Na Tiganya Vincent, Maelezo
MKUU wa Mkoa wa Tabora, Aggrey Mwanri ameagiza kuanzia msimu ujao wa kilimo kila mtu mwenye uwezo wa kufanyakazi alime heka mbili za alizeti.
Alisema hatua hiyo ni kwa ajili ya kuvutia wawekezaji kujenga viwanda vya kusindika na kuzalisha mafuta hayo kuanza ujenzi mkoani humo.
Alitoa kauli hiyo kwenye maonyesho ya Nanenane Kanda ya Mikoa ya Magharibi yanayofanyika mkoani Tabora.
RC alisema alizeti mkoani Tabora inastawi na ikiwa wakazi wake watalima kwa wingi kampuni mbalimbali zitajitokeza kwa wingi kuja kujenga viwanda vya kuzalisha mafuta hayo.
Alisisitiza kuwa wawekezaji wengi wamekuwa wanashindwa kujenga viwanda vya usindikaji wa mafuta hayo kwa sababu zao hilo limekuwa halitiliwi mkazo na kufanya uzalishaji kuwa wa chini.
Mwanri alisema kwa sasa itakuwa ajenda ya mkoa kama mkakati mojawapo wa kuwavutia watu kuja kujenga viwanda.
“Ndugu zangu wakuu wote wa wilaya na wakurugenzi kuanzia sasa akili yetu na agenda yetu kubwa iko katika kuhakikisha kila mkazi wa Tabora analima hekta mbili za alizeti kuanzia msimu ujao wa kilimo.
“Hii itatuwezesha tuwe na malighafi nyingi kwa ajili ya kulisha viwanda vitakavyoanzishwa kwa mwaka mzima.” Alisema.
Aliwaagiza maofisa ugani wote kuhakikisha wanawatembelea wakulima vijijini kuwaelimisha kilimo bora na mbegu bora za zao hilo.
RC alisema hatua hiyo itawawezesha wakulima kuanza mara moja kilimo hicho mvua ya masika itakapoanza.
Vilevile aliwaagiza wakurugenzi watendaji wote na maofisa ugani wote kuhakikisha wanawahimiza wakazi wa maeneo mbalimbali ya mkoa huo kuanza kilimo cha uwele, mtama, viazi na mihogo.
Alisema hatua hiyo ni katika kukabiliana na upungufu wa chakula kwa sababu ya mvua kuendelea kunyesha chini ya kiwango.