23.7 C
Dar es Salaam
Thursday, September 28, 2023

Contact us: [email protected]

RC Malima anusa ubadhirifu ujenzi Hospitali ya Halmashauri Handeni

Na Mwandishi Wetu, Tanga

Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Adam Malima amesema hajaridhishwa na kasi ya ujenzi wa Hospitali ya Halmashauri ya Wilaya ya Handeni na kubainisha kuwa kuna mazingira ya ubadhirifu.

Akizungumza wakati akikagua maendeleo ya mradi huo uliokuwa ukamilike Januari mwaka huu, Malima amesema mradi huo unaojengwa na serikali kwa kushirikiana na Taasisi ya Islamic Help,
una taswira ya ubadhirifu na rushwa ambapo ametoa wiki mbili kwa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) Mkoa wa Tanga kuchunguza.

“Hapa pana jambo, sielewi nini kimetokea kuhusu hili jengo mbona hammalizi, tulikubaliana mmalize Januari tukarudi tukakuta hawajafanya kitu wala hawana mpango eneo la mradi hawajaja, hawana maelezo ya kutosha.

“Sasa ikibidi tuendeshane kama tulivyofanya kwenye miradi ya Uviko-19 tukamatane sawa, watu wangu wa Kamati ya Ulinzi na Usalama wapo haina shida tutaweka kambi hapa, lakini tabu ya kuweka kambi ni kwamba tutaumizana,” amesema RC Malima.

Malima amesema katika hilo hatanii na atakuwa akipita kila baada ya siku tatu kuangalia maendeleo ya mradi huo ambao hadi sasa kiasi cha Sh bilioni 5.1 zimetolewa ambapo serikali imetoa Sh bilioni 2.1 huku Islamic Help wakitoa Sh bilioni tatu.

“Sifurahishwi na kasi yenu, ni ndogo sana, kuelekea chumba cha kuhifadhia maiti hakuna barabara… hapa pana tuhuma za ubadhirifu, Islamic Help na kamati yangu nawapa wiki moja tengenezeni hili jambo hatuwezi tukawa tunafanya masihara…” amesema.

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Handeni, Sirieli Mchembe amesema wamepokea maelekezo kutoka kwa Mkuu wa Mkoa na kuongeza kuwa awali changamoto kubwa kwenye jengo la wagonjwa wa dharura ilikuwa ni ramani lakini Tamisemi imeshamaliza hilo na kuahidi kuwa ndani ya miezi miwili hospitali hiyo itakuwa imekamilika.

Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi wa Wilaya ya Halmashauri ya Wilaya ya Handeni, Sekiara Kiariri alisema katika ujenzi huo, serikali imeingia mkataba na Taasisi ya Islamic Help kwa ajili ya ujenzi wa majengo sita ikiwamo kumalizia jengo la wagonjwa wa nje (OPD), wodi ya wajawawazito, jengo la mionzi, jengo la kufulia, mochwari na kichomea taka.

“Mkataba wa makubaliano kati ya halmashauri na Islamic Help ulisainiwa Aprili 30, mwaka jana na kazi ilitarajiwa kuanza Mei 30 lakini kutokana na fedha kutofika kwa wakati kutoka kwa mfadhili mkuu kazi ilianza Agosti 15, mwaka jana.

“Pamoja na hayo pia kuna changamoto mbalimbali ikiwamo kuchelewa kupatikana kwa mchoro wa ujenzi wa jengo la jengo la dharura kutoka wizarani na mvua zinazoendelea kunyesha zimesababisha kazi ya ujenzi kutokamilika kwa wakati,” amesema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,745FollowersFollow
574,000SubscribersSubscribe

Latest Articles