28.2 C
Dar es Salaam
Saturday, April 20, 2024

Contact us: [email protected]

RC Lindi aiomba kampeni wanaume kupima afya kuendelea

Na Mwandishi Wetu, Lindi

Mkurugenzi Mtendaji wa Tume ya Kudhibiti UKIMWI Tanzania (TACAIDS), Dk. Leonard Maboko, amefanya ziara ya kikazi katika Mkoa wa Lindi kwa lengo la kufanya ufatiliaji na tathimini ya afua za VVU na Ukimwi zinazotekelezwa katika mkoa huo.

Akiwa mkoani humo, Dk. Maboko alikutana na Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Zainab Telack ambaye amemweleza changamoto zilizopo mkoani hapo zinazochangia ongezeko la maambukizi ya VVU.

Katika maelezo yake, Zainab amebainisha kuwa changamoto hizo ni pamoja na uwepo wa maeneo hatarishi yanayosababishwa na shughuli za kiuchumi, mila na destri zinazofanyika katika mkoa huo.

Zainab ameiomba TACAIDS kuendeleza kampeni ya wanaume kupima afya zao, kwa kuwa suala la upimaji bado ni changamoto kwa wanaume waliowengi na kuendeleza maambukizi kwa wenza wao kwa kuwa hawajui hali zao za maambukizi ya VVU.

Amesema kuwa uwezekano wa maambukizi kuongezeka Lindi ni mkubwa kutokana  na uwepo wa wageni hasa katika maeneo ya vijijini ambapo pia elimu ya VVU na Ukimwi haijafika na ngono zinafanyika kwa wingi.

Ameshauri wadau wanaotekeleza afua za VVU na Ukimwi katika Mkoa wa Lindi wasimamiwe na kuratibiwa vizuri ili wafike hadi kwenye maeneo hatarishi ambayo yanaweza kuleta ongezeko la maambukizi mapya ya VVU.

“Tukiacha hali hii iendelee katika mkoa wetu tatizo litakuwa kubwa kwa kuwa wanaume wanaofanya ngono na wanawake hao bado watakuwa na wanawake wengine, kwa kufanya hivyo, maambukizi yatazidi kuwa makubwa”.amesisitiza mhe Zainab.

Aidha Dk. Maboko ameagiza waratibu wa Ukimwi wa mkoa huo kuhakikisha wanafanyia kazi hizo changamoto zilizoainishwa ili kuhakikisha wanapunguza maambukizi mapya, ili ifikapo mwaka 2030 tuwe tumefikia lengo la kidunia la kuwa na maambukizi mapya sifuri, unyanyapaa sifuri na vifo vitokanavyo na Ukimwi sifuri.

Ziara hiyo iliendelea katika Halimashauri ya Ruangwa, amekutana  na Kaimu Mkurugenzi Mtendaji, Rashid Namkulala na watendaji wengine ambapo alitaka kujua hali ya upatikanaji na usambazwaji wa kondomu katika halimashauri hiyo.

Dk. Maboko ameelezwa kuwa tayari kasha 308 zimepokelewa na kusambazwa katika maeneo ya vipaumbele, tayari kote kuna kondomu na wananchi wanaendelea kupata huduma hiyo ya kinga ya maambukizi mapya ya VVU.

Dk. Maboko amesisitiza kuwe na usimamizi mzuri na ushirikiano kati ya waratibu wa Ukimwi na wasimamizi wa maeneo husika ambapo makasha hayo yamefungwa ili kuhakikisha yanakuwa na kondomu wakati wote.

“Pamoja na njia nyingine zinazotumika katika kujikinga na maambukizi ya VVU kondomu ni rahisi sana na inakukinga na madhara mengine yanayotokana na ngono zisizo salama, mimi nashauri wananchi watumie kondomu kwa ufasaha ili kujikinga na maambukizi ya VVU pamoja na mimba zisizotarajiwa na magonjwa mengine ya ngono.

“Ni muhimu sana vikao vya kamati za Ukimwi ngazi ya halmashauri na vijiji/mtaa vikafanyika kwa wakati kwani ni njia moja wapo tunayoitegemea katika kutatua changamoto za VVU na Ukimwi zilizopo katika ngazi za chini”, amesema Dk. Maboko.

Naye Mratibu wa Ukimwi wa Ruangwa, Mariam Kimaro, amesema kuwa  harmashauri hiyo inachangamoto ya mwingiliano wa watu kutokana na machimbo ya madini, minada, kilimo cha ufuta na miradi ya maenedeleo inayoendelea.

Mariam ameeleza kuwa kutokana na maeneo hatarishi , elimu inaendelea kutolewa kwa wananchi japokuwa watendaji wanachangamoto ya rasilimali fedha kwa ajili ya uwezeshaji wa shughuli mbalimbali za VVU na Ukimwi wilayani hapo.

Aidha Dk. Maboko amewakumbusha watendaji malengo yaliyopo kwa nchi ni kuwa ifikapi 2030 Tanzania isiwe na maambukizi mpya ya VVU, vifo vitokananvyo na Ukimwi wala unyanyapaa na ubaguzi, kupitia ushirikiano wa kila mmoja wanaweza kufikia malengo hayo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles