29.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, October 20, 2021

RAIS ZUMA KUWASILI NCHINI KESHO

RAIS wa Afrika ya Kusini, Jacob Zuma

 

PATRICIA KIMELEMETA – Dar es Salaam

RAIS wa Afrika ya Kusini, Jacob Zuma, anatarajiwa kuwasili nchini kesho kwa ziara ya siku tatu.

Katika safari hiyo atafuatana  na wafanyabiashara 80 kutoka nchini kwake.

Akizungumza na waandishi wa habari   Dar es Salaam jana, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Dk.Augustine Mahiga, alisema ziara hiyo itatoa fursa kwa viongozi wakuu wa nchi hizo mbili kujadili masuala mbalimbali yanayohusu uwekezaji na biashara.

Alisema  akiwa nchini, Rais Zuma atasaini mikataba mitano ya ushirikiano ambayo ni pamoja na hati ya makubaliano ya ushirikiano katika masuala ya Bioanuwai na uhifadhi kati ya   Tanzania na Afrika ya Kusini.

Mkataba mwingine ni ushirikiano katika sekta ya maji na sekta ya uchukuzi.

“Kuna baadhi ya mikataba bado tunaifanyia kazi,   baada ya kukamilika  mawaziri wa sekta husika wataisani.

“Mikataba hiyo ni pamoja na sekta ya utalii, habari, kilimo, afya na mengine, lakini tunaamini  baada ya kusainiwa, kutakuwa na mabadiliko ya  maendeleo,”alisema Mahiga.

Akitoa mfano, alisema Afrika ya Kusini imepiga hatua kwenye kilimo cha umwagiliaji na uvunaji wa maji ya mvua.

Mahiga alisema  Watanzania wanapaswa kuelimishwa jambo hilo waweze kubadili mfumo wa shughuli za kilimo kwa kutumia umwagiliaji kuliko hivi sasa ambako wakulima wanatumia kilimo cha mvua za msimu bila ya uvunaji wa maji.

Baada ya kusaini makubaliano hayo, Rais Zuma atatembelea Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH)  kuangalia shughuli za matibabu  katika taasisi hiyo ambayo inachukua wagonjwa kutoka ndani na nje ya nchi.

Rais huyo  wa Afrika Kusini pia atazindua jengo jipya la ubalozi wa Afrika ya Kusini lililopo Posta.

Balozi Mahiga alisema licha ya uwekezaji, Tanzania na Afrika ya Kusini zina uhusiano wa undugu tangu wakati wa harakati za kuondoa utawala wa ubaguzi kupitia Chama Cha African National Congress (ANC) cha Afrika ya Kusini chini ya mwasisi wa chama hicho, Hayati Nelson Mandela.

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

66,457FansLike
162,594FollowersFollow
522,000SubscribersSubscribe

Latest Articles