23.6 C
Dar es Salaam
Tuesday, September 10, 2024

Contact us: [email protected]

RC Chalamila aipongeza TPDC kuwajengea uwezo Viongozi wa Dini na Madiwani kuhusu ulinzi wa miundombinu ya gesi

Na Esther Mnyika, Mtanzania Digital

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila, amepongeza Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) kwa kutoa elimu na kuwajengea uwezo viongozi wa dini na madiwani ili kuwa mabalozi wazuri kwa wananchi kuhusu utunzaji wa miundombinu ya shirika hilo.

Akizungumza leo Agosti 15, 2024, jijini Dar es Salaam wakati akifunga semina iliyohusisha wadau mbalimbali, Chalamila amesema TPDC imeandaa semina hiyo kwa lengo la kuwajengea uwezo na kuwaelimisha wadau hao juu ya ulinzi wa miundombinu ya usafirishaji wa gesi, mafuta na masuala mengine muhimu.

“Semina ya leo imewaleta pamoja viongozi wa dini na madiwani wa mkoa wa Dar es Salaam kutoka Wilaya za Ubungo, Kinondoni, Temeke, Ilala na maeneo mengine. Hawa ni watu muhimu katika kuhakikisha kwamba ujumbe wa kutunza miundombinu ya TPDC unafika kwa wananchi,” alisema Chalamila.

Ameongeza kuwa lengo kuu la semina hiyo ni kuwafanya viongozi hawa kuwa mabalozi wa kutunza miundombinu ya TPDC ambayo ni muhimu kwa kusafirisha gesi kwa Watanzania na watumiaji wengine.

Chalamila pia amesisitiza umuhimu wa viongozi wa dini kutumia nyumba za ibada kama misikiti na makanisa kupeleka ujumbe kwa jamii kuhusu umuhimu wa kutunza miundombinu hiyo.

Alisema TPDC imekuwa ikiendesha semina kama hizo mara kwa mara ili kuongeza uelewa katika maeneo ambako miundombinu ya shirika hilo imepita, na inaweza kuwa hatarini kuharibiwa na watu wenye uelewa mdogo.

Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa TPDC, Francis Mwakapalila, alisema semina hiyo ililenga kuwapa fursa ya kujifunza na kuelewa zaidi kuhusu gesi asilia na kuwakumbusha majukumu ya shirika hilo. Alieleza kuwa jukumu la msingi la TPDC ni kufanya tafiti, uendelezaji, na usafirishaji wa gesi asilia nchini.

Mwakapalila alibainisha kuwa TPDC inatekeleza miradi 19 ya kimkakati, ambapo miradi tisa ipo chini ya Wizara ya Nishati na miradi minne ipo chini ya TPDC, ikiwemo mradi wa gesi ya LNG, bomba la kusafirisha mafuta kupitia mikoa nane, na utafutaji wa mafuta na gesi asilia.

Naye Mwenyekiti wa Kamati ya Maridhiano ya Amani Kinondoni, Majaliwa Selemani, ameishukuru TPDC kwa semina hiyo na kusisitiza umuhimu wa kutunza miundombinu ya gesi asilia, akisema serikali imewekeza gharama kubwa kuhakikisha miundombinu hiyo inasalia salama.

“Serikali imetambua mchango wetu katika jamii, na tunatoa elimu kwa mtu mmoja mmoja kuhusu ulinzi wa miundombinu hii kwa faida yetu sote na Taifa kwa ujumla,” amesema Majaliwa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles