24.8 C
Dar es Salaam
Friday, June 2, 2023

Contact us: [email protected]

RAIS WETU TUFIKISHE KWENYE UMOJA WA KITAIFA


Na Askofu Stephen Munga  |

TAIFA letu limegawanyika katika misingi ya ushabiki wa vyama vya siasa. Itikadi za vyama zinalimega Taifa letu na tunaelekea kukubali hilo. Asiyeona kwamba tumegawanywa na tukagawanyika ni mnafiki na adui mkubwa wa Taifa hili. Ukweli na uhalisia ni kwamba sisi ni wamoja si vinginevyo. Inauma sana kwamba kila anayezungumza juu ya Taifa letu wakati huu anaonekana ama anaunga mkono chama hiki cha siasa au chama kile. Hatupendi kuwa taifa la wasiojielewa.

Hii ni dhana potofu inayoendelezwa na kudekezwa pasipo sababu za msingi. Hatuwezi kukaa kimya ilhali tunaona mgawanyiko wa taifa letu. Tunaipenda nchi yetu na tunaitakia amani. Tunaipenda nchi yetu na wala si kwa unafiki. Wakati mwingine inaelekea kama nchi hii imejaza wanafiki lukuki ambao hawalitakii taifa hili mafanikio ya dhati bali wanalinda masilahi yao binafsi. Inafika mahali hata Serikali ikifanya mambo ya manufaa kwa nchi hatuoni kwa sababu tumevaa miwani ya kuligawa taifa. Inafika mahali hata vyama vya upinzani vinapotoa hoja ya manufaa kwa taifa hatuoni kwa sababu tumegawanyika.

Heri kama tungesimama katika misingi ya Katiba tuliyo nayo sasa ya nchi yetu tungeweza kuliponya taifa letu. Tanzania ni kubwa kuliko mtu mwingine awaye yeyote, ukubwa wake umo katika misingi ya Katiba yetu. Ni sisi Watanzania wenyewe ambao tuna wajibu wa kumkataa yeyote anayejaribu kutugawa na kulipeleka taifa katika maangamizi. Sisi ni Watanzania na hatuhitaji kitu kingine zaidi ya kuwa Watanzania. Sisi ni taifa moja. Sisi ni Watanzania na hatutaki vinginevyo. Tunahitaji taifa lililounganishwa kwa ajili ya maendeleo, usalama na amani ya taifa letu.

Tunapomchagua mmoja wetu kuwa Rais kwa mujibu wa Katiba tunatazamia kwamba kiongozi huyo ataona umuhimu wa kuliunganisha taifa ili liweze kuwa salama na kutuletea maendeleo. Kwa sasa hivi Rais wetu ni Dk. John Magufuli, yeyote asiyekubali hili anajidanganya na hatukubaliani naye. Tunataka nchi hii iwe salama na tunataka Rais iliyeko madarakani alivushe taifa hili salama mpaka mwisho wa kipindi chake cha utawala kama ilivyokuwa kwa viongozi waliotangulia.

Hatuwezi kumhujumu Rais kwa namna yeyote kwa sababu tumempa dhamana hii ya kuliongoza taifa hili, yeyote anayekusudia kumhujumu Rais anajihujumu nafsi yake. Watanzania tunataka mafanikio na ni wajibu wa Rais wa nchi kuona kwamba taifa linafanikiwa. Hata sasa katika hali tulimo macho yetu yanamtazama Rais wetu alilete taifa la Watanzania pamoja kwa ajili ya usalama, amani na maendeleo ya nchi yetu. Nitasimama na Rais wangu pale anapoyafanya hayo kwa misingi ya haki na kwa mujibu wa Katiba ya nchi. Pale itakapokuwa hafanyi hayo ya kuliunganisha taifa nitasema wazi kwamba hafanyi sawa. Rais ni wa Watanzania wote na anapochaguliwa anakuwa hivyo kwa misingi ya Katiba yetu. Urais si chama bali ni suala la taifa na umoja wake.

Naomba nijieleze kwa kifupi kama alivyokuwa akifanya Mtume Paulo katika Biblia, kuhusu uraia wangu mimi ni Msambaa wa koo za Kikilindi tuliokuwa machifu wa kabila hilo. Wakati Baba wa Taifa Mwl. Julius Nyerere anatengeneza umoja wa kitaifa tulikubali juhudi zake na kuachilia uchifu ili tujenge taifa huru la Tanzania lililo na umoja wa nguvu. Hata hivyo, muhimu zaidi ni kwamba mimi ni Mtumishi wa Kristo na wakili wa siri za Mungu. Ninachodaiwa na Bwana wangu ni kwamba niwe mwaminifu. Nimejitahidi kwa neema ya Kristo kutokuwa mnafiki. Kitaaluma mimi ni mtheologia na mwanafalsafa. Ni mhadhili wa vyuo vikuu nikifundindisha lakini pia nikifanya uchungaji kama wito wangu. Nimepambana na miamba mingi kitaaluma katika sehemu mbalimbali duniani na sijawahi kutetereka katika misimamo yangu. Kwa kuwa ningali naishi bado nitaendelea kupambana katika taaluma yangu na imani yangu katika Kristo. Kwa kawaida najijua kwamba kitaaluma na kiimani si mtu mwepesi kuyumbishwa. Nimeyafanya hayo kwa kutegemea neema ya Mungu na nikijua kwamba Bwana wangu atanidai vingi kwa sababu amenipa upeo wa juu wa elimu.

Mtazamo wangu ni kwamba Tanzania iliyo bora ni kwa vizazi vya sasa na vile vijavyo. Uwepo wa Tanzania hautegemei uwepo wa vyama vya siasa vilivyopo bali hutegemea uwepo wa Watanzania walio na upenzi na nchi yao. Mimi najitangaza kuwa ni mmoja wapo wa wale walio na upenzi na nchi yao. Sina kadi ya chama chochote cha siasa bali nina kitambulisho cha Mtanzania tu basi. Mimi ni mtu mdogo sana ambaye Rais akitaka kichwa changu katika kombe, (kama Herode alivyotaka kichwa cha Yohana Mbatizaji) hakika atapelekewa kichwa changu. Lakini najua jambo moja kwamba nikisimamia kweli na haki kule mbinguni nitakaa na wateule ambao Mungu amewaheshimu. Tusitukane wakunga na uzazi ungalipo. Sipendi kuwa miongoni mwa wanafiki kwa Rais wangu. Hakuna mtu mwingine yeyote anayeweza kuliunganisha taifa hili kwa dhati zaidi yako Rais wetu.

Rais, unganisha taifa hili ili mihimili ya utawala, Mahakama na Bunge ifanye kazi zao kwa mujibu wa Katiba ya nchi. Kuilinda Katiba ya nchi ni kiapo ulichoweka wakati tulipokuwa tunakukabidhi kuliongoza taifa hili. Rais, kelele zote unazosikia ni kilio cha Watanzania wanaotamani uunganishe taifa letu kwa dhati. Tunatamani kukuona wewe kama alama ya umoja wa kitaifa na wala si shabiki wa chama cha siasa. I humbly beg you, your highness, Mr. president, unite our nation!

Tunajua kwamba wewe umeingia madarakani kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi -CCM lakini tangu ulipokuwa Rais tumekutambua kama kiongozi wa nchi. Unayo hekima ya kutosha kwa mujibu wa Katiba ya nchi kutembea na kofia mbili: kuwa kiongozi wa nchi na kuwa kiongozi wa chama pasipo kuamsha hisia hasi za umoja wa kitaifa. Watanzania tumeona hivyo katika awamu zote za utawala na kamwe haijawahi kuligawa taifa hili. Nirudie tena kusema kwamba kichwa changu katika kombe chaweza kuwa sadaka yako ya manukato mbele za Mungu ikiwa kwa dhamiri safi utaona kwamba nimekukosea. Tena ikiwa utaona ni sawa kuhojiwa na mamlaka ambazo ziko chini yako juu ya haya ninayosema, basi sitakuwa na hiari. Hata hivyo, sitakuwa na jingine la kusema zaidi ya kwamba unganisha taifa letu kwa ajili ya ustawi na usalama wake na kamwe sitakuwa mnafiki katika hili. Nitaendelea kukupenda na kukutambua kuwa ni Rais wetu na nitaendelea kukuombea kama nilivyokuwa nikifanya siku zote. Mungu akubariki sana. Mungu ibariki Afrika, Mungu ibariki Tanzania.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
213,268FollowersFollow
568,000SubscribersSubscribe

Latest Articles