*Atoa Sh milioni 20 kwa ajili ya kuziwezesha zifike ligi kuu Tanzania Bara
Na Clara Matimo, Mwanza
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Adam Malima ameahidi kuzisaidia timu za Mwanza zinazoshiriki ligi ya championiship kifedha na ushauri ili ziweze kushiriki ligi kuu Tanzania baramsimu wa 2023/24.
Malima ametoa ahadi hiyo Oktoba 25, 2022 alipokuwa akizungumza na wadau wa soka mkoani humo wamiwemo viongozi wa timu za Gwambina FC, Copco Veteran FC na Pamba FC zinazoshiriki ligi ya championship ambapo aliahidi kutoa kiasi cha Shmilioni 20 ikiwa ni mwanzo wa kuweka mikakati ya ushindi kwa timu hizo.
Amesema malengo na ndoto yake ni kupata timu kutoka mkoani humo itakayocheza ligi kuu mwaka kesho lakini mpira hauchezwi bila pesa ambapo aliwapa wiki moja viongozi wa timu hizo wakahamasishane kwenye michango maana ili kufanikiwa wanahitaji kuwa na dhamira ya dhati kwenye soka na kujitoa kwa hali na mali pia aliwaasa kutodharau fedha yoyote itakayotolewa na wanachama hata kama ni Sh 5,000.
“Kila mara nasema Mwanza bila kuwa na timu inayoshiriki ligi kuu hatuheshimiani hapa mjini, kitendo cha watu kutoka mkoani Kagera au Geita ili kutupa starehe sisi ya kuona mpira hapa ni jambo la fedheha sana mimi fedha hizo ni mwanzo tu yawezekana tukikutana wiki ijayo nikawa nimepata zaidi maana naendelea kuwachangisha marafiki zangu wengine lakini bila kuwa na dhamira ya dhati hatuwezi kusonga.
“Jambo ninaloendelea kuhimiza mimi pesa yangu ninayotafuta kwa wadau wangu mbalimbali pamoja na mimi mwenyewe nataka nikiitoa nione matokeo chanya maana mimi ni mchumi hivyo lazima tuwe na nia ya dhati ya kuhakikisha tunapata timu ambayo itacheza ligi kuu mwaka kesho hata kama tukipata timu zaidi ya moja ni sawa tena ni vizuri zaidi alisema na kuongeza.
“Tutaunda uongozi wa mkoa ambao utashirikiana na uongozi wa timu tutawapangia majukumu pamoja na wajibu wao lengo letu ni mafanikio lakini kwa kuwa tuna timu tatu pesa hizo nitazipeleka zaidi kwenye timu ambayo inaibua vipaji vya ndani tuviendeleze ili wachezaji wakacheze Taifa Stars,”amesema Malima.
Aliwataka wadau hao kuweka msingi imara wa soka ili wachezaji waweze kucheza mpira mzuri pia kuendesha club kwa uwazi maana mambo hayo yanasaidia kuleta mafanikio na matokeo chanya kwenye soka.
“Hakuna sehemu yenye majungu kama mpira tunaupenda lakini ni pasua kichwa hivyo uwazi ni jambo la msingi, mafanikio kwenye mpira hayaji kwa kutamani bali ni kujipanga kama nilivyosema awali mpira hauchezwi bila pesa ukicheza bila pesa siku zote utaona mazingaombwe uwanjani maana mchezaji ambaye anamudu mchezo kila siku atakuwa na changamoto mara atasema mguu unamuuma,”alifafanua Malima.
Katibu Mkuu wa Chama Cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Mwanza(MZFA), Leonard Malongo, alisema watashirikiana bega kwa bega na Mkuu huyo wa mkoa ili kuhakikisha mkoa ho unapata timu zitakazoshiriki ligi kuu mwaka kesho.