NA SHOMARI BINDA
MKUU wa Mkoa wa Mara, Dk.Charles Mlingwa, amewataka wananchi kuwa mstari wa mbele katika kupambana na uhalribifu wa mazingira ikiwamo uhifadhi wa bonde la mto Mara kuwafanya wanyama wanaovuka kupitia mto huo kuendelea kuvuka.
Katika miezi ya Aprili na Mei wanyama wakiwamo nyumbu, pundamilia na paa husafiri kutoka mbunga ya taifa Serengeti nchini na kwenda mbuga za Masai Mara Kenya kutafuta malisho na maji.
Wanyama hao hurudi Tanzania miezi ya Julai na Oktoba kwa kutumia mto Mara, tukio ambalo huonekana kuwa ni muhimu na la historia.
Alikuwa akizungumza na waandishi wa habari katika kuelekea siku ya Mara ambayo huadhimishwa kila Septemba 15 kwa ushirikino wa Tanzania na Kenya. Mwaka huu maadhimisho hayo yatafanyika wilayani Tarime.
RC alisema wananchi wana umuhimu mkubwa wa kushirikishwa katika tukio hilo na uhifadhi wa mazingira.
Alisema umuhimu wa maadhimisho hayo ni kutoa msukumo mkubwa kwa hifadhi ya mto Mara ambao unaanzia katika milima ya Mau nchini Kenya na kuishia ziwa Victoria upande wa Tanzania
Mkuu huyo wa mkoa alisema mto Mara huchangia kwa kiwango kikubwa kuwapo Hifadhi ya Serengeti ambayo ni tegemeo kubwa la pato la taifa na wananchi majirani na hifadhi kutokana na shughuli za utalii.
Alisema ili Hifadhi ya Serengeti iendelee kuwapo na kutambulika katika maajabu saba ya Afrika kuhusu kuhama kwa wanyama, ni muhimu kuhifadhi mazingira ya bonde la Mto Mara na uhifadhi huo ni muhimu kushirikishwa wananchi.
“Maadhimisho ya mwaka huu yatahusisha maonyesho na utoaji elimu ya umuhimu wa uhifadhi wa mazingira ya bonde la mto Mara kwa semina na makongamano, upandaji wa miti kwenye bonde, na haya yote wananchi wanapaswa kushirikishwa.
“Kaulimbiu ya maadhimisho ya mwaka huu ni “Afya ya Mto Mara kwa Maendeleo Endelevu”… lakini hatuwezi kuwa endelevu bila kuwashirikishwa wananchi katika utunzaji wa mazingira,”alisema.
RC alisema serikali ya mkoa ilikwisha kupiga marufuku wachenjuaji wa dhahabu kufanya shughuli zao katika vyanzo vya maji katika mto Mara ili kulinda mazingira yake.