‘RAIS ZUMA KUHAMIA DUBAI’

0
494

PRETORIA, AFRIKA KUSINI


KASHFA mpya kuhusu Rais Jacob Zuma imezuka nchini hapa ikidaiwa kiongozi huyo aliyekumbwa na mlolongo wa kashfa amepanga kuhamia Dubai.

Barua pepe zilizochapishwa na gazeti moja nchini hapa zinaonesha uwapo wa uhusiano mkubwa kati ya Zuma na familia yenye utata ya Kiasia ya Gupta hususan kuhusu madai kuwa anapanga kuhamia Dubai.

Wakati chama tawala nchini Afrika Kusini ANC kinakumbwa na vita vya ndani kwa ndani, barua pepe hizo zinatarajia kuibua mjadala mkali kuhusu tuhuma hizi mpya za ‘kutoroka’.

Barua pepe hizo baina ya mwanawe Zuma, Duduzane, na vigogo wa kampuni inayomilikiwa na familia tatanishi ya Gupta, zinashirikisha barua moja iliyotumwa kwa familia ya kifalme nchini Dubai, ambapo Zuma anasema angetaka kuwa na makao ya pili.

Madai hayo yanaibua mjadala wa iwapo Rais Zuma anajiandaa kubwaga manyanga kwani chama cha ANC kinaonekana kumgeuka.

Msemaji wa rais amepuuza barua pepe hizo kama uvumi na uchokozi.

Kwa sasa kuna kesi inaendelea katika Mahakama ya Katiba ya iwapo wabunge wa Afrika kusini wapige kura ya siri ya kutokuwa na imani na Rais Jacob Zuma.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here