniani maana hakina mbadala wake.

Alisema uwekezaji katika sekta ya kilimo utasaidia sana kuimarisha usalama wa chakula, pato la taifa na kupunguza umaskini  katika Kanda ya Ziwa Magharibi pamoja na taifa kwa ujumla kwani sekta za Kilimo, Uvuvi na Ufugaji ndizo zinazoajiri nguvu kazi kubwa hapa nchini kuliko zingine.

 “Kati ya asilimia 63 hadi 65 ya nguvu kazi  hapa nchini imeajiriwa na hutegemea kupata riziki katika sekta ya kilimo, lengo la serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan ni kuhakikisha nchi inaendelea kukua kiuchumi kufikia maendeleo ya viwanda ambapo malighafi za viwanda hivyo vitokane na sekta ya kilimo yaani kilimo, mifugo na uvuvi ndiyo maana rais wetu anashirikiana na wadau mbalimbali wa maendeleo,” alisema Malima.

Aliwahamasisha wananchi na wakulima wa mikoa ya Kanda ya Ziwa Magharibi kutumia fursa  katika sekta ya kilimo zinazopatikana ndani na nje ya kanda hiyo ikiwemo uwepo wa ziwa viktoria kwa kulima kilimo cha umwagiliaji lengo ni kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi hasa ukame na ufugaji wa samaki kwa njia ya vizimba ili kuchangia ukuaji wa sekta ya kilimo na uvuvi.

“Mkoa wa Mwanza umedhamiria kutekeleza Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa miaka mitano 2021 hadi 2026 kwa kuanzisha ufugaji wa samaki kwa njia ya vizimba ndani ya ziwa viktoria serikali kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi imegharamia mafunzo ya awali,  hadi sasa vijana 640 ambao wameunda vikundi 64 vimesajiliwa na vijana hao  wamejengewa uwezo katika ufugaji wa samaki kwa njia ya vizimba.

“Kanda ya Ziwa Magharibi ni kituo katika nchi za maziwa makuu, Afrika Mashariki, mikoa na kanda za jirani hivyo wakulima na wananchi katika kanda hii wanaweza kulitumia soko hili katika mikoa na kanda za jirani, nchi za maziwa makuu na Jumuiya ya Afrika Mashariki kwa kuuza mazao ya sekta ya kilimo katika nchi za Uganda, Rwanda, Kenya na Burundi,” alisema Malima.

Aidha aliwataka wakulima na wananchi kutumia fursa ya uwepo wa taasisi za fedha ikiwa ni pamoja na benki zaidi ya 24 zinazofanya kazi katika kanda hiyo ili kupata mitaji ya kuwekeza kwenye sekta ya kilimo kwani Mkoa wa Mwanza una eneo linalofaa kwa kilimo cha umwagiliaji linalokadiriwa kufikia hekta 36,000 kati ya eneo hilo takribani  hekta 1,635 tu sawa na asilimia 4.5 ndilo linalotumika kwa kilimo cha umwagiliaji.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi ya Maonesho ya Kilimo na Sherehe za Wakulima Nane Nane 2022 Kanda ya Ziwa Magharibi, Emily Kasagala, alisema  kauli mbiu ya maonesho ya mwaka huu inasema ‘Ajenda 10/30: Kilimo ni biashara, shiriki kuhesabiwa kwa mipango bora ya kilimo, mifugo na uvuvi’ inakumbusha kulima kibiashara kwa kufuata kanuni za kilimo bora kwa mazao ya kilimo, ufugaji na uvuvi.

“Tunataka kuachana na kilimo cha mazoea ambacho huwakatisha tamaa wakulima kwa kuwa hawapati faida stahiki, kauli mbiu hii inajulisha wananchi kwamba serikali inalenga kuona kuwa sekta ya kilimo inakuwa kwa asilimia 10 kufikia mwaka 2030,” alifafanua Kasagala.

Kasagala alisema Kanda ya Ziwa Maharibi iliundwa mwaka 2017 ambapo tangu mwaka 2018 maonesho hayo yamekuwa yakiadhimishwa katika viwanja vya Nyamhongolo  kuanzia Agosti Mosi hadi Agosti 8, kila mwaka na washiriki huonesha shughuli mbalimbali zinazohusiana na sekta za kilimo, mifugo na uvuvi, wakulima na wananchi hupata fursa ya kuona na kujifunza juu ya bidhaa na huduma zinazotolewa na washiriki ili wazitumie waweze kuzalisha kwa tija na ubora zaidi.

Kwa mujibu wa Kasagala maonesho hayo yamekuwa yakikumbwa na changamoto mbalimbali hususan ukosefu wa miundombinu ya kudumu hali hiyo huongeza gharama za uratibu hasa wakati wa ujenzi au ukarabati wa miundomhinu mara kwa mara.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles