24.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, September 11, 2024

Contact us: [email protected]

RC Kunenge azindua Oparesheni ya kudhibiti wahamiaji haramu

Na Gustaphu Haule,Pwani

MKUU wa Mkoa wa Pwani, Abubakar Kunenge, amezindua oparesheni maalum ya kudhibiti Wahamiaji haramu ndani ya mkoani humo huku akiwapiga marufuku maofisa wahamiaji watakaoendesha oparesheni hiyo kuacha tabia ya kujihusisha na vitendo vya rushwa.

Aidha, Kunenge amesema kuwa afisa ambaye atabainika kuchukua rushwa kutoka kwa wahamiaji hao au sehemu yoyote inayohusiana na kuwalinda wahamiaji hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi yake.

Kunenge ametoa kauli hiyo leo Machi 14, Mjini Kibaha wakati akizindua oparesheni hiyo kwa maofisa wa Uhamiaji wa Mkoa wa Pwani huku ukishuhudiwa na kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa.

Amesema kuwa, lengo la oparesheni hiyo ni kuhakikisha inadhibiti mianya ya wahamiaji wanaoingia katika utaratibu usio rasmi na kwamba zoezi hilo litafanyika katika Wilaya 7 na Halmashauri Tisa za Mkoa wa Pwani.

Kunenge amesema wengi wa wahamiaji hao wamekuwa wakijihusisha katika matendo ya uhalifu na hivyo kuhatarisha usalama wa wananchi wa maeneo husika na kwamba kufanyika kwa operesheni hiyo itasaidia kupunguza vitendo hivyo.

Amesema kutokana na umuhimu wa zoezi hilo lazima maofisa wa Uhamiaji wafanyekazi zao kwa uadilifu na uaminifu mkubwa na kwamba isiwe sehemu ya kuchukua rushwa na kama wanaona wamepewa sehemu ya kuchukua rushwa Serikali haitawaacha salama.

“Natoa pongezi kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mama Samia Suluhu Hassan na Kamishna Jenerali wa Uhamiaji Anna Makakala kwa kuanzisha oparesheni hii maaana umuhimu wake ni mkubwa hasa katika kuleta usalama wa mipaka yetu na wananchi wetu,”amesema Kunenge.

Kunenge,amewaomba wamiliki wa viwanda kutoa ushirikiano kwa maofisa Uhamiaji watakaokuwa wanapita katika maeneo yao ilikusudi waweze kufanyakazi yao vizuri sambamba na kuwasaidia wahamiaji waliopo katika Viwanda hivyo kufanyakazi zao vizuri.

“Mimi mwenyewe nitakuwa mstari wa mbele kuongoza oparesheni hii siku zote lakini niwaombe Wakuu wa Mikoa wenzangu watoe ushirikiano wa kubaini Wahamiaji haramu maana haiwezekani wahamiaji wapite Mikoa mingine halafu wakamatiwe Pwani,”ameongeza Kunenge.

Kwa upande wake Ofisa Uhamiaji wa Mkoa wa Pwani, (ACI) Omary Hassan,amesema kuwa oparesheni hiyo ya Siku 10 itaanza leo Machi 14 na kumalizika Machi 23  mwaka huu.

Hassan amesema kuwa Mkoa wa Pwani kuna wageni wengi ambao wanatoka nchi mbalimbali na kufuatia hali hiyo wapo wahamiaji haramu ambao wamekuwa wakiingia na hatimaye kufanya vitendo vya uhalifu.

“Kuna athari kubwa za wahamiaji haramu kwakuwa miongoni mwao hufanya vitendo vya uhalifu na ndio maana Serikali imeona ifanye oparesheni hiyo kwa ajili ya kudhibiti Wahamiaji haramu lakini pia kudhibiti vitendo vinavyofanywa na Wahamiaji waliopo nchini,”amesema Hassan.

Hassan,amesema kuwa maofisa wa Uhamiaji Mkoa wa Pwani wamejipanga vizuri kuhakikisha zoezi hilo linafanyika kwa kufuata sheria na taratibu zilizowekwa na anaimani ndani ya muda huo watafikia malengo.

Hata hivyo, Hassan ametoa wito kwa wakazi wa Mkoa wa Pwani kuhakikisha wanasaidia kuwaibua wahamiaji haramu waliopo katika maeneo yao ili vyombo dola vichukue hatua ya kuwakamata kwa haraka.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles