29.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, December 6, 2023

Contact us: [email protected]

RC aonya wawekezaji kutumia madalali

GUSTAPHU HAULE – PWANI

MKUU wa Mkoa wa Pwani, Evarist Ndikilo, amewaonya wawekezaji wa viwanda waliopo mkoani hapa kuacha tabia ya kuwatumia madalali kupata vibali ya ukazi kwani kufanya hivyo ni kinyume na utaratibu uliowekwa na Serikali.

Amesema njia bora na sahihi ya kupata vibali hivyo ni kwenda moja kwa moja Uhamiaji pamoja na Idara ya Kazi na kwamba maeneo hayo watapata vibali sahihi na kwa wakati mwafaka.

Kauli hiyo aliitoa juzi alipokuwa akizungumza na wawekezaji wa kiwanda cha China Boda kilichopo Kibaha –Tamco mkoani Pwani, wananchi na watendaji wa Serikali alipokwenda kuweka jiwe la msingi katika kiwanda hicho.

Alisema kuwa tabia ya kuwatumia madalali kupata vibali vya ukazi inawachukua muda mrefu kuvipata, lakini pia inawafanya kuibiwa fedha nyingi pasipo kupata mafanikio jambo ambalo linaleta usumbufu kwa wawekezaji.

“Acheni kutumia madalali kupata vibali maana watu hao si sahihi kwenu, mmekuwa mkipigwa fedha nyingi bila sababu na wakati mwingine hata mkitoa fedha hizo hampati vibali hali ambayo inaleta kero katika kufanikisha malengo yenu ya uwekezaji,” alisema Ndikilo.

Katika hatua nyingine, Ndikilo aliomba Shirika la Maendeleo ya Taifa (NDC),  ambao ndio wamiliki wa eneo la Tamco lenye ukubwa wa zaidi ya ekari 230 kuhakikisha wanasimamia kikamilifu ili wawekezaji waliopewa viwanja katika eneo hilo waweze kujenga viwanda kwa wakati.

Alisema kuwa hakuna sababu ya watu kupewa viwanja halafu wanavikumbatia kwa muda mrefu bila kuviendeleza, huku akisema ni vyema kama wameshindwa wanyang’anywe ili wapewe wawekezaji walio tayari kuwekeza kwa kujenga viwanda.

Aliwataka watendaji mbalimbali wa Serikali kuendelea kushirikiana na wawekezaji waliopo maeneo yao kuhakikisha wanafanikiwa kuwekeza kwa kujenga viwanda vyao kwa wakati.

Mkurugenzi wa kiwanda cha China Boda kinachoshughulika na uchakataji wa betri, Chen Tianhai, alisema kiwanda hicho kilianza kujengwa mwaka juzi na uzalishaji wake ulianza Januari mwaka huu, lakini upanuzi wake mkubwa utakamilika 2023.

Tianhai alisema bidhaa zinazotengenezwa kiwandani hapo zitauzwa Afrika na kwamba ameiomba Serikali kutoa kibali kwa kiwanda hicho ili kiweze kununua betri chakavu nchini kote.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
580,000SubscribersSubscribe

Latest Articles