30.2 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

RC Bendera atoa maelekezo Bima ya Afya

Joel-BenderaNa ELIYA MBONEA, MANYARA

VIONGOZI wa Halmashauri ya Wilaya ya Babati, mkoani Manyara, wametakiwa kuhakikisha kaya 40,642 zinajiunga kwenye Mfuko wa Afya ya Jamii (CHF) kabla ya Desemba mwaka huu.

Agizo hilo lilitolewa wilayani hapa juzi na Mkuu wa Mkoa huo, Joel Bendera, alipokuwa akizungumza na wananchi wa Kata ya Duru, Tarafa ya Goroa.

Akizungumza katika mkutano huo, Bendera alisema ili kufikia malengo ya kuwa na asilimia 50 za kaya zilizojiunga na CHF, viongozi wa wilaya hiyo wanatakiwa kutimiza wajibu wao ipasavyo.

“Wilaya ya Babati ina kaya 81,284, hivyo ni wajibu wa viongozi wa wilaya kuhakikisha wanasajili angalau nusu ya kaya hadi ifikapo Desemba mwaka huu.

“Suala la kupewa matibabu pindi mwananchi anapougua halina mjadala ndiyo maana nawaagiza viongozi wa wilaya kufuatilia kwa kina ili tuziwezeshe kaya ambazo hazijajiunga na CHF ili ziweze kujiunga haraka,” alisema Bendera.

Pamoja na hayo, aliwataka pia viongozi wa ngazi za chini kuhakikisha wakazi wao au jamii wanazoziongoza zinajiunga na mfuko huo.

“Nyinyi viongozi wa ngazi za chini, tembeleeni hawa wananchi, muwahamasishe wajiunge na mpango huu ili siku mtakapoondoka kwenye uongozi, wananchi wawakumbuke kwenye eneo la afya,” alisema Bendera.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo, Hamis Malinga, alisema uongozi wa halmashauri hiyo umejipanga kutekeleza agizo hilo kwa kuwa wanajua umuhimu wake.

“Tuna timu nzuri kuanzia ngazi ya vijiji, kata na tarafa na tunaahidi kutimiza agizo hili kwani tumejipanga kupeana mrejesho kila mwezi,” alisema Malinga.

Naye Meneja wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF), mkoani Manyara, Isaya Shekifu, alisema kuboreshwa kwa CHF kutawezesha kila kaya yenye watu sita, kupata matibabu kwa gharama ya Sh 30,000 kwa mwaka.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles