29.3 C
Dar es Salaam
Thursday, June 1, 2023

Contact us: [email protected]

RC ahimiza utunzaji miradi inayofadhiliwa na GGML

Na Mwandishi Wetu, Geita

Mkuu wa Mkoa wa Geita, Mhandisi Robert Gabriel ameeleza kuridhishwa na miradi ya Kampuni ya Geita Gold Mining Ltd.(GGML) inayotekelezwa kupitia mpango wake wa uwajibikaji kwa jamii katika halmashauri ya Wilaya ya Geita.

Pia amewataka wananchi kuunga mkono jitihada za Kampuni na Serikali katika kulinda miradi hiyo ili kufanikisha lengo la kuwapatia wananchi maendeleo.

Mhandisi Gabriel alitoa sifa hizo kwa GGML katika ziara ya siku saba kwenye halmashauri ya Wilaya ya Geita baada ya kutembelea zaidi ya miradi 45 inayohusisha shule za sekondari za Buyangu, Nyalwanzaja, Kamena, Nyamalimbe, Butobela, Bukoli, Nyaluyeye, Nyarugusu, Nyakamwaga, Busanda, Kaseme, Magenge na Lwamgasa.

Ziara hiyo imehusisha pia zahanati za Nyabulolo, Kamena, Bujula, Bukoli, Busolwa na Nyakamwaga. Miradi yote hiyo imetekelezwa kwa udhamini wa Kampuni ya GGML kupitia mpango wake wa kusaidia jamii.

“Hizi ni jitihada kubwa zinazofanywa na GGML kwa kushirikiana na Serikali kuhakikisha halmashauri ya Wilaya ya Geita na nyingine kwenye Mkoa huu zinasimamia utekelezaji miradi yenye tija inayonufaisha wananchi na kuwapatia maendeleo,” alisema.

Mhandisi Gabriel aliitaka Halmashauri ya Wilaya ya Geita kutumia zaidi mapato ya ndani ili fedha za wajibu wa Kampuni kwa Jamii (CSR) kutoka GGML zianzishe miradi mipya inayojitegemea.

Mkuu huyo wa mkoa pia ameeleza kuridhishwa na ubora na viwango vya miradi inayofadhiliwa na GGML kupitia fedha za wajibu wa Kampuni kwa Jamii (CSR) katika Halmashauri ya Wilaya ya Geita.

Pia aliitaka kampuni hiyo kuendelea kufadhili utekelezaji wa miradi yenye manufaa kwa jamii hususan ile inayozunguka mgodi.

GGML imekuwa kinara wa uwekezaji kwenye jamii tangu kuanzishwa kwake mwaka 2000 na kufikia mwaka 2014/15 Kampuni hiyo iliongeza kiwango chake cha uwekezaji kwenye miradi ya kijamii kwa kiasi kikubwa sana.

Tangu kuanzishwa kwake GGML imewekeza zaidi ya shilingi bilioni 60 za Kitanzania kwenye jamii ya Geita ambapo vipaumbele vikuu vimekuwa ni miradi ya elimu, afya, maji, barabara, miradi ya kukuza kipato na miradi mingine mingi ya kijamii ili kuhakikisha jamii mwenyeji inapata maisha bora.

Aidha, GGML imekuwa ikiendelea kushirikiana na Serikali kutekeleza miradi katika maeneo mengine mbali na halmashauri za Geita Mji na Wilaya ya Geita.

Miradi hiyo ni pamoja ufadhili wa miradi ya kijamii katika halmashauri za Chato, Mbogwe na Bukombe.

Kutokana na utendaji wake, hivi karibuni GGML iliibuka mshindi wa jumla wa kampuni zinazofanya vizuri kwenye sekta ya madini nchini kwa mwaka 2019/2020.

Maeneo mengine ni katika vipengele vya Wajibu wa Kampuni kwa Jamii, utunzaji mazingira na usalama, ukusanyaji wa mapato ya Serikali (kodi) pamoja na uwezeshaji wa wazawa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
213,225FollowersFollow
568,000SubscribersSubscribe

Latest Articles