Na MWANDISHI WETU-RUKWA
MKUU wa Mkoa wa Rukwa, Joachim Wangabo amesema ili kukabiliana na ukatili dhidi ya watoto, Serikali haina budi kufanya kazi kwa karibu na viongozi wote wa dini wa madhehebu mbalimbali katika mkoa huo ikiwamo kuwataka kuwa karibu na watoto.
Amesema hali hiyo itawafanya watoto hao wawe huru kuwataarifu viongozi hao aina yoyote ya manyanyaso wanayoyapata wakiwa nyumbani.
Hayo aliyasema jana wakati akitoa salamu za Mwaka Mpya katika ibada ya kuukaribisha mwaka 2020 iliyofanyika Kanisa Katoliki Parokia ya Kristu Mfalme, mjini Sumbawanga.
Alisema kuwa kwa muda mrefu katika mkoa huo watoto wamekuwa wakiathirika kutokana na ugomvi baina ya wazazi na hatimae kutopata mapenzi ya baba na mama.
Wangabo alisema hali hiyo inasababisha watoto hao kutopata malezi mazuri ya kifamilia na hatimae kuishia mitaani na kuwa na kizazi kisichofaa katika jamii na kusisitiza kuwa Serikali ya mkoa imejizatiti kupambana na hali hiyo.
“Chimbuko la maisha yetu wote liko kwenye familia na familia ni watoto, kwahiyo tujielekeze zaidi katika malezi ya watoto wetu, lakini pia kuhakikisha ya kwamba tunawapa na kuheshimu haki zao.
“Haki za watoto tunakwenda kuzifungua kwa watoto wetu wote kama Serikali, tutawaelimisha watoto haki zao, tutawaambia wakifanyiwa manyanyaso waende kwa nani, waripoti kwa nani matatizo hayo.
“Lakini narudi kwa viongozi wa dini na wenyewe tutawaomba wawe karibu sana na watoto ili watoto waweze kufunguka wawaambie manyanyaso wanayoyapata majumbani, nasi tutashirikiana na viongozi wa dini kupambana na hayo manyanyaso na huo ukatili wa watoto,” alisema Wangabo.
Mwishoni mwa mwaka 2019 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Rukwa ulizindua mpango mkakati wa miaka mitano wa kukabiliana na kupambana na mimba za watoto pamoja na kupunguza watoto wa mitaani, ambao utekelezaji wake unaanza mwaka 2020.