Na MWANDISHI WETU-DAR ES SALAAM
MKUU wa Mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo anadaiwa kumfukuza katika kikao cha kujadili hoja za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Mkuu wa Wilaya ya Arumeru, Alexander Mnyeti.
Mnyeti anadaiwa kufukuzwa baada ya kuchelewa kwenye kikao hicho kilichofanyika Arusha hivi karibuni kikilenga kila halmashauri kufika kwenye Kamati ya Ulinzi na Usalama kutetea hoja zake.
Chanzo cha kuaminika kilieleza kuwa wakati kikao hicho kikiendelea, Mnyeti aliwasili akiwa amechelewa ndipo Gambo alipodaiwa kumuondoa akaendelee na mambo mengine.
Licha ya taarifa hizo kuandikwa katika mitandao ya jamii juzi, MTANZANIA lilifanya juhudi za kumtafuta Mkuu wa Mkoa, Mrisho Gambo kupata ufafanuzi hatua ya kumfukuza mkuu huyo wa wilaya kikaoni.
Pamoja na kupigiwa simu zake za mkononi zilikuwa hazipokelewi na hata alipotumiwa ujumbe mfupi wa simu bado haukujibiwa.
Mnyeti mwenyewe alikiri kuondoka kwenye kikao hicho kutokana na sababu za msingi alizokwisha kuziwasilisha kwa bosi wake (Gambo) kupitia ujumbe mfupi wa simu.
“Ni kweli nilichelewa kufika kwenye kikao hicho kutokana na majukumu ya kufanya kazi za operesheni mpaka saa 9 usiku ya jana yake.
“Nilimtumia taarifa kwa njia ya simu, nadhani ujumbe utakuwa ulichelewa kumfikia na nilipofika alinitaka nirudi kuendelea na mambo mengine. Tafsiri hiyo ilichukuliwa kama nimefukuzwa,” alidai Mnyeti.
Akizungumza kwenye kikao hicho, Gambo aliwataka watumishi hao kujipanga na kuendana na kasi ya Serikali ya Awamu ya Tano iliyojipambanua kuwatumikia wananchi hususan wanyonge.