Florence Sanawa, Mtwara
MKUU wa Mkoa wa Mtwara, Gelasius Byakanwa, amesikitishwa na mafundi ujenzi wa shule kongwe zinazokarabatiwa mkoani humo, kwa alichosema wanafanyakazi bila kuwa na mpango kazi hali ambayo inawakwamisha wasimamizi kufatiliaji ujenzi wa shule hizo.
Akizungumza wakati wa ziara yake aliyoifanya katika Shule ya Sekondari ya Wasichana Mtwara, Chuo cha Ualimu Mtwara Ufundi na Chuo cha Ualimu Mtwara, alisema kukosekana kwa mpango kazi kumesababisha miradi hiyo kukosa miongozo ili kazi hizo ziweze kukamilika kwa wakati.
Alisema kuwepo kwa mipango kazi kutaleta picha itakayoonyesha miradi hiyo lini ilianza lini na ipo Katika hatua gani na inaisha lini.
“Naomba mnielewe unapofanyakazi bila kupewa mpango kazi hiyo itabaki hadithi, hatuwezi kukamilisha kwa wakati ujenzi huu mbaya zaidi hatujui vyuo na shule vinafunguliwa lini, hili ni tatizo.
“Serikali ya awamu ya tano imetoa zaidi ya Sh bilioni 2 kwaajili ya ukarabati wa shule kongwe lazima hatua zichukuliwe kwa kuona mipango kazi itakayosaidia kumalizika haraka kwa ujenzi huu kwakuwa hatujui siku wala saa ambayo shule na vyuo vitafunguliwa.
“Mfano hii shule ya Wasichana Mtwara ujenzi wake unasimamiwa na Jeshi la Magereza, dhamana hii ni kubwa tunaamini wataigawanya kazi na utafanyika kwa ufasaha zaidi kwakuwa wanazo nguvu kazi ya kutosha ambayo itawezesha ukarabati wa kutosha hawatatuangusha,” alisema Byakanwa
Mkuu wa Shule ya Wasichana Mtwara, Sikujua Anangisye, alisema shule ilijengwa mwaka 1952 hivyo ukarabati wake umekuja wakati sahihi.
“Kutokana na kuongwe wa shule miundombinu mingi inahitaji ukarabati hasa kwenye majengo yenyewe, milango, mabati na vyoo havipo kwenye mazingira rafiki” alisema Anangisye