24.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, April 23, 2024

Contact us: [email protected]

Rc Gabriel aagiza kuundwa timu maalum kufuatilia mapato Jiji la Mwanza 

*Asema Jiji limeshindwa kufikia lengo la ukusanyaji

Na Clara Matimo, Mwanza

Kufuatia Halmashauri ya Jiji la Mwanza kutofikia malengo ya ukusanyaji mapato, Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Mhandisi Robert Gabriel, ameagiza kuundwa timu maalum itakayofuatilia jambo hilo ili kubaini tatizo lililopo.

Mhandisi Gabriel ametoa agizo hilo leo Jumanne, Juni 21, 2022 katika mkutano maalum wa Baraza la Madiwani uliolenga kujadili utekelezaji wa hoja za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kwa Mwaka wa Fedha 2020/2021.

Baadhi ya madiwani wa Halmashauri ya Jiji la Mwanza wakiwa katika kikao maalum cha kujadili utekelezaji wa hoja za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kwa Mwaka wa Fedha 2020/2021.

Amesema kwa mujibu wa ripoti ya CAG, Jiji hilo limeshindwa kufikia lengo la ukusanyaji mapato ambapo ametolea mfano sekta ya hoteli na kusema imekusanya asilimia 23 kati ya 100 zinazotakiwa, hivyo asilimia 77 haikukusanywa.

“Timu hiyo itatusaidia kufahamu ni nini kinasababisha CAG kutoa hoja hiyo mara mbili kwa miaka tofauti kwa nini tunaacha malimbikizo ya ukusanyaji mapato, tuwe makini, mimi ofisini siangalii muda wa kutoka, naangalia kazi iishe huwezi kuwa na viporo vya uwajibikaji huo ni uzembe Mkurugenzi wa jiji, Sekiete Yahya, kwenye taarifa yake ya majibu ya utekelezaji wa hoja za CAG amesema asilimia 62 ya hoja hazijakamilika zilizokamilika ni asilimia 38 inabidi watendaji tujitafakari,” amesema Mhandisi Gabriel.

Kwa upande wao baadhi ya madiwani wa halmashauri ya jiji hilo akiwemo, Joseph Kabadi, Hamidu Said na Bhiku Kotecha kutoka CCM wameomba waombaji wa tenda za kukusanya ushuru wapitishwe kwenye kata wawajadili ili watakapopewa tenda waweze kuwasimamia kikamilifu pia washirikishwe katika timu itakayoundwa ili wawaonyeshe  watendaji vyanzo vya mapato vilipo kwani wao ndiyo wanaoishi kwenye jamii hivyo wanavielewa vizuri.

“Mimi nimezaliwa hapa Mwanza wilaya hii ya Nyamagana, nimekulia hapa, nimesoma hapa kwa hiyo naelewa vizuri vyanzo vyote vya mapato vilipo, mkuu wa mkoa nakuomba mimi na madiwani wenzangu waliotangulia kuchangia kama walivyosema timu utakayoiunda na sisi tuhusishwe naamini mapato ya halmashauri yetu yataongezeka,” amesema Kotecha.

“Kwa mfano Mawakala wa usafi na kukusanya ushuru, unakuta uchafu umerundikana kwa sababu wakati wa mchakato wa kumpata mzabuni madiwani wala kamati ya maendeleo ya kata hazihusishwi, mnakutana na wakala kwanza hakutambui kama diwani lakini uchafu unaoonekana kwenye kata wa kwanza kulaumiwa ni diwani na kamati yake ya maendeleo ya kata,” amesema Kabadi.

Nae Mkaguzi Mkuu wa Nje wa Hesabu za Serikali Mkoa wa Mwanza, Athuman Mustapha, amesema:

“Kitu kikubwa ambacho naweza kuishauri halmashauri yetu wamekuwa wazuri sana kwenye kujibu hoja lakini inatakiwa wawe wazuri sana kwenye kuzuia hoja, nilitarajjia hoja hizi zilizopo hapa  tuzikute huko vijijini ambako kuna wataalamu wachache wajitahidi kufanya kazi kwa mujibu wa kanuni ,sheria na taratibu zilizopo,” amesema.

Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana, Amina Makilagi, aliahidi kwamba atasimamia maagizo hayo ili kuhakikisha asilimia 62 ya hoja zilizotolewa na CAG ambazo hazijakamilika zinafungwa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles