MCHEZAJI wa timu ya taifa ya Hispania na Real Madrid, Sergio Ramos, anatarajia kukosa mchezo wa kimataifa dhidi ya Romania utakaochezwa Jumanne hii, kutokana na kusumbuliwa na maumivu ya goti aliyopata kwenye mchezo wa kirafiki dhidi ya Italia.
Beki na nahodha huyo wa timu ya Madrid alilazimika kutolewa nje kipindi cha kwanza kutokana na maumivu hayo na kushuhudia timu yake ikitoka sare ya bao 1-1 dhidi ya Italia.
Kwa mujibu wa Shirikisho la Soka la Hispania (FA), mchezaji huyo ameondoka kwenye kambi ya timu hiyo Ijumaa iliyopita kutokana na majeraha hayo.
Beki huyo wa kati alilazimika kuondolewa kwenye kambi hiyo na kurudi Hispania kwa uchunguzi zaidi, huku timu hiyo ikiendelea kujiandaa kuvaana na Romania.
Hata hivyo, Madrid itakuwa na hamu ya kuona beki huyo anarejea uwanjani mapema akiwa yupo fiti kabla ya mchezo wao wa El Clasico dhidi ya Barcelona, utakaochezwa Jumamosi ijayo.